TFF isitwishwe zigo la vibanda umiza

11May 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TFF isitwishwe zigo la vibanda umiza

BAADA ya kimya cha takriban mwezi mmoja na wiki tatu sasa, hatimaye Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imeweka wazi endapo itapata baraka za serikali inatarajia kuruhusu ligi za soka nchini kurejea mapema Juni mwaka huu.

Hatua hiyo ya TPLB imekuja baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kueleza anafikiria kwa siku zijazo kuruhusu ligi za soka kuendelea na anachosubiri ni kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wake.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli ilikuja wakati muafaka ambapo TPLB na Shirikisho la Soka nchini lilikuwa katika kikao cha pamoja kujadili hatima ya Ligi Kuu kufuatia agizo la Shirikisho la Soka Afrika, Caf.

Hiyo ni baada ya mwishoni mwa Aprili Caf kuwataka wanachama wake, ikiwamo TFF hadi ifikapo Mei 5, kila shirikisho kueleza hatima ya ligi yake endapo itaendelea ama kufutwa ili iweze kupanga kalenda yake ya michuano mbalimbali.

Caf ililazimika kutoa kauli hiyo kutokana na karibu ligi zote barani Afrika kusimama kwa kipindi kisichojulikana baada ya mlipuko wa maambukizo ya virusi vya corona (COVID-19), ambavyo hadi jana mchana jumla ya watu 4,114,896 duniani kote walishabainika kupatwa na maambukizo huku waliopona wakiwa 1,445,980 na waliopoteza maisha wakiwa 280,564.

Kwa Tanzania pekee maambukizo yamefikia 509, vifo vikiwa 21 na waliopona wakiwa 183, idadi hiyo ikiwa ni ongezeka la watu 508 kutoka mtu mmoja aliyekuwa na maambukizo wakati serikali inatangaza kusitisha shughuli zote zinazosababisha mikusanyiko ya watu ikiwamo michezo Machi 17, mwaka huu.

Tayari TFF imeeleza kuwa wakati ikisubiri baraka za serikali ya ruhusa ya ligi hiyo kurejea, mbali na tahadhari zote kufuatwa kama inavyoelekezwa na wizara ya afya, pia huenda wakaruhusu mashabiki wachache mno kuingia viwanjani ama kuwazuia kabisa.

Hata hivyo, kumeibuka mjadala mzito kutoka kwa wadau wa soka wakihoji namna TFF itakavyoweza kuzuia mashabiki wanaokusanyika katika kumbi mbalimbali za starehe, baa na vibanda umiza kushuhudia mechi.

Wengi wanadai ni rahisi kwa TFF kuzuia mashabiki kuingia viwanjani wakati wa mechi, lakini ni kazi kubwa kwa shirikisho hilo kuweza kuzuia watu kukusanyika katika vibanda umiza na kumbi za starehe kuangalia mechi jambo ambalo wanaona kuruhusiwa kurejea kwa ligi hiyo kutazidisha maambukizo.

Kwanza kabisa kama ambavyo katika nyakati tofauti Rais Magufuli amenukuliwa akisema Watanzania waendelee kuchapa kazi na kuchukua tahadhari zote kama inavyoelekezwa na wizara ya afya, tunaunga mkono kauli hiyo.

Pia tukumbuke Ujerumani ambapo kuna jumla ya watu 171,324 waliopatwa na maambukizo huku vifo vikiwa 7,549 na walipona kati yao wakiwa 144,400, idadi ambayo ni zaidi ya Tanzania, lakini serikali ya nchini humo imeruhusu Ligi Kuu ya Bundesliga kuendelea na inatarajiwa kurejea rasmi Jumamosi wiki hii kwa tahadhari zote kuchukuliwa, hivyo hili la kuhofia mashabiki kurundikana katika vibanda umiza lisiwe sababu ya kuzuia ligi kurejea.

Na katika hilo, jukumu la TFF liendelee kubaki kuhakikisha tahadhari zote zinachukuliwa endapo wataruhusu mashabiki wachache kuingia viwanjani ikiwa ni pamoja na kulinda afya za wachezaji, lakini hili la vibanda umiza na baa linapaswa kuwa la kila mmoja kuchukua tahadhari.

Tunasema hilo kwa kuamini kuwa elimu ambayo imeshatolewa na inayoendelea kutolewa kila uchao kuhusu namna ya kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona imewafikia wengi na ni wakati sasa wa kuchapa kazi na kuendelea kuchukua tahadhari.

Hivyo, shughuli za kiserikali, uzalishaji mali ikiwamo michezo na maisha ya kila siku lazima yaendelee huku kila mmoja akichukua tahadhari ya kujikinga na janga hili la dunia.

Habari Kubwa