Tahadhari muhimu Dar dhidi ya dengue

10May 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tahadhari muhimu Dar dhidi ya dengue

Taarifa kwamba wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam wanaugua ugonjwa wa homa ya dengue, zinapaswa kutushtua na kuchukua hatua za tahadhari.

Imeelezwa kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Mei mwaka huu, jumla ya watu 1,200 katika mkoa mzima wa Dar es Salaam wameugua homa ya dengue na mtu mmoja kupoteza maisha.

Wagonjwa kadhaa wamebainika kutoka maeneo ya Ilala, Kariakoo, Upanga, Kisutu, Buguruni na Tabata wilayani Ilala. Mengine ni Ubungo, Mbezi wilayani Ubungo na Msasani, Masaki na Kinondoni wilayani Kinondoni.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Yudas Ndugile alitoa takwimu hizo hivi karibuni wakati akizungumza na Nipashe kuhusu hali ya ugonjwa ilivyo katika jiji hilo, lenye wakazi takribani milioni tano kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.

Dk. Ngudile alibainisha kuwa wametoa tahadhari kadhaa katika kuudhibiti,ikiwamo za kuangamiza mazalia ya mbu kama vifuu, makopo, vyungu chakavu, matairi chakavu,na kufukia madimbwi kwenye maeneo ya makazi.

Ni vyema kuzingatia tahadhari zilizotolewa ikiwa ni pamoja na kusafisha maeneo ya ofisi, shule, vyuo, gereji, stendi za mabasi, masoko, maeneo ya mama lishe, baa, sehemu wanazouza vinywaji, hoteli, migahawa na hosteli za wanafunzi.

Pia wananchi wametakiwa kuepuka ugonjwa huo kwa kuzuia kunga'atwa na mbu kwa kulala ndani ya chandarua chenye dawa, kupaka mafuta ya kufukuza mbu mikononi na miguuni na kuvaa nguo ndefu kufunika mwili kama mikono, miguu na mgogo.

Tumesikia Serikali kwa upande wake imechukua tahadhari kwa kufanya upuliziaji dawa za kuua mbu katika maeneo ya shule, vyuo, gereji, masoko, kwa mama lishe, kwenye baa, hoteli, migahawa, hosteli za wanafunzi na stendi za mabasi.

Hivi karibuni akiwasilisha bungeni hotuba kuhusu makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, pamoja na mambo mengine naye aliwatahadharisha wananchi kuhusu ugonjwa huo.

Waziri Ummy aliwataka wananchi kuwa makini wapatapo homa wahakikishe wanakwenda kupata huduma katika vituo vya afya ili wapimwe na kupatiwa tiba sahihi.

Waziri alibainisha kuwa wizara imeshakamilisha mpango mkakati wa kudhibiti ugonjwa huo ambao unajumuisha kujenga uwezo wa watumishi wa afya katika kutambua, kupima, matibabu na udhibiti wa mbu wanaoueneza.

Homa ya dengue hutajwa pia kama homa ya kuvunja mifupa kwa sababu inaweza kuwafanya watu wawe na maumivu makali hadi wahisi kama mifupa yao inavunjika.

Dalili za ugonjwa huu huanza kujitokeza ndani ya siku tatu hadi kumi na nne baada ya kuambukizwa, ambapo aliyeambukizwa hupata homa kali, kuumwa na kichwa, kuota vipele kwenye ngozi na maumivu kwenye misuli na maungio au kuvuja damu.

Tunasisitiza kwamba wataalam wa afya wamekuwa wakituhamasisha kuwa kinga ni bora kuliko tiba, hivyo tuzingatie kwa kuzitekeleza mbinu za tahadhari tulizopewa ili kuepuka kuugua ugonjwa huu hatari.

Pia wananchi waache kupuuzia ugonjwa huo, bali wachukue hatua kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya na serikali kwa kuwa ugonjwa huo ni hatari kwa maisha.

Habari Kubwa