Soka letu bado linahitaji wachezaji wa kigeni zaidi

17Feb 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Soka letu bado linahitaji wachezaji wa kigeni zaidi

MWISHONI mwa wiki kwa mara nyingine tena Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, aliibua hoja ya kupunguzwa kwa idadi ya wachezaji wa kigeni Ligi Kuu Bara.

Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Bara, kila klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi 10, jambo ambalo Dk. Mwakyembe anataka mjadala mpana akipendekeza wapungue hadi watano.

Hii si mara ya kwanza kwa Waziri Mwakyembe kutoa pendekezo hilo, na safari hii ameweka hoja hiyo mezani akitaka viongozi na wadau wa soka, kuijadili kwa mapana zaidi.

Hoja ya Mwakyembe, yeye anaona klabu kuruhusiwa kusajili wachezaji 10, kunapunguza nafasi ya wazawa kucheza na kuibuliwa kwa vipaji. Hata hivyo, Nipashe tunaona hoja hiyo haina mashiko kwa maendeleo ya soka kwa sasa kwani soka letu linawahitaji wachezaji wa kigeni zaidi.

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba Ligi Kuu kwa sasa ina klabu 20, na zenye uwezo wa kusajili wachezaji hao 10 wa kigeni hazizidi tatu. Kwa ujumla kila klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji wasiozidi 30, hivyo kwa msimu mzima kwa klabu 20, jumla ya wachezaji 600 hucheza ligi hiyo.

Kama klabu zinazoweza kusajili wachezaji wote 10 wa kigeni hazizidi tatu, hiyo ina maana watakuwa 30, hata hivyo tufanye jumla ya nyota wote wa kigeni kwa msimu Ligi Kuu ni 50.

Hiyo inamaana kwa msimu mzima kuna wazawa 550 watakaoonekana wakicheza Ligi Kuu, tunashindwa kuelewa ni vipi wageni 50 wanaweza kuzuia vipaji hivyo kuonekana.

Lakini pia, tunashindwa kuielewa hoja ya Waziri Mwakyembe kuwa wachezaji wa kigeni eti wenyewe wanalipwa mishahara mikubwa kuliko wazawa. Ikumbukwe tunaelekea katika soka la kulipwa, hivyo suala la mchezaji wa kigeni kulipwa zaidi ya mzawa, hilo haliwezi kuepukika kwa vyovyote vile.

Leo hii Muargentina Lionel Messi, ndiye mchezaji anayelipwa zaidi Ligi Kuu, Hispania huku Mjerumani Metus Ozil akiongoza kwa kulipwa zaidi Ligi Kuu England kama ilivyo kwa Mreno Cristiano Ronaldo pale Juventus kwenye Ligi Kuu Italia.

Lakini Waziri Mwakyembe pamoja na wadau wengine wanaotaka wageni kupunguzwa kutoka 10 hadi watano, watambue kwamba uwapo wao Ligi Kuu Bara unaboresha viwango vya wachezaji wetu.

Wachezaji wetu wengi wanacheza soka la ndani jambo ambalo tumekuwa tukipiga kelele tukiwataka kwenda kucheza soka la kulipwa ili waweze kuwa msaada kwa timu ya Taifa, Taifa Stars, kama hilo limeshindikana tuvutie wageni wenye viwango kuja nchini kucheza nao.

Hivyo, kinachotakiwa ni Shirikisho la Soka nchini (TFF) kusimamia kanuni yake ya wageni wanaosajili nchini kuwa na viwango vya hali ya juu ili kutoa changamoto ipasavyo kwa wazawa.

Mwisho pamoja na kuwapo wageni bado tunaona wazawa kama Hassan Dilunga, Erasto Nyoni, Jonas Mkude pale Simba huku Yanga, Kelvin Yondan, Metacha Mnata, Juma Makapu na Azam FC wachezaji kama Agrey Moris na wengine wengi wakiwa katika vikosi vya kwanza.

Na hao ndio wamekuwa tegemeo wanapoitwa kuitumikia Taifa Stars, hiyo inaonyesha ni kwa namna gani wanapambana kuwania namba klabuni jambo linaloboresha viwango vyao kila uchao.

Habari Kubwa