TFF itembee kwenye mstari wake, isipangue ovyo ratiba Ligi Kuu

23Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TFF itembee kwenye mstari wake, isipangue ovyo ratiba Ligi Kuu

MAPEMA wiki hii, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitoa ratiba ya msimu mpya wa michuano ya Ligi Kuu Bara.
Kwa mujibu wa shirikisho hilo, michuano hiyo imepangwa kuanza Agosti 20 mwaka huu.

Tunaamini muda ulitolewa ratiba hiyo unatosha kwa timu kujiandaa vizuri kabla ya kushuka dimbani.

Hata hivyo, kama wadau wa michezo tungependa kuchukua fursa hii kuishauri TFF kusimamia vizuri ratiba hiyo ili kupunguza malalamiko kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Wote ni mashahidi, msimu uliopita tulishuhudia madudu mengi yaliyofanywa na TFF katika kusimamia ratiba yake yenyewe.

Usimamizi mbovu, kupanguliwa ovyo ratiba za mechi na malalamiko mengi dhidi ya waamuzi, yaliifanya TFF kuwa kiini cha lawama msimu mzima.

Upanguaji mbovu wa ratiba ndiko kulikoifanya Yanga kumaliza mechi zake nne za mwisho ugenini.

Ni jambo la ajabu kwenye ligi timu moja inabaki na viporo vya mechi nne na zote zinachezwa ugenini.

Uamuzi huo wa TFF ulilalamikiwa na wadau wengi wa michezo hasa klabu ya Simba iliyotishia kutopeleka timu uwanjani hadi wapinzani wao Yanga watakapomaliza mechi zao za viporo.

Leo TFF imetoa tena ratiba ya ligi kuu, tukiamini yale yaliyoifanya TFF kupoteza imani kwa wadau hayatarudiwa tena.

Tungependa kuona TFF ikijipanga upya na kuendesha ligi katika utararibu utakaopunguza kama siyo kufuta kabisa malalamiko.

Msimu huu uwe alama ya TFF kujirekebisha kwa yale yaliyotokea msimu uliopita kwa kuendesha ligi vizuri na kuepuka kupangua ratiba bila sababu za msingi.

Tunatambua kuwa ratiba ya safari hii imezingatia kalenda za mashindano ya kimataifa, hivyo hatutashuhudia tena migongano kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Lakini pia tunaamini kuwa, kama TFF itaamua kuondokana na utumwa wa kubeba lawama kila msimu, Nipashe, tunaamini kama TFF itaamua kusimamia vizuri kanuni na sheria zake, hakuna shaka msimu huu utakuwa na mvuto.

Tungependa kuona msimu huu bingwa anapatitaka bila kuwapo na manung'uniko wala lawama dhidi ya waamuzi.

Tunafahamu kuwa kwenye ushindani wowote, malalakino hayawezi kukosekana, lakini haitakuwa na maana kama malalamiko yatakuwa yeleyale kila msimu.

Nipashe, tunachukuwa nafasi hii pia kuzitaka timu zitakazoshiriki michuano hiyo kutumia vizuri muda mfupi uliobaki kujiandaa na michuano hiyo.

Habari Kubwa