Takwimu sahihi mahitaji sukari nchini zizingatiwe

05Sep 2017
Mhariri
Nipashe
Takwimu sahihi mahitaji sukari nchini zizingatiwe

KUNA taarifa kuwa taifa halina takwimu sahihi za mahitaji halisi ya sukari kwa mwaka. Hali hiyo ilijidhihirisha wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

Wakati akizungumza na watumishi wa umma na wale wa vyama vya siasa katika ziara yake hiyo iliyokuwa siku moja kutembelea shamba la miwa na eneo litakalojengwa kiwanda cha sukari cha Mbigiri, Dakawa mkoani humo, Waziri Mkuu alieleza wazi kutofurahishwa na hali hiyo.

Alisema wazi kuwa miongoni mwa wale wanaosababisha tatizo hilo ni Bodi ya Sukari (SBT), ambao wameshindwa kufanya utafiti, ili kujua mahitaji halisi ya sukari nchini.

Waziri Mkuu alisema mahitaji yanayotajwa sasa na bodi hiyo ni tani 600,000 kwa mwaka, kiasi ambacho ni cha kutilia shaka juu ya uhalisia wake kutokana na idadi ya watu waliopo nchini. Kiasi kinachozalishwa ni tani 320,000 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, taifa lina watu wanaokadiriwa kuwa milioni 50, takribani sawa na idadi ya watu wa Kenya ambayo yenyewe, mahitaji yake ya bidhaa hiyo kwa mwaka ni tani 800,000.

Kwa sababu hiyo, Waziri Mkuu aliwataka SBT wafanyie kazi suala hilo mara moja, hasa kwa kutambua kuwa tayari jambo hilo walishaagizwa kulitekeleza tangu Oktoba mwaka jana.

Hakika, kutokuwapo kwa takwimu sahihi za mahitaji ya sukari nchini siyo jambo lililotarajiwa. Ndiyo maana Waziri Mkuu amelizungumzia jambo hilo kwa hisia kali, lengo likiwa ni kuwafikishia ujumbe viongozi wa SBT, ili waamke na kutekeleza wajibu huo.

Sisi, kama ilivyo kwa Watanzania wengine, wenye ndoto ya kuona kuwa taifa linapiga hatua zaidi za kiuchumi, tunaungana na Waziri Mkuu katika kuona kuwa jambo hilo linafanyiwa kazi. Tunasisitiza hilo, ili watu wa Bodi ya Sukari watambue kuwa suala hilo siyo la kucheleweshwa tena.

Kimsingi, kutokuwapo kwa taarifa sahihi za mahitaji ya sukari kuna athari kubwa kwa uchumi wa nchi. Ni kwa sababu sukari ina umuhimu kwa matumizi ya nyumbani na viwandani ambako hivi sasa inatajwa kuwa kiwango kinachohitajika kwa mwaka ni tani 100,000.

Kutokuwapo kwa takwimu sahihi kunaathiri uchumi kupitia uagizaji wa bidhaa hiyo nje ya nchi. Kwa mfano, kama itabainika kupitia utafiti huo kuwa kiwango cha mahitaji ya sukari nchini ni tani milioni moja na siyo 600,000 kama inavyoelezwa sasa, maana yake ni kuwa tofauti iliyopo imekuwa ikitoka nje kila mwaka na kunufaisha zaidi mataifa yenye kutuingizia bidhaa hiyo.

Aidha, ni kupitia takwimu kama hizo ndipo huonekana umuhimu wa kujenga haraka viwanda vya bidhaa hiyo muhimu kwa matumizi ya kila siku kwa kila nyumba na pia viwanda vya bidhaa mbalimbali ambavyo huitumia kama malighafi, ikiwamo vile vya vitafunwa na vinywaji baridi vya soda na juisi.

Ni wazi kwamba kuwapo kwa taarifa sahihi za mahitaji ya sukari nchini kutaongeza kasi ya uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda zaidi vya bidhaa hiyo na mwishowe manufaa yake kuwagusa Watanzania moja kwa moja kupitia ajira na kodi. Na mambo hayo ni vigezo muhimu katika kujipima juu ya kuimarika kwa uchumi wa nchi.

Ni kwa kutambua yote hayo, ndipo sisi tunapoona kuwa sasa kuna kila sababu kwa wadau wa sukari nchini kuona umuhimu wa kuwapo kwa taarifa sahihi za mahitaji halisi ya sukari nchini.

Shime, Bodi ya Sukari iamke sasa na kufanyia kazi agizo la serikali haraka iwezekanavyo, ili mwishowe kuwe na takwimu sahihi za matumizi ya sukari nchini zitakazosaidia katika mchakato wa kuinua uchumi, hususan kupitia viwanda vyenye kutumia bidhaa hiyo kama malighafi.

Habari Kubwa