Simba, Yanga na Azam kwa hili, sasa badilikeni

18Jan 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Yanga na Azam kwa hili, sasa badilikeni

TAYARI hata kabla raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara haijamalizika, tumeshuhudia miamba ya soka nchini, klabu za Yanga, Simba na Azam zikivunja mabenchi yao ya ufundi, kama si kuachana na makocha wakuu, kwa sababu mbalimbali.

Yanga ilianza msimu ikiwa na Kocha Mkuu, Mkongomani Mwinyi Zahera akisaidiwa na Mzambia Noel Mwandila kabla ya Novemba mwaka jana benchi nzima la ufundi kuvunjwa na makocha hao kutimuliwa.

Makocha hao walitimuliwa baada ya kushindwa kuiwezezesha timu hiyo kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kile kilichoelezwa kuwa ni kutounda timu ya ushindani kutokana na kushindwa kukiunganisha kikosi.

Kwa upande wa Simba, nayo ilianza msimu na aliyekuwa kocha wao, Mbelgiji Patrick Aussems akisaidiwa na Mrundi Masoud Juma kabla ya kumkataa msaidizi huyo na kisha kuletewa Dennis Kitambi.

Hata hivyo, licha ya kutolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, kushindwa kuunda timu ya ushindani na kudhibiti nidhamu ya wachezaji kilielezwa ni sababu tosha ya uongozi wa Simba kuamua kumtimua Mbelgiji huyo na kisha kufikia makubaliano ya kuachana na msaidizi wake, Kitambi.

Azam FC, yenyewe ilianza msimu na Mrundi Etienne Ndayiragije akisaidiwa na Iddi Cheche, lakini ilifikia makubaliano ya kuachana naye baada ya Shirikikisho la Soka nchini (TFF), kuhitaji huduma yake timu ya Taifa, Taifa Stars.

Kwa sasa Yanga, iliyokuwa ikinolewa na Kaimu Kocha Mkuu, Boniface Mkwasa, imemuajiri Mbelgiji Luc Eymael kuwa kocha mkuu, huku ikiwa katika mazungumzo na Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime ikimtaka akawe kocha msaidizi.

Na Simba inanolewa na Mbelgiji mwingine, Sven Vandenbroeck akisaidiwa na Selemani Matola ambaye aliajiriwa baada ya Aussems kutimuliwa. Azam FC, baada ya kuachana na Ndayiragije iliamua kumrejesha aliyekuwa kocha wake wa zamani, Mromania Aristica Cioaba, ambaye ameendelea kusaidiwa na Cheche.

Kwa mtiririko huo, inaonyesha wazi uamuzi wa nani awe kocha msaidizi bado ni jukumu la uongozi wa klabu hizi tatu na kocha mkuu hana nafasi ya kupendekeza nani awe msaidizi wake kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia kwa klabu na timu za taifa za wenzetu waliopiga hatua kisoka.

Ikumbukwe Maxime, alianza kuhusishwa na Yanga kabla hata ya Eymael kutua katika klabu hiyo, hivyo, pendekezo hilo ni wazi hayo ni matakwa ya uongozi wa klabu kumwajiri na si chaguo la kocha mkuu kumtaka awe msaidizi wake.

Nipashe tunatambua, uongozi wa klabu hizi tatu, umekuwa msatari wa mbele katika kuajiri makocha na kuwatimua kwa sababu ya kutopata matokeo wanayoyataka, lakini tunashangazwa na namna makocha hao wasivyopewa nafasi ya kufanya maamuzi hayo muhimu kwao.

Tunatambua kocha mkuu wa klabu ya soka, ni lazima apendekeze msaidizi wake ambaye anaamini anaweza kufanya naye kazi pamoja wote wakiamini katika falsafa moja ili kutotofautiana katika ufundishaji.

Lakini kwa utaratibu ambao, klabu hizi tatu zinautumia kwa uongozi kuajiri kocha mkuu na kisha kumchagulia msaidizi wake, hakuna ubishi kwamba wanaweza kutofautiana katika falsafa ya ufundishaji, hivyo kocha msaidizi kushindwa kutekeleza majukumu ya bosi wake ipasavyo.

Tulishuhudia, Aussems akimkataa msaidizi wake, Masoud kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutofuata maelekezo yake anayompangia jambo ambalo lilizua mvutano mkubwa kabla ya uongozi wa Simba kuamua kuachana na Mrundi huyo na kumuajiri Kitambi.

Kwa mantiki hiyo, tunaona umefika wakati sasa kwa klabu hizo kubadili utaratibu huo kwani tunaamini wapo baadhi ya wasaidizi ambao lengo lao ni kuhakikisha wanawapindua makocha wakuu na wengine wamekuwa vikwazo katika klabu kupiga hatua kimaendeleo.

Habari Kubwa