Taifa Stars malizeni biashara mapema kwa Mkapa kesho

06Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Taifa Stars malizeni biashara mapema kwa Mkapa kesho

KWA mara nyingine tena timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, itashuka dimbani kesho, baada ya kutoka sare bao 1-1 ugenini dhidi ya DR Congo kwenye mechi yao ya kwanza ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar.

Kwa matokeo hayo, Stars sasa ina alama moja sawa na DR Congo huku Benin ikiwa kileleni katika Kundi J, baada ya Ijumaa iliyopita yenyewe kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Madagascar.

Hivyo, Stars ambayo itaikaribisha Madagascar katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kesho, ushindi pekee ndio utakaohitajika kwake ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kumaliza nafasi ya kwanza kwenye Kundi lao la J.

Ikumbukwe katika mbio hizo za kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar, kwa Ukanda wa Afrika kuna makundi 10, na kila timu itakayomaliza nafasi ya kwanza kwenye kundi lake ndiyo itakayotinga hatua inayofuata ya kuwania tiketi tano za kushiriki fainali hizo.

Kwa Ukanda wa Afrika unatakiwa kutoa wawakilishi watano tu kushiriki fainali hizo, hivyo baada ya kupatikana timu 10 zitakazoongoza makundi yao, kutachezwa tena mechi za mchujo ili kupata miamba mitano itakayotinga Qatar mwakani.

Kwa mantiki hiyo, Stars inatakiwa kupigana kiume katika mchezo huo wa kesho huku ikihakikisha haipoteza mechi yoyote hususan inapokuwa uwanja wake wa nyumbani na kisha ugenini kwenda kusaka matokeo chanya ama angalau sare, lakini si kukubali kupoteza.

Tunaamini kwa soka ililoonyesha Ijumaa tena ikiwa ugenini nchini DR Congo, Stars ina nafasi kubwa ya kupata matokeo chanya kesho kama wachezaji watajituma zaidi na kuona thamani ya kuvaa jezi ya taifa kwa niaba ya Watanzania zaidi ya milioni 50.

Aidha, Nipashe tunatambua mashabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani hususan timu inapokuwa uwanja wake wa nyumbani, hivyo kila mmoja kwa nafasi yake kesho iwe siku ya kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenda kuipa sapoti Stars katika mchezo huo ambao ni wazi utakuwa mgumu kwa kila upande.

Matarajio yetu si kuona idadi kubwa ya mashabiki wakijitokeza kwa wingi uwanjani pekee, bali pia kuwashuhudia wakibeba jukumu lao la kushangilia mwanzo mwisho katika mchezo huo, ambao kama Stars ikishinda inaweza kuwa miongoni mwa timu zitakazokuwa katika nafasi nzuri ya kuongoza kundi lao.

Tunatambua matokeo chanya pekee kwa Benin, ndiyo yanayoweza kuizuia Stars kukaa kileleni endapo tu itashinda kesho, kwani kama Wabenin hao watapoteza, DR Congo itakuwa na pointi sawa na Tanzania ikishinda, lakini endapo Wakongomani hao watapoteza basi Benin itaendelea kuongoza kundi hilo.

Hivyo, biashara kwa Stars inapaswa kuwa mapema kwa kutafuta matokeo kwenye mechi hizi za awali, na haipaswi kujisuasua hadi kusubiri matokeo ya mechi za raundi ya mwisho kuanza kupiga hesabu za kuombea timu nyingine kupoteza katika kundi lake ili kupata nafasi ya kusonga mbele.

Ingawa tunatambua hautakuwa mchezo rahisi kwa Stars hasa ukizingatia Madagascar ilipoteza mchezo wa awali, hivyo itataka angalau kupata pointi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele, lakini dhamira, kujitoa na kuthamini jezi ya taifa kwa wachezaji wakiungwa mkono na mashabiki kuishangilia mwanzo mwisho, hakuna litakaloshindikana kesho kwa Mkapa.

Habari Kubwa