Stars kujipima na Misri haitoshi kuelekea Afcon

06May 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Stars kujipima na Misri haitoshi kuelekea Afcon

WIKI iliyopita Kocha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Emmanuel Amunike, alitangaza kikosi chake kitakachoingia kambini mwezi ujao kwa ajili ya kujiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) nchini Misri.

Katika fainali hizo zitakazoanza kutimua vumbi Juni 21, Stars imepangwa Kundi C pamoja na Algeria, Senegal na majirani zao, Kenya (Harambee Stars).

Ni dhahiri hili si kundi jepesi kwa Stars ambayo hii ni mara ya kwanza kushiriki fainali hizo tangu mwaka 1980 iliposhiriki kwa mara ya kwanza.

Hivyo, maandalizi ya kina yanahitajika ili kutotia aibu kwa kupoteza mechi zote kama ambavyo timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), ilivyoitia nchi aibu katika michuano ya Afcon U-17 iliyomalizika hapa nchini mwezi uliopita.

Katika michuano hiyo, Serengeti Boys iliyokuwa Kundi À pamoja na Angola, Nigeria na jirani zao Uganda ilipoteza mechi zote licha ya kuandaliwa kwa muda mrefu kwa kucheza mechi nyingi za kirafiki na kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa. 

Kwa mantiki hiyo, kwa kuzingatia ukweli kwamba baadhi ya wachezaji wa Stars kutokuwa na uzoefu wa mechi za kimataifa huku wakicheza soka la ndani, tunaona ipo haja ya kupata zaidi ya mechi moja ya kujipima nguvu.

Stars itacheza mechi yake ya kwanza ya michuano ya Afcon Juni 23 dhidi ya Senegal kabla ya mchezo unaofuata kuivaa Uganda.

Tunatambua Senegal ni timu yenye wachezaji wengi wazoefu wa mechi za kimataifa na wanaocheza soka la kulipwa katika klabu kubwa Ulaya akiwamo mshambuliaji hatari anayeichezea Liverpool ya England, Sadio Mane.

Na katika kuelekea fainali hizo, tayari Shirikisho la Soka nchini (TFF) limetangaza kuwa Stars itaweka kambi Misri na kucheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya wenyeji hao wa Afcon 2019.

Tunaipongeza TFF kwa kufanikiwa kuitafutia Stars mechi hiyo ya kirafiki kwani tunatambua itakuwa ni jaribio nzuri kwa timu yetu hasa ukizingatia ukweli kwamba Misri nayo inaundwa na wachezaji wengi wazoefu wa mechi za kimataifa na baadhi wakicheza Ulaya.

Na si hilo tu, tunaamini kuwa safu ya ulinzi na idara nyingine zitapata nafasi ya kujifunza namna ya kumkaba Mane na wachezaji nyota wengine kwa kupitia Mohamed Salah anayecheza na Msenegal huyo kwenye Klabu ya Liverpool.

Pamoja na kufanikisha kupata mchezo huo wa kirafiki bado Nipashe tunaona ipo haja zaidi kwa TFF kuingia mawindoni na kuitafutia Stars mechi nyingine angalau mbili kabla ya kuanza kwa fainali hizo.

Kwa kufanya hivyo, si tu kutawasaidia wachezaji wa Stars kuendelea kujiimarisha, bali pia kutampa uwanja mpana kocha Amunike kupata kikosi cha kwanza na mifumo tofauti kulingana na aina ya wapinzani watakaokutana nao kwenye fainali hizo.

Tunaamini hilo linawezekana na lipo ndani ya uwezo wa TFF, na si lazima iumize kichwa sana kwani hata kama ikipata timu ambayo haipo kwenye fainali hizo, bado inaweza kuwa msaada kwa Stars na benchi lake ufundi katika maandalizi yao.

Aidha, wachezaji walioitwa Stars kujiandaa kwa fainali hizo, hawana budi kuanza maandalizi binafsi sasa na si kusubiri hadi watakapoingia kambini baadaye mwezi ujao.

Nipashe kama mdau namba moja wa soka nchini, tunataka kuona Stars ikipeperusha vema bendera ya Taifa na kuijengea Tanzania heshima katika medali ya soka kimataifa.

Habari Kubwa