Stars fanyeni kweli kwa Senegal kesho

22Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Stars fanyeni kweli kwa Senegal kesho

BAADA ya jana mashabiki wa soka kushuhudia fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 zikifunguliwa kwa wenyeji, Misri kuvaana na Zimbabwe, kesho macho na masikio ya Watanzania yataelekezwa kwa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Taifa Stars itashuka dimbani kwenye fainali hizo ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1980 iliposhiriki fainali hizo nchini Nigeria.

Katika mchezo wa kesho, Stars itaanza kutupa karata yake ya kwanza dhidi ya Senegal na kisha Alhamisi Juni 27 kurudi dimbani kuwavaa majirani zao, Kenya ('Harambee Stars') kabla ya Julai Mosi, mwaka huu kuhitimisha mechi zake za hatua ya makundi dhidi ya Algeria.

Mechi ya kesho ni ngumu sana kwa Stars kwani inakabiliana na timu inayoundwa na wachezaji wengi wenye vipaji na uwezo wa hali ya juu ukilinganisha na nyota hao wa Tanzania walioko chini ya Mnigeria Emmanuel Amunike.

Mbali na sifa hizo, lakini pia kikosi cha Senegal kina wachezaji wengi wenye uzoefu wa mechi za kimataifa na wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya, na pengine ahueni kwa Stars inaweza kuwa kukosekana kwa Sadio Mane aliyetoka kuipa Liverpool ubingwa wa Ulaya, ambaye atakuwa nje akitumikia adhabu ya kadi.

Kwa ujumla Mane ni mmoja tu kati ya wengi na huwezi kulinganisha nyota wa kikosi cha Senegal na Stars ambayo kwa asilimia kubwa inategemea uzoefu mkubwa kutoka kwa nahodha wake, Mbwana Samata anayecheza soka la kulipwa KRC Genk ya Ubelgiji.

Hata hivyo, Nipashe kama wadau wakubwa wa soka hapa nchini hatuna shaka wala hofu na Stars kwani tunaamini inaweza kuwashangaza wengi kutokana na dhamira ya wachezaji kutaka kuonyesha uwezo wao ili kujitafutia soko nje ya nchi.

Tunatambua Stars itaingia uwanjani kama timu ambayo haipewi nafasi ('underdog') na kama Senegal nayo itaidharau tunauhakika inaweza kuushangaza Ulimwengu.

Kama ambavyo Senegal iliweza kuishangaza dunia kwa kuwafunga mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, Ufaransa kwenye fainali hizo zilizofanyika mwaka 2oo2 na kutinga robo fainali, ndivyo ambavyo Stars inaweza kufanya maajabu.

Kinachotakiwa na ambacho Nipashe tunaamini benchi la ufundi la Stars litakifanyia au limeshakifanyia kazi nikuwajenga wachezaji kisaikolojia kwamba inawezekana.

Hilo litawasaidia wachezaji kuondoa woga na kujenga moyo wa upambanaji, lakini pia ni muhimu kuandaliwa kucheza kitimu zaidi kwani siku zote katika soka hiyo ndiyo silaha ya kukidhibiti kikosi kinachoundwa na nyota wengi.

Tunaamini hivyo kwani hata wakati Senegal inaichapa Ufaransa haikuwa na wachezaji wa kiwango cha juu wengi kama Mane, bali iliamini katika kucheza kitimu wakati huo Wafaransa wakiwa na nyota wa Kizazi cha Dhahabu kama Zinedine Zidane, Didier Deschamps, Thierry Henry na wengine.

Kila mchezaji akitimiza jukumu lake ipasavyo, tunaamini inawezekana kabisa kwa Stars kupata matokeo kesho na kuishangaza dunia jambo ambalo litavutia mawakala wengi kumulika soka la Tanzania.

Wachezaji hawana budi kufahamu kwamba kushinda mechi ya kwanza kutawaongezea ari ya kuweza kufanya vizuri mechi zinazofuata na hatimaye kutinga robo fainali, hivyo kesho wanapaswa kucheza kufa au kupona.

Nipashe kama ilivyo kwa wadau wengine wa soka na Watanzania kwa ujumla tunaiombea Stars na tutaendelea kuitakia kila la kheri katika mechi zake zote kwenye michuano hiyo.