Simba malizieni kazi  Caf kwa JS Saoura

04Mar 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba malizieni kazi  Caf kwa JS Saoura

WAWAKILISHI pekee wa Afrika Mashariki na Kati katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba wanaondoka jijini Dar es Salaam kesho kuelekea Algeria kwenye mechi yao ya hatua ya makundi dhidi ya JS Saoura.

Mechi hiyo ya marudiano ya Kundi D,  itakayopigwa Jumamosi Machi 9, mwaka huu, inatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na nafasi ya timu hizo katika kundi lao hilo linalozijumuisha pia Al Ahly ya Misri na AS Vita ya DR Congo.

Simba iliyopo nafasi ya pili ikiwa na pointi sita, moja nyuma ya vinara Al Ahly na moja mbele ya JS Saoura, endapo itashinda mechi hiyo inaweza ikawa imefunzu robo fainali kutegemeana na matokeo dhidi ya timu hiyo ya Misri na AS Vita inayoburuza mkia ikiwa na pointi nne.

Kimahesabu endapo AS Vita, itapoteza nyumbani dhidi ya Al Ahly ama kutoka sare na kisha Simba ikashinda, moja kwa moja timu hiyo ya Tanzania itakuwa imefuzu kutokana na kufikisha pointi tisa ambazo zinaweza kufikiwa na timu hiyo ya Misri pekee.

Ikumbukwe katika hatua hii ya makundi, kila kundi kutoka manne, linatoa timu mbili zitakazotinga robo fainali, hivyo Simba inatakiwa kushinda, huku ikiombea AS Vita ipate matokeo mabaya dhidi ya Al Ahly.

Aidha, kushinda kwa Simba kutaiondolea kucheza kwa presha katika mechi ya mwisho nyumbani dhidi ya AS Vita, hivyo kinachotakiwa sasa ni kumaliza mchezo huo ikiwa ugenini, Algeria.

Tunaamini kama Simba itacheza kwa kiwango ilichokionyesha dhidi ya Al Ahly Uwanja wa Taifa na kisha kwenye Ligi Kuu dhidi ya Yanga, African Lyon, Azam FC, Lipuli na Stand United, inaweza kushangaza kwa kushinda mechi yake ya kwanza ugenini katika mashindano hiyo.

Kinachotakiwa kwa viongozi wa Simba na benchi la ufundi ni kuwaandaa wachezaji kisaikolojia zaidi kwa kuwaaminisha kwamba inawezekana kushinda ugenini.

Hata hivyo, kinachoonekana kwa wachezaji wa Simba ni kucheza pasipo kujiamini pindi wanapokuwa ugenini kwenye michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Hivyo, wakati huu benchi la ufundi likiwa limeongezewa nguvu kufuatia uongozi kumleta Denis Kitambi kuwa msaidizi wa Kocha Mkuu, Mbelgiji Patrick Aussems, tunaimani watashirikiana vema kuleta matokeo chanya.

Tanatambua tangu ilipofungwa mabao 3-0 dhidi ya Simba, JS Saoura haijapoteza tena mechi yoyote ile ikicheza nyumbani au ugenini.

Imevuna jumla ya pointi tano kutokana na kutoka sare ugenini dhidi ya AS Vita na kisha kuichapa ikiwa nyumbani, huku pia ikitoka sare dhidi ya Al Ahly nyumbani.

Lakini hilo, halitutii hofu kwa Simba, kwa kuwa ilishacheza na timu hiyo na kuifunga, hivyo tunaamini inajua uchezaji wao na haina sababu ya kuwaogopa wapinzani wao hao.

Viongozi wa Simba, benchi la ufundi na wachezaji wanapaswa kusahau matokeo yaliyopita na kuichukulia mechi hiyo kama fainali ya wao kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

Katika mechi hiyo, pamoja na Simba kutakiwa kumheshimu mpinzani wake, inatakiwa kuingia uwanjani ikitambua kuwa inahitaji matokeo mawili tu kwenye mechi hiyo, kushinda au ikishindikana kabisa angalau sare.

Ni kweli tunatambua katika michuano hii hutawaliwa na fitina nyingi nje na ndani ya uwanja, hivyo viongozi na benchi la ufundi wanapaswa kujiandaa kwa kila kitu.

Hata hivyo, hatuna shaka sana katika hilo kutokana na ukweli kuwa klabu ya Simba wanatambua kuwapo kwa mbinu hizo chafu, ila tunasisitiza umakini zaidi ikiwa ni pamoja na wachezaji kuaswa kucheza kwa kutomtegemea zaidi mwamuzi. Tunaitakia Simba kila la kheri katika kuipeperusha bendera ya Taifa katika michuano hii.

Habari Kubwa