Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iwezeshwe kwa bajeti

26May 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iwezeshwe kwa bajeti

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imesema kuwa kwa siku mbili inatarajia kuokoa Sh. milioni 180, baada ya kufanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa wagonjwa 18 kwa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo bila kuusimamisha.

Mkuu wa Kitengo cha Matibabu ya Moyo. Dk. Peter Kisenge, amesema upasuaji huo ulianza Jumatatu wiki hii kwa ushirikiano wa taasisi na wataalamu kutoka hospitali ya BLK ya India na kwamba wameshawafanyia upasuaji wagonjwa wanane na wanaendelea vizuri.

Wagonjwa waliotarajiwa kupewa huduma hiyo ni takriban 18 na kuiwezesha taasisi hiyo kuokoa Sh. milioni 180 kwa siku mbili kama wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu hayo.

Tunaipongeza taasisi hiyo kwa mafanikio hayo ambayo yameiwezesha kuanza kutimiza lengo lake kubwa la kuanzishwa kwake mwaka jana, ambalo ni kuokoa fedha ambazo serikali ilikuwa inazitumia kupeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa nje. Kinatia moyo ni taarifa kwamba upasuaji huo ni wa kwanza kufanyika katika eneo la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Wakati wa uzinduzi wa jengo la taasisi hiyo mwaka jana, ilielezwa kuwa kuanzishwa kwa JKCI kungeiwezesha serikali kuokoa Sh. bilioni 2.5 kwa mwaka.
Katika kudhihirisha kwamba inatekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi, Dk. Kisenge kwa mwaka huu pekee JKCI imefanya operesheni 471 ikiwamo upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua 99, vipandikizi 78, kuzibua njia (265) na nyinginezo 29.

Kutokana na tija na ufanisi ulioonyeshwa na JKCI kwa kuda mfupi tangu kuzinduliwa kwa gharama ya Sh. bilioni 16.6 ukiwa ni msaada kutoka serikali ya China kwa ujenzi wa jengo lake, kuna haja kwa serikali na jamii nzima kutambua mchango JKCI na kuiunga mkono kwa hali na mali ili iendelee kuwapatia Watanzania huduma za matibabu ya moyo na kuokoa mamilioni ya fedha kuwapeleka nje.

Jukumu la msingi kwa serikali ni kuhakikisha kuwa JKCI inaendelea kuwapo na kutekeleza majukumu yake bila vikwazo. Kwa hiyo serikali hainabudi kuitengea fedha. Taasisi hiyo inahitaji fedha za kutosha kwa mambo mbalimbali, ikiwamo za kutunza vifaa vya kisasa saidi iliyonavyo, ambavyo vilivyogharimu zaidi ya Sh. bilioni 10.

Pamoja na taasisi hiyo kutekeleza vizuri majukumu yake na kuokoa fedha nyingi ambazo serikali ingezitumia kuwapeleka nje wagonjwa wa moyo, lakini haipati fedha za kutosha.

Mara kadhaa uongozi wake umekuwa ukieleza kwamba bajeti inayotengewa ni ndogo isiyotosheleza mahitaji yake. Hivi karibuni, Kaimu Mkurugenzi, Prof. Mohamed Janabi, alisema wana vyumba viwili vya upasuaji ambavyo kwa sasa vimezidiwa na kwa mwaka 2015/16 hawakuwa wamepokea fedha kutoka serikalini.

Aidha, kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, 2016 taasisi hiyo ilihudumia wagonjwa 17,237 na kuokoa kiasi kikubwa cha fedha, lakini haikupokea fungu lolote la fedha za maendeleo na kwamba gharama za upasuaji iliyoufanya ni Sh. bilioni 1.036 na kama wangewapeleka wagonjwa hao India gharama zingekuwa Sh. bilioni 2.95.

Kwa sasa JKCI inahitaji mashine moja kwa ajili ya kufanyia upasuaji wa moyo na gharama yake ni Dola za Marekani milioni mbili (Sh. bilioni 4.28). Changamoto inazokumbana nazo ni za msingi na ni jukumu la serikali kuiwezesha kwa kuipatia fedha za kutosha ili itoe huduma kwa wagonjwa wa moyo ambazo ni bora na endelevu.

Bila kufanya hivyo, serikali haiwezi kueleweka na hali hiyo inaweza kupoteza lengo la kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

Habari Kubwa