TFF iwe makini mrithi wa Wambura TPLB

19Oct 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TFF iwe makini mrithi wa Wambura TPLB

JUMANNE wiki hii, Shirikikisho la Soka nchini (TFF), lilitangaza rasmi kuwa kesho yake [Jumatano], litaanza mchakato wa kumtafuta Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), kufuatia aliyekuwa akikalia nafasi hiyo, Boniface Wambura, kumaliza mkataba wake.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, akitangaza uamuzi huo, alisema Jumatano wiki hii wangeanza kutoa matangazo kwa ajili ya wadau mbalimbali wa soka kuomba nafasi hiyo muhimu kwa ajili ya kuliongoza soka la nchi hii.

Aidha, Wambura ambaye amewahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na baadaye Ofisa Habari wa TFF, amepewa majukumu mengine ambapo sasa atakuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Masoko wa TFF akishirikiana na Clifford Ndimbo katika upande wa habari wakati Aaron Nyanda, atafanya naye kazi za kutafuta masoko.

Tunampongeza Wambura si tu kwa majukumu mapya aliyopewa, bali kwa changamoto kubwa alizokabiliana nazo wakati akiwa Mtendaji Mkuu TPLB, kwani ni idara ambayo inahitaji umakini mkubwa na uelewa wa kutosha wa masuala ya soka.

Hivyo, tunatumai ataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika majukumu yake mapya, lakini pia pale mrithi wake katika nafasi ya Mtendaji Mkuu wa TPLB atakapopatikana.

Hata hivyo, kuelekea mchakato mpya wa kumsaka mrithi wa Wambura, tunaitaka TFF kuwa makini na kuifanya kazi hiyo kwa kutumia weledi wa hali ya juu kwani idara hiyo ndiyo mhimili mkubwa wa soka la Tanzania.

Kwa muda mrefu klabu, makocha, mashabiki na wadau wa soka kwa ujumla wamekuwa wakilalamikia suala zima la mabadiliko ya ratiba ya Ligi Kuu mara kwa mara, jambo ambalo mara nyingine tumeshuhudia timu moja ikiwa na viporo hadi zaidi ya sita kwa kisingizio tu inashiriki michuano ya kimataifa ambayo kalenda yake hutoka mapema hata kabla ya ile ya Ligi Kuu kupangwa.

Hali kadhalika, msimu uliopita tulishuhudia ukimalizika bila Ligi Kuu kuwa na mdhamini jambo ambalo hadi leo haijajulikana bingwa wa ligi hiyo, Simba atapewa zawadi gani mbali na kombe ambalo walikabidhiwa.

Kwa hayo machache tu, bila kuwa na Mtendaji Mkuu wa TPLB, mwenye taaluma ya kutosha atakayeweza kuunda timu yake imara ya kufanya nayo kazi, hakika soka la Tanzania litaendelea kuwa la kujikongoja na itakuwa vigumu kuweza kufikia kule tunapopatamani walipo wenzetu waliopiga hatua kisoka.

Aidha, pamoja na mchakato ambao Nipashe tunaamini TFF itauendesha kwa umakini na weledi wa hali ya juu kabisa bila kutazama itikadi ya vyama, siasa, dini ama klabu kwa manufaa ya soka letu, pia tunataka utakapokamilika na kuiacha Bodi ya Ligi kuwa huru kama ambavyo zinavyofanya nchi za wenzetu zilizopiga hatua kisoka.

Tunatambua hata kama TFF itafanikiwa kumpata Mtendaji Mkuu wa TPLB mwenye taaluma ya kutosha na makini katika kazi hiyo, kama hatakuwa huru katika kutekeleza majukumu yake, itakuwa ni kazi bure kwani tutaendelea kuyashuhudia madudu yale yale ambayo hatutamani kuyaona katika soka letu.

Tunaamini Rais wa TFF, Wallace Karia na Katibu wake, Kidao si tu watahakikisha mchakato huo haufanyiki kwa lengo la maslahi yao binafsi, bali watamulika zaidi nani anayeweza kuleta mapinduzi mapya kwenye ligi yetu ikiwa ni pamoja na kuwezesha vyanzo vingi vya mapato vinazidi kupatikana.

Ni aibu kubwa kwa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo tunaamini ni miongoni mwa ligi bora kabisa Afrika Mashariki na Kati na inayotazamwa zaidi, kuwa na wadhamini watatu tu, Kampuni ya Vodacom ambao ni wadhamini wakuu, Benki ya KCB wadhamini wenza pamoja na Azam TV inayodhamini upande wa kurusha matangazo ya mechi.

Hivyo, kama TFF itakuwa makini katika kumtafuta Mtendaji Mkuu wa TPLB lakini pia ikatoa uhuru kwake katika kutekeleza majukumu yake, ni wazi tutashuhudia soka letu likipiga hatua kubwa na kuvutia wawekezaji wengi kuliko ilivyo sasa.

Ni matumaini yetu TFF itazingatia hayo tuliyoyaeleza ili kuliinua soka letu hususan Ligi Kuu ambayo kwa sasa imeanza kuwa kivutio kikubwa ndani na nje ya nchi kwa makocha wengi na wachezaji kuvutiwa kuja kufanya kazi nchini.

Habari Kubwa