TFF, klabu sasa ni wakati wa kutafuta wadhamini

17Jun 2019
Mhariri
Nipashe
TFF, klabu sasa ni wakati wa kutafuta wadhamini

TAYARI tumeshuhudia timu zilizoshuka kutoka Ligi Kuu Bara hadi Ligi Daraja la Kwanza kufuatia msimu wa 2018/19 kumalizika tangu Mei 28, mwaka huu.

Katika ligi hiyo iliyojumuisha jumla ya timu 20 kwa mara ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu Tanzania Bara, zilizoshuka ni African Lyon ya jijini Dar es Salaam na Stand United ya mkoani Shinyanga.

 

Aidha, kuelekea msimu mpya wa 2019/2020 unaotarajiwa kuanza Agosti mwaka huu, timu zilizopanda Ligi Kuu ni Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi na Polisi Tanzania ya Kilimanjaro.

Hata hivyo, msimu uliomalizika wa 2018/19, ulitawaliwa na changamoto nyingi za ndani ya uwanja zikiwamo waamuzi kuchezesha chini ya kiwango ama kinyume cha sheria 17 za soka na nyingine nyingi.

Kwa upande wa changamoto nje ya uwanja, ukiachilia mbali viporo vya Klabu ya Simba vilivyotokana na kushiriki michuano ya kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika, tumeshuhudia Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF),  ikishindwa kuandaa ratiba rafiki kulingana na uchumi wa wanachama wake ambao ni klabu.

Lakini kubwa kuliko ni bingwa wa Ligi Kuu, Simba kuishia kukabidhiwa kombe tupu pasipo zawadi yoyote, hali hiyo ikitokana na kukosekana kwa mdhamini mkuu. Hakika ilikuwa ni ligi ngumu si tu kutokana na ratiba ndefu iliyotokana na kushirikisha timu 20, bali changamoto kubwa ilikuwa ni hali ya uchumi kwa klabu shiriki.

Hivyo, wakati huu klabu zikiendelea kujiandaa kwa msimu mpya, hazina budi kujipanga ipasavyo hususan kwa upande wa kujizatiti kiuchumi kwa kutafuta wadhamini wao binafsi badala ya kuitegemea TFF kutafuta mdhamini mkuu.

Ni wazi suala la kutafuta mdhamini wa Ligi Kuu kwa TFF, limeonekana kuwa changamoto kubwa, hivyo klabu zinapaswa kuingia sokoni rasmi kutafuta wadhamini wao binafsi.

Ikumbukwe mdhaminni mkuu wa ligi hapaswi kuwa chanzo kikuu cha mapato kwa klabu bali ni jukumu kwa kila klabu kujitafutia wadhamini wake mfano wa jezi na vifaa vingine vya michezo, ili kujiimarisha kiuchumi.

Nipashe tunashangaa kuona klabu zikielekeza lawama kwa TFF kufuatia shirikisho hilo kushindwa kupata mdhamini mkuu jambo ambalo zinadai limechangia hali ngumu kwao kiuchumi katika kujiendesha.

Sisi tunakiri ni aibu kwa TFF kushindwa kutoa zawadi kwa bingwa wa Ligi Kuu na kuishia kupewa kombe na medali tu, lakini si kwa klabu njaa zao kuzielekeza TFF kwa kushindwa kupata mdhamini mkuu wa ligi hiyo.

Tunatambua kote duniani klabu hujiendesha kwa kutumia vyanzo vyake binafsi vya mapato na si kwamba hutegemea wadhamini wa shirikisho husika.

Katika hili, pia TFF inapaswa kulaumiwa kwa kupunguza hamasa, msisimko na ushindani kwenye Ligi Kuu kutokana na timu kucheza pasipo kujua bingwa, mshindi wa pili hadi wa tatu ama wa mwisho anazawadiwa nini.

Lakini katika hilo pia, TFF haina budi kuimarisha kitengo chake cha masoko ili kutafuta wadhamini na kutangaza mapema bingwa hadi mburuza mkia atavuna nini kabla ya ligi kuanza.

Ni vema kutambua kuwa ligi iliyo bora haiishii tu kumzawadia bingwa ama mpaka mshindi wa tatu, bali zawadi huanzia kileleni hadi mkiani, na kwa kufanya hivyo huongeza ushindani kwa kuwa kila nafasi ya juu ina kiwango cha kupendeza cha zawadi.

Hilo likifanyika itakuwa vigumu pia kuona hata baadhi ya timu zikihofiwa kupanga matokeo kwenye mechi za mwisho kutokana na kuwania zawadi katika kila nafasi, hivyo ni wakati sasa kwa TFF na klabu kuanza kujipanga mapema kwa kutafuta wadhamini.

Habari Kubwa