Stars iandaliwe mapema kuelekea fainali za CHAN

29Jun 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Stars iandaliwe mapema kuelekea fainali za CHAN

TIMU ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), ilifuzu kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani maarufu (CHAN), mashindano ambayo yanaandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Taifa Stars inayonolewa na Kocha Mkuu Mrundi, Etienne Ndayiragije, ilifuzu kushiriki fainali hizo kwa mara ya pili tangu zianzishwe baada ya kuwafunga Sudan hapo Oktoba mwaka jana.

Hii ni mara ya pili kwa Taifa Stars kukata tiketi ya kushiriki fainali hizo, kwa mara ya kwanza ilishiriki fainali hizo mwaka 2008 nchini Ivory Coast na Mbrazil Marcio Maximo ndio alikuwa Kocha Mkuu.

Hata hivyo, michuano hiyo kama ilivyokuwa katika mashindano mengine mbalimbali yaliyotarajiwa kufanyika, ilisimamishwa kutokana na janga la ugonjwa wa corona.

Aidha, CHAN ilipangwa kufanyika kuanzia Aprili 4 hadi 25, mwaka huu katika miji mitatu tofauti huko Cameroon.

Kwa sasa timu zote 16, zilizofuzu kushiriki fainali hizo, zinasubiri tarehe mpya ya mashindano ili kwenda kuwania taji hilo la pili kwa ukubwa hapa barani Afrika.

Michuano hiyo inashirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani na kwa hapa nchini, kikosi chetu kinaundwa na nyota wengi wanaoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo kwa sasa inaelekea ukingoni.

Nipashe linalikumbusha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuanza mikakati ya kuiandaa Taifa Stars ili ratiba ya mashindano hayo itakapotolewa wawe imara kwenda kupeperusha vema bendera ya nchi.

Tunaamini timu itakayoandaliwa vizuri, itakwenda kushindana na tuache mazoea ya kusubiri ratiba inapotoka ndio tunaanza kuandaa kikosi na matokeo yake badala ya kwenda kushindana, tunakwenda kuwa wasindikizaji.

Ni vema TFF ikatekeleza mipango ya Ndayiragije ya kukijenga kikosi cha Stars kwa kutafuta mechi mbalimbali za marafiki kabla ya kuanza kwa fainali hizo.

Hii inatokana na viwango vya wachezaji wa Stars hasa kwa kuzingatia ubora wa Ligi Kuu Tanzania Bara na ligi wanazotoka wachezaji wa timu wapinzani watakazokutana nazo.

Mara nyingi maandalizi ya zimamoto yamekuwa yakifanya na Stars au timu yoyote kwenda katika mashindano kukamilisha ratiba badala ya kwenda kuchukua kikombe.

Mbali na kupata taji, mashindano hayo ni sehemu nyingine ya kutangaza vipaji vya wachezaji wa Kitanzania ambao wengi bado wana ndoto za kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya, wanaweza kuonekana na mawakala wanaotafuta wachezaji.

Lazima tukumbuke wachezaji wengi wa Tanzania hawajapitia katika akademi za soka na hivyo kukosa baadhi ya misingi, kwa maana hiyo wanahitaji kupata muda mrefu zaidi wa maandalizi tofauti na nyota watakaokutana nao kutoka mataifa yaliyopiga hatua kama Misri, Algeria au Afrika Kusini.

Pia Stars imetinga katika hatua ya makundi katika mashindano ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo la Kombe la Dunia, michuano ambayo mechi zake huwa na ushindani zaidi kwa sababu kila nchi inajua umuhimu wa kupeperusha bendera yake kwenye michuano hiyo.

Ili Stars iende katika mashindano yote ikiwa imara, wadau wote wanatakiwa kushiriki katika maandalizi kuanzia sasa kwa ushirikiano na TFF na kuacha tabia ya kusubiri kulaumu pale wawakilishi wetu hao watakapofanya vibaya.

Habari Kubwa