TFF, Bodi ya Ligi andaeni ratiba rafiki msimu mpya

31Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TFF, Bodi ya Ligi andaeni ratiba rafiki msimu mpya

SHIRIKISHO la Soka Nchini (TFF), tayari limeshafungua dirisha la usajili wa wachezaji ambao watashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na Ligi Kuu ya Wanawake kwa ajili ya msimu mpya wa 2021/2022.

Kwa upande wa Ligi Kuu Tanzania Bara, msimu ujao utakuwa na timu 16 ambazo ni mabingwa Simba, Yanga, Azam, Biashara United, Namungo, KMC, Polisi Tanzania, Kagera Sugar, Dodoma Jiji, Ruvu Shooting, Mbeya City, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar, Coastal Union, Mbeya Kwanza na Geita Gold FC.

Usajili huo utafungwa rasmi ifikapo Agosti 31, mwaka huu na TFF imesisitiza klabu zote kuzingatia kalenda hiyo kwa sababu hakutakuwa na muda wa nyongeza katika kukamilisha mchakato huo muhimu.

Ili kufanya vyema katika msimu ujao, klabu zote zinakumbushwa kufanya usajili mzuri ili kuwa na vikosi imara ambavyo vitaonyesha ushindani na si kuwa wasindikizaji kwenye ligi hizo na mashindano mengine ya ndani na nje ya nchi watakayoshiriki.

Timu pia zinakumbushwa kuboresha mabenchi ya ufundi kwa kuajiri makocha wenye sifa na uzoefu wa kushiriki ligi hizo pamoja na mashindano ya kimataifa kwa klabu nne ambazo msimu ujao zitapeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Klabu zikumbuke kufanya usajili kwa kufuata mapendekezo ya kiufundi waliopewa na makocha walioziongoza timu hizo na kuacha kusajili wachezaji kwa kusikiliza 'kelele' za mashabiki wao ambao kiufundi hawana nafasi.

Nipashe inazikumbusha klabu kusajili wachezaji ambao watakwenda kuimarisha vikosi vyao na si kwenda kusotea benchi, lakini hili pia likibakia kwenye uamuzi wa wachezaji husika ambao hukubali kuweka saini katika timu ambazo wanafahamu kupata namba ya kucheza ni kitendawili.

Umefika wakati wa kuwakumbusha wachezaji wetu kufanya uamuzi wa kujiunga na timu itakayomsaidia kuendeleza kipaji chake na si kuzingatia kipengele kimoja tu cha maslahi, kama ambavyo tumeshuhudia kwa baadhi ya nyota wakipotea, hali ya kuwa walitarajiwa kulitangaza taifa vyema ndani na nje ya Tanzania.

Baada ya klabu kukamilisha mchakato wa usajili kwa usahihi na kukamilisha programu za mazoezi vyema, sasa kilichobaki ni kwa wasimamizi TFF kupanga ratiba rafiki ambayo haitaumiza wachezaji wetu kama ambavyo tumeshuhudia katika misimu miwili iliyopita.

TFF inatakiwa kuhakikisha inatoa ratiba rafiki itakayowapa wachezaji nafasi ya kupumzika na kuonyesha viwango vyao halisi na si kwenda vituoni kukamilisha ratiba hizo.

Tayari inafahamika msimu ujao ambao utaanza mapema Septemba, mwaka huu, Tanzania itawakilishwa na timu nne katika mashindano ya CAF, TFF isione aibu kuomba msaada kwa nchi zilizoendelea katika kusaidia au kushauri upangaji wa ratiba ili suala la klabu moja kuwa na idadi kubwa ya mechi za viporo lisijirudie.

Mechi za viporo zinapokuwa nyingi, hupunguza ushindani lakini huruhusu malalamiko yasiyo na msingi kwa sababu baadhi ya mechi huchezwa kwa kukamilisha ratiba na jambo hilo hupunguza ushindani, lakini vile vile linaweza 'kuamsha' upangaji wa matokeo.

Pia tunakumbusha ratiba hiyo isisahau kuzingatia jiografia ya Tanzania na hali halisi ya kiuchumi ya klabu zetu kwa kujaribu kuzipangia kucheza mechi zote inapokwenda kwenye ukanda mmoja. Hii itasaidia timu kucheza kwa amani na vile vile kupata muda wa kufanya mazoezi kila baada ya kumaliza mchezo mmoja.

Tunaendelea kuwakumbusha Ligi Kuu Tanzania Bara ndio tegemeo kubwa la Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen kupata wachezaji ambapo hupeperusha bendera ya nchi katika mashindano mbalimbali, hivyo kuifanya ligi hiyo kuchezwa kwa mtindo wa bora liende, itakuwa tu si kuziumiza klabu, lakini pia itaidhoofisha Stars.

Hakuna kisichowezekana, kama nchi za Ulaya timu zake zaidi ya sita hushiriki mashindano ya Ulaya na bado ratiba zao zinakuwa rafiki, kwa nini Tanzania ratiba ya Ligi Kuu huonekana imejaa idadi kubwa ya viporo? Tubadilike ili twende na kasi ya digitali ambayo nchi nyingine wanaitumia na mwisho wa msimu bingwa hupatikana bila ya kuwapo kwa malalamiko ya upendeleo au harufu ya kuandaliwa mshindi.

Habari Kubwa