Tahadhari ichukuliwe kuepuka kipindupindu

28May 2019
Mhariri
DAR
Nipashe
Tahadhari ichukuliwe kuepuka kipindupindu

ATHARI zitokanazo na mvua zimeanza kujitokeza, baada ya kuripotiwa kuwa kuna mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika Jiji la Dar es Salaam.

Kwa kawaida mvua zinaponyesha hususan za masika ambazo huchukua kipindi kirefu, hutokea magonjwa ya mlipuko kama kuharisha, homa ya matumbo na kipindupindu.

Chanzo cha magonjwa haya huwa ni uchafu wa maji pamoja na mazingira kwa ujumla, kwa mujibu wa wataalamu wa afya.

Katika toleo letu la jana tuliripoti kwamba ugonjwa wa kipindupindu umeibuka katika Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam na mgonjwa mmoja kulazwa katika Zahanati ya Vingunguti.

Kwamba kutokana na hali hiyo, hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa na mamlaka husika, ikiwamo kutengwa eneo maalum kwa ajili ya kupokea na kuhudumia wagonjwa hao kama wataendelea kuongezeka.

Kaimu Meya wa Manispaa ya Ilala, Omari Kumbilamoto, alisema kutokana na kugundulika kwa mgonjwa huyo Manispaa yake imetenga eneo maalum la kuhudumia wagonjwa ikiwa wataongezeka.

Kumbilamoto alisema hadi sasa wamebaini kuwa chanzo cha ugonjwa huo ni baadhi ya wananchi kutiririsha majitaka ambayo yanakwenda kwenye maji yanayotumiwa na wananchi.

Kwa mujibu wa Kumbilamoto ambaye pia ni diwani wa Vingunguti, hatua za awali zilizochukuliwa ni kunyunyiza dawa kwenye maeneo ya maji machafu yaliyotuama ikiwamo kuchukua hatua dhidi ya wanaotiririsha maji hayo kutoka kwenye vyoo.

Aidha, alisema wanawaelimisha wananchi kunyunyiza dawa, kuchemsha maji, kunawa kwa maji ya moto kabla ya kula na kuhakikisha usafi wa mazingira kila wakati.

Kwa mujibu wa Meya huyo, kwenye maeneo ya masoko wamewaelekeza wahusika kuhakikisha takataka hazikai kwa muda mrefu na usafi wa wafanyabiashara na watumiaji wengine. Mlipuko wa kipindipindu katika Manispaa ya Ilala ni jambo ambalo linapaswa kuwaamsha wakazi wa maeneo mengine kuchukua hatua za tahadhari.

Tunasema hivyo kwa kuwa tabia na mienendo ya maisha ya wakazi wa manispaa zote za Jiji la Dar es Salaam zinafanana, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa maeneo mengine zaidi ya Ilala kutokea mlipuko wa ugonjwa huo.

Kwa mfano, tabia ya kutiririsha majitaka kutoka vyooni umekuwa utamaduni wa wakazi wengi wa Jiji hilo hususan ambao makazi yao yana changamoto ya miundombinu. Kutokana na hali hiyo, mvua zinaponyesha kuzitumia kutiririsha maji hayo yenye uchafu kikiwamo kinyesi.

Pia katika maeneo mengi uchafu unapozolewa kwenye masoko kurundikwa kwa muda mrefu kando ya barabara bila kuzolewa, hivyo kuwa chanzo cha kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Kadhalika, kumekuwapo na tabia ya wananchi hususan jijini Dar es Salaam kupika na kuuza vyakula kwenye maeneo machafu barabarani na karibu na mitaro ya maji, huku mamlaka husika zikiwaacha bila kuwachukulia hatua za kisheria.

Kwa Dar es Salaam pamoja na sababu nyingine, mamlaka hususan halmashauri kutosimamia sheria za usafi na afya ndiko kunakosababisha mlipuko wa kipindupindu kila uchao.

Miongozo ya afya imekuwa ikitolewa na mamlaka hizo kwa wananchi, zikiwamo hatua za tahadhari za kuchukua dhidi ya mlipuko wa kipindupindu.

Tunazishauri mamlaka za afya kuanzia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, halmashauri pamoja na ngazi za kata, vijiji, mitaa na vitongoji kuzitumia sheria zilizopo kusimamia usafi, ikiwamo kuwachukulia hatua kali wanaokaidi kuzifuata.

Bila kufanya hivyo, tutaendelea kutwanga maji kwenye kitu, na kipindupindu kitaendelea kusababisha madhara kwa wananchi, ikiwamo vifo.

Habari Kubwa