Stars bado ina nafasi Rwanda

17Jul 2017
Mhariri
Nipashe
Stars bado ina nafasi Rwanda

JUZI kulikuwa na mchezo wa kimataifa wa kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) kati ya Tanzania 'Taifa Stars' na Rwanda 'Amavubi'.

Katika mchezo huo uliochezwa jijini Mwanza, Taifa Stars ililazimishwa sare ya bao 1-1 na wageni hao.

Kimsingi, matokeo hayo yanaweza yasiwe mazuri kwa Taifa Stars ambayo italazimika angalau kupata sare kama hiyo ya hapa nyumbani na kutarajia kusonga mbele kwa 'matuta', kutoka sare zaidi ya bao 1-1 au kuwafunga kabisa Rwanda nyumbani ili kupata nafasi ya kusonga mbele katika harakati hizo za fainali za mwakani.

Taifa Stars ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo wa juzi hasa baada ya kufika nusufainali ya Kombe la COSAFA la nchi za Kusini mwa Afrika mapema mwezi huu, lakini kwa sababu soka ni mchezo usiotabirika kirahisi ilijikuta ikitoka sare.

Pamoja na matokeo hayo, Nipashe tunasema, Taifa Stars bado ina nafasi ya kushinda mchezo wa marudiano utakaochezwa Rwanda Jumamosi.

Kikubwa, Nipashe tunaona, ni wachezaji na benchi la ufundi kufanyia kazi mapungufu yaliyoonekana kwenye mchezo wa juzi na kujipanga kikamilifu kuhakikisha hayajirudii mjini Kigali, kuwatoa Rwanda na kusonga mbele.

Hakuna kinachoshindikana kunapokuwa na dhamira ya kweli ya kutaka kusonga mbele, wachezaji wa Stars ni lazima wafahamu na hivyo matokeo ya juzi hayapaswi kuwakatisha tamaa Stars.

Kimsingi Watanzania na wadau wa soka tunapaswa kuendelea kuisapoti timu yetu na kuwapa moyo wachezaji ili waende kupambana kwenye mchezo wa marudiano wakiwa na ari zaidi.

Rwanda inaweza kuona ni kama imamemaliza kazi baada ya kulazimisha sare ya ugenini hiyo jijini Mwanza, lakini kwa kuwa wahenga walisema mpira unadunda, bado nafasi ipo wazi kwa timu yetu.

Nipashe tunaamini Taifa Stars ilikuwa na makosa madogo madogo yaliyoruhusu Rwanda kupata bao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Hivyo basi ni vyema kwa benchi la ufundi likakaa chini na kufanya tathmini juu ya mchezo uliopita na kufanya utatuzi wa makosa madogo hayo ya Jumamosi.

Na kama makocha wa Stars watafanyia kazi mapungufu yaliyoonekana juzi, uwezekano ni mkubwa kwa Stars kusonga mbele, Nipashe tunaamini.

Stars inapaswa kuwa na ari zaidi ya kufanya vizuri kwa kuwa endapo itaitoa Rwanda, itabakiza kikwazo kimoja tu kama ama Uganda au Sudan Kusini ili kukata tiketi ya kushiriki fainali za Chan, na bahati nzuri timu zote mbili tunazifahamu vizuri.

Na kwa kuwa Jumamosi siyo mbali, ni vyema sasa kocha Salum Mayanga na benchi zima la ufundi wakazitumia siku zilizobakia kufanya maandalizi.

Taifa Stars imewahi kwenda fainali ikiwa katika mazingira kama haya, kikosi cha safari ya CHAN ni lazima kikumbuke hilo.

Na kama timu ya Joel Bendera ilimudu kuibuka kutoka mazingira kama haya ya kikosi cha Mayanga mwaka 1979 nchi ilipofuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za CAN kwa mara ya kwanza na ya mwisho, Stars ya leo inakosa nini ishindwe kufuzu CHAN kwa mara ya pili?