Simba, Namungo zikipania fainali Afrika inawezekana

27Feb 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Namungo zikipania fainali Afrika inawezekana

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano mikubwa na inayoongoza kwa utajiri barani Afrika kwa ngazi ya klabu, Simba na Namungo wameonyesha cheche na kwa kuwashtua wapinzani wao katika mashindano Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Simba ambayo inaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, tayari imeshinda mechi zake mbili za hatua ya makundi, hivyo kuongoza Kundi A mbele ya Al Ahly ya Misri na AS Vita ya DR Congo zenye pointi tatu kila moja huku Al-Merrikh ya Sudan ikiburuza mkia baada ya kupoteza mechi zake mbili za mwanzo.

Aidha, Simba imeonyesha inaweza kufika mbali kwani mbali na kumfunga bingwa mtetezi wa michuano hiyo, Al Ahly kwa bao 1-0 zilipokutana hapa nchini, pia iliibuka na ushindi kama huo ikiwa ugenini DR Congo dhidi ya AS Vita katika mechi yake ya kwanza.

Kadhalika, Simba ndiyo timu pekee katika michuano hiyo kushinda mechi zote mbili za mwanzo, lakini ikiwa miongoni mwa timu nane ambazo hazijaruhusu nyavu zake kutingishwa katika hatua ya makundi msimu huu.

Ushindi huo na rekodi hiyo huku ikiwa moja ya timu iliyoonyesha kiwango cha juu hadi sasa, ni wazi kama wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wa klabu hiyo wataendelea kuwa kitu kimoja na malengo yao yakiwa ni kufika fainali, tunaamini hicho ni kitu kinachowezekana.

Hakuna ubishi kuwa Simba kwa sasa inaonekana kukamilika kila idara na imesheheni wachezaji wenye vipaji ambao wanaweza kuamua matokeo wao binafsi wakati pindi mipango, mbinu na ufundi wa kocha unapokwama uwanjani, jambo ambalo linatufanya kuamini timu hiyo inaweza kufika fainali kama tu dhamira na kiu hiyo itaingia akilini mwa wachezaji.

Na kwa upande wa Namungo ambayo inaipeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, tayari imetinga hatua ya makundi baada ya kupata matokeo ya jumla ya mabao 7-5 katika mechi mbili za mchujo dhidi ya CD de Agosto ya Angola.

Kwa Namungo kufika tu hatua hiyo, ni mafanikio makubwa kwake, kwani tayari imeweka rekodi kwa kuwa klabu ya kwanza Tanzania kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza na kufanikiwa kufika hatua ya makundi.

Lakini kuitoa timu kongwe kama De Agosto, huo ni ujumbe tosha kwa wapinzani wao kwenye hatua ya makundi kujiandaa vizuri kabla ya kukutana wakati huu Namungo ikijiandaa kwenda Morocco kuivaa Raja Casablanca Machi 10, mwaka huu.

Namungo ambayo ipo Kundi D pamoja na Raja Casablaca ya Morocco, Pyramids (Misri) na Nkana ya Zambia, kwa hakika ni moja kati ya kundi gumu na lenye timu kongwe na zoefu kwenye michuano hiyo ya Afrika.

Ingawa halitakuwa kundi jepesi kwake kuweza kufurukuta, sisi tunaamini hakuna kinachoshindikana uwanjani kama wachezaji na benchi la ufundi la Namungo watajipanga huku uongozi ukihakikisha unamaliza masuala yote ya nje ya uwanja.

Tunapata imani zaidi kwa Namungo kuweza kufanya vizuri na kufika mbali hasa tukitumia kigezo cha kuweza kuibuka na ushindi wa mabao 6-2 katika mechi ya kwanza dhidi ya De Agosto, timu ambayo ni kongwe na kigogo katika michuano hiyo ya Afrika, hivyo huu ni mwaka ambao Watanzania wanatarajia mafanikio makubwa kwenye michuano hiyo ya CAF kutoka kwa timu hiyo pamoja na Simba.

Habari Kubwa