Suala la maambukizi ya VVU kwa vijana lisifanyiwe mzaha 

03Dec 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
Suala la maambukizi ya VVU kwa vijana lisifanyiwe mzaha 

TANZANIA juzi iliungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani ambayo huwa mahsusi kutoa elimu na kuweka mikakati mbalimbali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo ambao umegharimu maisha ya watu tangu kugunduliwa miaka ya 1980. 

Katika kuadhimisha siku hiyo juzi, miongoni mwa mambo yaliyofanyika kwa hapa nchini ni uzinduzi wa matokeo ya utafiti juu ya viashiria na matokeo ya ugonjwa huo kwa mwaka 2016/17. 

Utafiti huo ulionyesha kuwa kumekuwa na mafanikio katika mapambano dhidi ya Ukimwi kwa kuwa maambukizi yamepungua hadi asilimia 4.7 kulinganisha na asilimia 5.1 ilivyokuwa mwaka 2011/12. 

Aidha utafiti huo ulibainisha kwamba inakadiriwa kuwa Watanzania milioni 1.4 wanaishi na virusi vya Ukimwi (VVU) huku kiwango cha maambukizi kwa wanawake kikiwa asilimia 6.5 na wanaume asilimia 3.5.

Pamoja na mafanikio hayo, utafiti huo umeonyesha hali inazidi kuwa mbaya kwa vijana ambao maambukizi yako juu hivyo kuashiria kuwapo kwa hatari kwa kundi hilo ambalo ni nguvukazi ya taifa. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vijana wenye umri wa miaka kati ya 15 na 24 wameathirika kwa kiasi kikubwa huku wasichana wakiwa ndio waathirika zaidi. Taarifa hiyo iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimishio hayo ilionyesha kuwa katika vijana 10 wenye VVU, wanane kati yao ni wasichana huku wawili wakiwa wavulana. 

Sababu kubwa za wasichana kuwa na kiwango cha juu cha maambukizi, kulingana na taarifa hiyo, ni kutokana na tabia ya kujiingiza katika biashara ya ukahaba kwa madai ya kujitafutia riziki. 

Kwa ujumla, matokeo hayo ya utafiti juu ya maambukizi ya VVU kwa vijana yanaashiria kwamba bado kazi ya kupambana na tatizo hilo ni kubwa na inahitaji nguvu za ziada vinginevyo taifa linaweza kujikuta linakosa nguvukazi kwa maendeleo kulingana na mipango iliyopo kwa kuwa na uchumi wa kati unaobebwa na viwanda. 

Tunasema hivyo kwa sababu ukweli uliopo ni kwamba kama kundi hilo halitakuwa salama, ni vigumu kuwa na nguvu kazi kwa ajili ya utekelezaji wa mipango hiyo ya maendeleo ya uchumi. 

Kwa mantiki hiyo, suala hili si la kulifanyia mzaha. Wadau wote kwa maana ya serikali na sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na vyama vya siasa, wanapaswa kulibeba kama ajenda muhimu katika shughuli za kila siku. 

Kama alivyosema Samia, vijana wanapaswa kubadilika na wale wenye tabia ya kujiuza, hawana budi kuacha mara moja ili kuliokoa taifa dhidi ya hatari ya kupoteza nguvukazi kwa shughuli za kisiasa, kiuchumi na kijamii. 

Mapambano haya ikiwamo elimu kwa vijana kuanzia ngazi ya shule za msingi yanapaswa kutekelezwa kwa nguvu zote bila kusita. Kinyume cha hapo ni ndoto kufikia malengo ya maendeleo ikiwa nguvukazi inayotegemewa ikiwa na afya mgogoro.