Taifa Stars anzeni kwa ushindi CHAN

18Jan 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Taifa Stars anzeni kwa ushindi CHAN

BAADA ya Jumamosi kushuhudiwa wenyeji Cameroon wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zimbabwe kwenye mechi ya ufunguzi wa michuano ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), huku siku hiyo Mali nayo ikipata ushindi kama huo dhidi ya Burkina Faso, kesho ni zamu ya Taifa Stars dhidi ya ...

Zambia.

Mechi hiyo ya Taifa Stars na Zambia ni ya saba katika michuano hiyo tangu ifunguliwe Jumamosi, baada ya kushuhudiwa pia Libya na Niger zikimenyana, DR Congo wakipepetana na ndugu zao Congo, Morocco ikichuana na Togo pamoja na Rwanda wakitoana jasho na Uganda.

Mbali na Zambia kundi hilo la Stars pia linazijumuisha Guinea na Namibia, ambazo nazo zitashuka dimbani kesho kukamilisha raundi ya kwanza ya michuano hiyo ambayo imepangwa katika makundi manne.

Katika kundi hilo, Zambia ndiyo timu inayoonekana kuwa tishio zaidi, hivyo kama Taifa Stars itapata matokeo kesho itakuwa imejiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kupenya hatua inayofuata ambayo ni robo fainali.

Tunaamini maandalizi yaliyofanywa na Taifa Stars chini ya Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije, yanatosha kuweza kuibuka na ushindi kama wachezaji watafuata vema maelekezo yake huku wakijituma na kujitoa mwanzo mwisho kwa kutanguliza mbele thamani ya kuaminiwa kuvaa jezi ya taifa.

Mbali na kila mchezaji kutakiwa kuonyesha uwezo binafsi lakini pia kucheza kitimu ni silaha nyingine itakayoweza kuibeba Taifa Stars hususan dhidi ya vigogo hao wa soka Afrika, Zambia.

Kila mchezaji hana budi kuona ushindi ndio kila kitu katika mechi hiyo ya kwanza ya kundi lao, kwani endapo Stars itapata matokeo kwenye mechi hiyo, utachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza morali katika mechi zinazofuata na kuifanya kujiweka mazingira mazuri ya kutinga robo fainali.

Ni wazi haitakuwa mechi rahisi kwa kila upande, lakini wachezaji wa Taifa Stars hawana budi kutambua kwamba mbali na malengo yao ya kupeperusha vema bendera ya nchini kimataifa, pia huu ni wakati wakutangaza vipaji vyao na kuviweka sokoni.

Nipashe tunatambua mawakala wengi wanaitupia jicho CHAN ili kupata wachezaji wakuwauza katika klabu mbalimbali ndani na nje ya bara la Afrika, hivyo ni wakati wa kila mchezaji kujituma mwanzo mwisho ili kuitumia michuano hiyo kama daraja la kufikia malengo yao ya kucheza soka la kulipwa.

Tunaamini kila mchezaji ndoto zake ni kucheza soka la kulipwa Ulaya na kwingineko barani Afrika kulikopiga hatua kisoka, hivyo hii ni fursa adimu ambayo wachezaji wengi hususan wa nchi za Magharibi wamekuwa wakiitumia kama daraja lao la kwenda kucheza Ulaya, jambo ambalo linapaswa kuigwa pia na nyota wa Taifa Stars.

Katika soka hakuna njia ya mkato ya kufikia malengo zaidi ya kuonyesha uwezo dimbani hususan kwa wachezaji wanaopata fursa kama hii ya kucheza michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika kwa ngazi ya timu za taifa baada ya ile ya Afcon.

Matarajio na maombi yetu si tu kuona Taifa Stars ikitinga robo fainali, nusu na hata fainali kama si kuubeba ubingwa huo, bali pia tunataka kushuhudia wachezaji wengi wakipata nafasi ya kucheza soka la kulipwa Ulaya na kwingineko Afrika kupitia vipaji vyao kuonekana kwenye michuano hiyo.

Hivyo, tunaitakia kila la kheri Taifa Stars katika mwanzo mwema wa michuano hiyo na mechi zinazofuata kwenye michuano hiyo ambayo hii ni mara ya pili kwa Tanzania kushiriki baada ya 2009 kushiriki kwa mara ya kwanza na kuishia hatua ya makundi nchini Ivory Coast

Habari Kubwa