Taifa Stars itavuka CHAN ikiiva Guinea kama fainali

25Jan 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Taifa Stars itavuka CHAN ikiiva Guinea kama fainali

TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, keshokutwa, Jumatano itashuka tena dimbani nchini Cameron kwenye mechi ya mwisho ya Kundi D ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) baada ya Jumamosi kuibuka na ushindi wake wa kwanza katika michuano hiyo kwa kuifunga Namibia bao 1-0.

Stars, ambayo ilianza kwa kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Zambia, Jumatano itavaana na Guinea iliyopo kileleni mwa Kundi D ikiwa na pointi nne sawa na Zambia inayoshika nafasi ya pili kutokana na kuzidiwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Hata hivyo, ushindi pekee ndio utakaoiwezesha Taifa Stars yenye pointi tatu katika nafasi ya tatu, kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayoshirikisha jumla ya timu 16 zikiwa zimepangwa katika makundi manne kila moja likiwa na timu nne.

Katika Kundi D, Namibia ndiyo inaburuza mkia kutokana na kupoteza mechi zake mbili na siku hiyo ya Jumatano itakuwa ikicheza dhidi ya Zambia ambayo itakuwa ikihitaji sare yoyote ili kusonga mbele kama ilivyo kwa Guinea.

Kwa ujumla katika kundi hilo, mchezo kati ya Guinea na Stars, ndio utakaokuwa mgumu zaidi kwani Tanzania itakuwa ikihitaji ushindi ili kusonga mbele huku wapinzani wao, sare yoyote ikiwapa tiketi ya kutinga robo fainali.

Tunaamini hakuna njia ya mkatao ya kuweza kupata matokeo zaidi ya wachezaji kujituma mwanzo mwisho na kuuchukulia kama fainali mchezo huo utakaopigwa majira ya saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Lakini pia tunaamini Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije pamoja na wasaidizi wake, Suleimani Matola na Juma Mgunda, tayari wanafahamu ubora, uimara na udhaifu wa Guinea, hivyo watakuwa wamewapa mbinu zaidi wachezaji wao ili kuibuka na ushindi na kisha kutinga robo fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya mwaka 2009 kuishia hatua ya makundi.

Pamoja na kwamba utakuwa mchezo mgumu kwa Stars kutokana na ubora wa Guinea, ni wakati wa kila mchezaji kutambua na kuona thamani ya kuthaminiwa na Watanzania zaidi ya milioni 50 kwa kupewa dhamana ya kuvaa jezi ya taifa na kwenda kuipeperusha bendera ya nchi katika mashindano hayo ya pili kwa ukubwa barani Afrika kwa ngazi ya timu za taifa.

Hata hivyo, kutokana na ubora wa timu ya Guinea na mchezaji mmoja mmoja, njia pekee ya Stars kuibuka na ushindi, ni kucheza kitimu zaidi na kutokata tamaa mwanzo mwisho kila mmoja akitambua hiyo ni nafasi pekee kwake ya kuonyesha kocha hakukosea kumjumuisha katika kikosi hicho.

Tunalazimika kuyasema hayo kutokana na kutambua wapo mashabiki wengi na wadau wa soka nchini, ambao wanakibeza kikosi cha Stars kutokana na kuonyesha kiwango cha chini katika michuano hiyo, lakini pia tangu mwanzo wakionyesha kutokukubaliana na uteuzi wa wachezaji uliofanywa na Ndayiragije kuunda kikosi hicho.

Hivyo, njia pekee ya kuwafunga mdomo wote wanaowakosoa na wasiowakubali, ni wachezaji kuonyesha ubora na kujituma zaidi katika mechi hiyo ya mwisho ili kushinda na kutinga hatua ya robo fainali.

Lakini pia, kwa kuwa wachezaji wengi hii ni mara ya kwanza kujumuishwa katika kikosi hicho, ni wakati wa kuonyesha ubora wao ili kuendelea kushikilia 'tiketi ya kuitwa Taifa Stars' huku wakitambua wapo mawakala wengi wanaoitupia macho michuano hiyo, hivyo kama watafanikiwa kusonga mbele wataendelea kujitengenezea soko la kucheza soka nje ya nchi kwa kupata klabu kubwa ndani na nje ya bara la Afrika.

Nipashe tunaungana na Watanzania wote wanaoitakia kila la kheri Taifa Stars kupata ushindi kuelekea mechi hiyo ya Jumatano, lakini pia tukiendelea kuwasisitiza wachezaji wasituangushe kwani tunachotaka ni ushindi tu.

Habari Kubwa