Soka la Tanzania linahitaji wachezaji wa kigeni zaidi

18May 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Soka la Tanzania linahitaji wachezaji wa kigeni zaidi

KUTOKANA na mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona (COVOD-19), mkutano uliokuwa ukitarajiwa kuwakutanisha wadau wa soka nchini ili kujadili na kisha kupata muafaka wa hatma ya idadi ya wachezaji wa kigeni nchini, hautakuwapo tena.

Kufanyika kwa mkutano huo ilikuwa ni agizo la serikali kupitia kwa wizara husika ya michezo ambayo kwa maoni ya Waziri wake, Dk. Harrison Mwakyembe anaamini idadi ya wachezaji 10 wa kigeni wanaoruhusiwa kwa sasa ni kubwa, hivyo inapaswa kupunguzwa.

Hata hivyo, kutokana na mlipuko wa maambukizo ya virusi vya corona vilivyosababisha serikali kupiga marufuku shughuli zote zinazosababisha mikusanyiko ya watu, sasa mjadala huo utafanyika kwa kupitia mtandao wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kwa kila mdau kutoa maoni yake.

Tunapongeza hatua hii ya serikali ya kutoingilia moja kwa moja kufanya uamuzi katika shughuli za michezo na badala yake kuwaachia wadau kujiamulia. Hivyo, ni wakati wa wadau wa soka kutumia fursa hii adhimu kutoa maoni yao sasa ili uamuzi ukifanyika uwe wa wote badala ya kukaa kimya na kisha baadaye kuanza kulalamika kwa umuazi utakaofikiwa.

Kwa mujibu wa maoni ya Waziri Mwakyembe kama ilivyo kwa baadhi ya wadau wachache wa soka, wanaamini uwapo wa wachezaji wengi wa kigeni unaua vipaji vya wazawa hivyo kuidumaza timu ya Taifa, Taifa Stars jambo ambalo Nipashe kamwe hatuwezi kukubaliana naye.

Tukiwa kama wadau namba moja wa soka nchini, tunaamini wachezaji wa kigeni wanapaswa kubaki 10 kama ilivyo sasa ama kuongezwa na si kuwapunguza, kwani ndiyo wanaowafanya wazawa kuongeza juhudi kwa kupigania namba uwanjani, na si hili la kutaka kuwarahisishia nafasi ya kucheza.

Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba; kwanza klabu zenye uwezo wa kusajili wachezaji 10 wakigeni sana sana ni tatu, Simba, Yanga na Azam FC na bado katika vikosi vyao vya kwanza kuna wazawa wengi wanaotoa ushindani wa namba na kupata nafasi, jambo ambalo limewafanya kuwa bora hata kwenye timu ya taifa.

Pili mara nyingi tumekuwa tukipiga kelele wachezaji wetu kuonyesha uwezo na kutafuta nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa ili kuwa na nyota wengi katika timu ya Taifa, lakini imekuwa vigumu kwao kuweza kupata timu kubwa nje, hivyo hawa wageni wanaotoka nje ndiyo wanaoweza wazawa kuwa bora humu humu nchini.

Kwa mantiki hiyo, kinachotakiwa ni TFF kuhakikisha wachezaji wa kigeni wanaokuja kucheza soka nchini wanakidhi vigezo watakavyoviweka hususan viwango vitakavyoweza kutoa changamoto kwa wazawa kujiimarisha, lingine labda kuweka kanuni ya idadi ya watakaoruhusiwa kucheza katika mechi moja.

Lakini pia kwa wadau wanaotaka wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa na klabu nchini kupunguzwa kutoka 10 wa sasa, kama ukitazama Ligi Kuu ambayo msimu ujao itashirikisha timu 16 huku kanuni ikiruhusu kila klabu kusajili jumla ya wachezaji wasiozidi 30, hiyo inamaana jumla yao watakuwa 480, ukitoa 30 wa kigeni kutoka Simba, Yanga na Azam na unaweza kufanya 50 wengine wa kigeni ni kutoka klabu zingine 13 na kufanya jumla ya wageni kuwa 80.

Kwa mantiki hiyo wazawa watakuwa 400, hivyo ni vipi wachezaji 80 wa kigeni wazuie wenyeji 400 kuonyesha uwezo wao? Hata hivyo, idadi hiyo ya 'mapro' 80 ni makadrio ya juu sana kwani hata wakati huu Ligi Kuu ikishirikisha klabu 20 bado wageni hawajafikia 80, hivyo kuendelea kuzuia wageni ni kuwalemaza wazawa kwa kuwafanya washindwe kujituma kwa kupigania namba.

Habari Kubwa