Simba, Mtibwa zijiandae kisaikolojia ugenini Caf

03Dec 2018
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Mtibwa zijiandae kisaikolojia ugenini Caf

WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika michuano ya kimataifa Simba na Mtibwa Sugar, baada ya wiki iliyopita kuanza vema kampeni zao kwenye raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, kesho zitashuka tena dimbani.

Mtibwa inayoiwakilisha Tanzania Bara kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, ilikuwa ya kwanza kuonyesha nyota njema kwenye michuano hiyo baada ya Jumanne iliyopita kuichapa Northern Dynamo ya Shelisheli kwa mabao 4-0 kwenye mchezo mkali uliopigwa Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.

Simba ilifuata kwa kujibu mapigo baada ya kuichapa Mbambane Swallows ya Swaziland kwa mabao 4-1, katika mechi yakuvutia iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kesho timu hizo zitashuka dimbani ugenini huko Swaziland na Shelisheli kusaka sare ama ushindi wowote ili kuweza kusonga mbele kwenye michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.

Ingawa kwa mtazamo wa mashabiki wa Mtibwa na Simba, kama si Watanzania kwa ujumla, wanaamini kazi imekwisha, sisi Nipashe tunaamini shughuli hiyo si rahisi kwa namna hiyo.

Matokeo ya soka yanaweza kupinduliwa wakati wowote, hivyo Mtibwa na Simba hazina budi kushuka uwanjani kwa tahadhari kubwa, huku zikiwaheshimu wapinzani wao.

Tayari kocha wa Mbambane Swallows, Kihna Phiri, alishaeleza kwamba anaamini wanaweza kupindua matokeo na kushinda. Na si kushinda tu, bali Phiri alifafanua kuwa ni ushindi utakaowawezesha kusonga mbele katika hatua inayofuata.

Ili Mbambane Swallows iweze kusonga mbele, inapaswa kushinda kwa mabao 3-0 ama zaidi. Ingawa wengi wanaona ni vigumu, lakini Nipashe kama mdau mkongwe wa soka hapa nchini, tunaamini hilo linawezekana.

Tunasema hivyo si kwa sababu tu Phiri amejiaminisha kikosi chake kinaweza kupindua matokeo mechi ya marudiano nyumbani, la hasha.

Kauli yetu hiyo inatokana na uimara wa kikosi chake na rekodi ya Mbambane Swallows ilipopindua matokeo dhidi ya Azam FC kwenye Kombe la Shirikisho Afrika Machi 19, mwaka jana.

Azam FC ikiwa nyumbani iliichapa Mbambane Swallows kwa bao 1-0, hata hivyo haikuamini kilichotokea mechi ya marudiano baada ya kuchapwa 3-0 na kurudi nchini na visingizio kibao.

Sote tunajua kuwapo kwa mbinu nyingi za ushindi nje na ndani ya uwanja hususan kwa soka la Afrika ambalo hutawaliwa na ujanja- ujanja kibao.

Lakini hayo ni mambo yanayoeleweka na Simba pamoja na Mtibwa zinalifahamu hilo, hivyo hazina budi kujipanga na kujiandaa kisaikolojia kuelekea mechi hizo za marudiano ugenini.

Mbambane Swallows inaelezwa kuwa haitofautiani kimbinu nje na ndani ya Uwanja na timu za Uarabuni, hivyo Simba inapaswa kuchukua tahadhari mapema.

Hatutarajii na wala halitatuingia akilini kusikia matokeo ya Simba na Mtibwa yamepinduliwa na kutolewa nje ya michuano hiyo, huku zikitoa visingizio vya 'fitina nje na ndani ya uwanja' kwa kuwa hivi ni sawa na 'vita' hazina budi kujipanga kwa kina namna.

Mwisho tunazitakia kila la kheri Simba na Mtibwa kesho.

 

 

Habari Kubwa