TFF izishushe daraja timu zilizopanga matokeo

15Feb 2016
Mhariri
Nipashe
TFF izishushe daraja timu zilizopanga matokeo

MATOKEO ya kupangwa ya mechi mbili za Ligi Daraja la Kwanza kati ya Geita Gold ya Geita dhidi ya JKT Kanembwa na Polisi Tabora dhidi ya JKT Oljoro, hayawezi kupita bila kukemewa vikali.

Matokeo ya mechi hizo yana shaka kubwa, siyo kwa sababu timu hazina uwezo wa kufungana mabao mengi kiasi hicho, lakini tunaposimama kwenye mstari wa kweli, tunaamini kulikuwa na mipango ya makusudi ya kuachiana mabao kwa timu hizi.

Katika mechi hizo, ambazo timu mbili zilikuwa zinawania nafasi moja ya kupanda kucheza Ligi Kuu Bara, zilimaliza dakika tisini na matokeo ya ajabu.

Geita iliifunga JKT Kanembwa mabao 8-0, Polisi ikaishushia mvua ya mabao 7-0 JKT Oljoro.

Ingawa tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeyafuta matokeo hayo ili kupisha uchunguzi, lakini hiyo haiondoi doa wala aibu iliyoachwa na timu hizo kwenye soka letu.

Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya timu kucheza chini ya kiwango ili kutoa matokeo ya kuzisaidia baadhi ya timu.

Hata kama hakukuwahi kutolewa kemeo kubwa kutoka mamlaka husika, lakini kilichotokea kwenye mechi hizi mbili ni ushahidi tosha.

Soka letu limekuwa likirudi nyuma kila siku badala ya kusonga mbele na sababu, huku rushwa ikiwa kiini cha kusababisha hali hiyo.

Pamoja na kuipongeza TFF kwa hatua waliyochukua, lakini kuna kila sababu ya mamlaka hiyo inayoratibu na kuendesha mchezo wa soka nchini kuchukua hatua kali.

Ni hatari kubwa kuacha kuchukua hatua katika mazingira ya kuharibu mchezo wa soka kama zilivyofanya timu hizo.
Tunadhani, ipo haja kubwa kwa TFF kuzipa adhabu timu hizo, siyo tu wachezaji bali hata viongozi wake kwa sababu wapo pia ni sehemu ya kutengeneza aibu hii.

Lakini pia tunadhani hata waamuzi waliochezesha mechi hizo nao kuchunguzwa kama kwa namna yoyote walihusika kuchawishi matokeo ya mechi hizo.

Kwa nchi zilizoendelea, japo tutoe mfano wa Italia baadhi ya timu zilishushwa daraja kwa kupanga matokeo, huku zingine zikipokwa pointi.

Tungependa kuona TFF inafuta aibu hii kwa kutoa adhabu kali kwa timu zilizohusika na ikibidi hata kuzishusha madaraja ya chini ili iwe fundisho kwa timu zingine.

Hatuwezi kufunga macho na kuruhusu aibu kama kuteka soka letu linalohitaji ustawi ili kupata mafanikio.
Kinyume na adhabu kali dhidi ya waliohusika kupanga matokeo haya, maana yake ni kamba tumebariki rushwa katika soka letu.