Sio Nkana tu, hata Waarabu Simba mnaweza kufanya vizuri

12Jan 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Sio Nkana tu, hata Waarabu Simba mnaweza kufanya vizuri

MARA ya mwisho kwa timu ya Tanzania kucheza hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa mwaka 2003 ambapo Simba waliwatoa waliokuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Zamalek ya Misri.

Miaka 15 baadae klabu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi inakuwa klabu nyingine kutinga hatua hiyo baada ya kupita miaka hiyo 15.

Leo mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla wataishuhudia Simba ikicheza tena hatua hiyo kwa kucheza mchezo wake wa kwazna dhidi ya Waarabu wa Algeria, JS Saoura FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo wa leo unasubiriwa kwa hamu na mashabiki na Watanzania kwa ujumla hasa baada ya kuishuhudia Simba ikiwaondoa Nkana FC ya Zambia na kukata tiketi ya kushiriki hatua hiyo.

Kabla ya kuingia hatua hiyo yaMakundi, Simba ilianza kuwaondoa Mbabane Swallows kwa jumla ya mabao 8-1 kwenye michezo miwili na kukubaliana na Nkana kwenye hatua ya mwisho kabla ya kutinga hatua ya makundi.

Kimsingi Nipashe tunaamini juu ya uwezo wa Simba, tunaamini chini ya kocha Patrick Aussems, Simba inaweza kufanya kile walichofanya kwenye mchezo wao wa mwishi dhidi ya Nkana.

Wachezaji wa Simba wanapaswa kutambua ukubwa wa klabu ya Simba na thamani ya kuvaa jezi yaklabu hiyo kubwa hapa nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Tunaamini kwenye kujituma na nidhamu ya mchezo ndanio ya uwanja ndio silaha kuu ya wachezaji wa Simba kuweza kupata ushindi kwenye mchezo wake wa kwanza leo dhidi ya timu hiyo ya Algeria anayochezea Mtanzania Thomas Ulimwengu.

Wachezaji wa Simba wanapaswa kufahamu umati utakaojitokeza leo kwenye uwanja wa Taifa utakuwa nyuma yao pamoja na watanzania wengine watakaofuatilia mchezo huo kwenye televisheni.

Lakini pia pamoja na upinzani wetu watanzani kwenye soka, tunapswa kufahamu Simba wanaikwakilisha nchi kwenye michuano hii mikubwa zaidi kwa ngazi ya vilabu Afrika, hivyo ni vyema kuiunga mkono kuhakikisha wanapata ushindi ambao ushindi huo hautakuwa wa Simba peke yake bali ni wa watanzani wote.

Nipashe pia tunataka kuwakumbusha wachezaji umuhimu wa michuano hii, Afrika nzima na Dunia wanaifuatilia hivyo ni sehemu nzuri ya kujitangaza kuweza kupata malisho bora nje ya Tanzania.

Kwa wachezaji ambao wana ndoto yakucheza soka nje ya Afrika kama ilivyo kwa Mbwana Samatta, Abdi Banda, Himid Mao na Simon Msuva, hii ni sehemu muafaka ya kuonyesha kiwango cha juu ili kuweza kupata timu nje ya nchi.

Ikimbukwe, Samatta alianza kupata jina Afrika kupitia michuano hii baada ya kuonyesha kiwango cha juu kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe kwenye uwanja wa taifa na kupelekea wakongo hao kumsajili.

Nipashe tunasema, sio kwa Nkana tu, hata kwa waarabu Simba mnaweza kufanya vizuri kwenye mchezo wa kesho na kuanza vizuri hatua hiyo ya makundi.

Watanzania tunataka kuona tunaingiza timu kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hii na kuweka rekodi yakuwa nchi ya kwanza kutoka Tanzania kuingiza timu kwenye hatua hiyo kubwa.

Mbali na kuwatakia heri na mafanikio wachezaji wa Simba, lakini pia Nipashe tunakumbusha vyombo vya usalama kuweka ulinzi wa kutosha uwanjani ili kuepekua vulugu zozote.

Uongozi wa Simba, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na jeshi la Polisi, waweke mazingira mazuri na utaratibu shahiki kwa mashabiki kuingia na kutoka uwanjani bila kuleta vurugu.

Lakini pia ikumbukwe JS Saoura nao watakuwa na mashabiki wake, na inafahamika timu za kiarabu zimekuwa na mashabiki wenye miemko mikubwa hivyo lazima ulizni uimarishwe ili kila timu mashabiki wake washangilia kwa nafasi zao na kuzisapoti timu zao.

Yote kwa yote, Nipashe kama wadau wa soka na watanzania, tunaitakia kila la heri Simba kuweza kupata ushindi kwenye mchezo huo wa kwanza.

Habari Kubwa