Taifa Stars kazeni buti Harambee inafungika

03Aug 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Taifa Stars kazeni buti Harambee inafungika

KESHO Taifa Stars itashuka uwanjani ugenini nchini Kenya kuivaa timu ya Taifa hilo, Harambee Stars, kwenye mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Taifa Stars itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare tasa na Harambee Stars katika mechi ya awali iliyopigwa Uwanja wa Taifa Jumapili iliyopita.

Kwa matokeo hayo, Stars sasa inahitaji ushindi ama sare yoyote ya mabao ili kuweza kusonga mbele katika michuano hiyo itakayofanyika mwakani nchini Cameroon.

Timu itakayopata matokeo kwenye mechi hiyo ya kesho itakutana na mshindi wa jumla kati ya Sudan Kusini ama Burundi ambayo katika mechi ya awali ikiwa nyumbani ilishinda 2-0.

Kwa ujumla tunaimani kubwa na kikosi hicho cha Stars chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Mrundi Etienne Ndayiragije akisaidiwa kwa karibu na wazawa Selemani Matola pamoja na Juma Mgunda.

Hiyo ni kutokana na namna ambavyo Taifa Stars ilivyocheza na kufanikiwa kumiliki mpira kwa asilimia kubwa zaidi ya Harambee Stars katika mechi ya awali ikiwa ni baada ya Ndayiragije na wasaidizi wake kuanza kukinoa kikosi hicho kwa muda mfupi mara baada ya kuteuliwa kukinoa katikati ya mwezi uliopita.

Kwa namna ambavyo Stars ilicheza mechi ya awali, ilionyesha kukamilika idara zote, lakini makosa madogo madogo katika safu ya ushambuliaji na viungo wa kati kushindwa kuelewana vizuri, yanaweza kuwa chanzo cha kukosa ushindi kwenye mchezo wa awali.

Kwa kuwa hiyo ilikuwa ni mechi ya kwanza kabisa kwa Ndayiragije na wasaidizi wake kukiongoza kikosi hicho, tunaimani amegundua makosa yaliyojitokeza na tayari ameyafanyia kazi kuelekea mechi hiyo ya kesho ugenini.

Lakini pia ari na hamasa kutoka kwa wachezaji ni baadhi ya mambo ambayo yanatupa imani kwa Taifa Stars kupata matokeo na kusonga mbele hatimaye kufuzu michuano hiyo kwa mara ya pili tangu ilipoanzishwa mwaka 2009.

Tunatambua si rahisi kupata ushindi kwa Harambee Stars ikiwa nyumbani huku ikiwa na kocha wake, Mfaransa Sebastien Migne ambaye wamekuwa naye kwa muda mrefu sasa, lakini kama wachezaji watakaza buti huku wote wakiwa na nia moja tu ya ushindi, tunaamini Taifa Stars inaweza kupata matokeo na kuwashangaza wengi ambao wanaamini haiwezekani.

Kinachotakiwa kwa wachezaji wa Stars ni kuondoa woga wa kucheza ugenini na kujiona kama wapo uwanja wa nyumbani na kupambana mwanzo mwisho bila uoga wowote.

Tunatambua Harambee Stars watakuwa 12 uwanjani kwa maana ya mashabiki wao jukwaani ambao jukumu lao litakuwa moja tu kuwapa hamasa wachezaji wao 11 dimbani kwa kuwashangilia mwanzo mwisho, lakini hilo haliwezi kuwa sababu kwetu kukataa tamaa ya kupata matokeo.

Taifa Stars inaundwa na wachezaji wengi walioshiriki michuano ya Afcon mwaka huu nchini Misri ukilinganisha na Harambee Stars, hivyo uzoefu walioupata katika fainali hizo, tunaamini watautumia vema wakiwa ugenini kuweza kupata matokeo kwa kuwa si mara yao ya kwanza kucheza mechi ya kiushindani ugenini.

Nipashe kama ilivyo kwa wadau wengi wa soka nchini, tunatamani kuona Stars ikifuzu fainali hizo na Watanzania kuanza kujiandaa kwa safari ya kwenda Cameroon kuiunga mkono kama ambavyo hamasa ilivyokuwa katika fainali za Afcon 2019 nchini Misri.

Tunaitakia kila la kheri Taifa Stars wakati huu tukiamini huu ni mwaka wa Tanzania kufanya vizuri kimataifa kwa kufuzu fainali hizo baada ya mwaka huu kutimiza lengo la awali la kufuzu na kushiriki Afcon kwa mara ya pili katika historia ya Tanzania kwenye michuano hiyo.

Habari Kubwa