Tahadhari corona iwekwe kwenye masoko, magulio

26Mar 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tahadhari corona iwekwe kwenye masoko, magulio

WAKATI hatua mbalimbali za tahadhari zikiendelea kuchukuliwa nchini kwa lengo la kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa corona, kuna kasoro ambazo tumezibaini, hivyo hatua zinapaswa kuchukuliwa ili kuzipatia ufumbuzi.

Ufuatiliaji wetu katika maeneo kadhaa ya biashara yenye idadi kubwa ya watu kwa mfano katika Soko Kuu la Kariakoo, jijini Dar es Salaam tumebaini kuwa hakujawa na hadhari ya kutosha kuepukana na uwezekano wa watu kuambukizwa.

Katika maeneo hayo watu wengi wanaonekana aidha kupuuza au kutokuwa na uelewa wa maelekezo yaliyotolewa na serikali kuhusiana na hatua za kuchukua kama tahadhari ya kujiepusha na maambukizi.

Licha ya serikali kuwaagiza wafanyabiashara kuweka maji na vitakasa mikono kwenye maeneo ya biashara zao, lakini baadhi ya wafanyabiashara eneo la Kariakoo wameonekana kupuuza agizo hilo ambalo lina lengo la kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo tishio duniani ambao umeshaua maelfu ya watu katika nchi kadhaa.

Baadhi ya maduka sokoni humo yanayotembelewa na mamia ya watu yalishuhudiwa bila kuwa na ndoo zenye majisafi yenye mabomba ya kuyatiririsha, sabuni za maji na vitakasa mikono.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao walisema hawajaweka vifaa hivyo kwa sababu vinauzwa ghali.
Mfanyabiashara wa vyombo vya nyumbani, alisema kuwa hawajaweka vifaa hivyo kwa sababu hawajaelimishwa.
Alisema Jumamosi na Jumapili ameambiwa na wenzangu kuwa magari ya manispaa yalipita kutoa elimu ya matumizi ya vitakasa mikono au sabuni za maji na maji yanayotiririka.

Alisema baada ya wenzake kumwelimisha, wapo kwenye harakati ya kutafuta fedha ili kununua vifaa hivyo kwa ajili ya kujikinga na pamoja na wateja wao.

Mwingine anayeuza urembo, sokoni hapo, alisema elimu ya corona ameipata, lakini changamoto inayowakabili wafanyabiashara wadogo ni gharama ya vifaa hivyo.

Baadhi yao walidai bei ya vifaa hivyo ni kubwa kwa wafanyabiashara wadogo. Uchunguzi wetu ulibaini ndoo maalumu ya kunawia mikono inauzwa kati ya Sh. 10,000 hadi 20,000, sabuni za maji zinauzwa kati ya Sh. 3,500 hadi 4,500 sokoni hapo.

Hata hivyo, Meneja wa soko alisema utaratibu waliouweka ni kutoa elimu kwa wafanyabiashara wanaozunguka soko hilo ili kila mmoja awajibike kuweka vifaa hivyo.

Alisema tangu serikali itoe maagizo kuhusu virusi vya corona na kutaka maeneo yenye mikusanyiko yote yachukue tahadhari ikiwamo kuweka vifaa vya kunawia mikono, uongozi wa soko umefanya hivyo.

Alisema kama bei ya vitakasa mikono ni kubwa, wanaweza kutumia mchanganyiko huo wa kidonge cha chloride au sabuni ya kawaida ya maji.

Pia alitaja changamoto nyingine ni baadhi ya watu ambao hawana makazi hulala sokoni, na wengine huwa ni wagonjwa.

Mbali na kwenye masoko, pia kuna tatizo katika minada, ambayo inahusisha makundi ya watu. Katika minada changamoto inatokana na kufanyika mara moja kwa wiki, hivyo kuwa vigumu kuweka utaratibu mzuri wa kuchukua hatua za tahadhari.

Kutokana na hali hiyo, tunaona kuwa mamlaka husika zinapaswa kuchukua hatua za ziada ikiwamo elimu zaidi na kutumia kupita kukagua wanaokaidi maelekezo ya serikali.

Tunawashauri wafanyabiashara katika masoko na kwenye minada kuheshimu maelekezo ya serikali ili kuepusha uwezekano wa kufungwa kwa sehemu hizo kutokana na ukaidi.

Wafanyabiashara wasikubali hatua hiyo kuchukuliwa kwa kuwa shughuli zao ni muhimu na zinategemewa na kila mtu.

Habari Kubwa