TFF, klabu tupieni jicho mabadiliko ya kanuni

05Aug 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TFF, klabu tupieni jicho mabadiliko ya kanuni

ZIBAKI siku 18 kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuanza rasmi, ligi hiyo ikitarajiwa kushirikisha timu 20 kama ilivyokuwa msimu uliomalizika wa 2018/19.

Kuelekea msimu huo mpya kwa sasa timu zipo katika maandalizi makubwa zikicheza mechi kadhaa za kirafiki kujaribu vikosi vyao kabla ya mtanange huo kuanza rasmi Agosti 23, mwaka huu.

Maandalizi hayo kwa timu pekee, bali pia tumeshuhudia Shirikisho la Soka nchini (TFF), kwa kushirikiana na kamati yake ya waamuzi na Chama cha Waamuzi nchini, likiendesha semina kwa waamuzi pamoja na mazoezi ya utimamu kimwili.

Lengo la semina hiyo ikiwa ni kuwafanya waamuzi kuwa fiti kimwili lakini pia kuelewa mabadiliko muhimu yaliyojifanyika katika sheria mbalimbali za mchezo huo.

Hilo ni jambo la msingi ambalo pia linatakiwa kuambukizwa kwa klabu na TFF haina budi kuwakumbusha wanachama wake ambao ni klabu kutoa darasa kwa wachezaji, viongozi na hata mabenchi yao ya ufundi.

Hadi sasa ni Klabu ya Simba pekee ambayo tulishuhudia ikitoa darasa hilo la mabadiliko ya kanuni mbalimbali za soka kwa wachezaji wake kabla ya kuelekea kambini Afrika Kusini.

Kutokana na malalamiko mengi yaliyoelekezwa kwa waamuzi msimu uliopita, Nipashe tunaona ipo haja kubwa kwa kila klabu kualika wataalamu wa soka ili kutoa darasa hilo la mabadiliko ya kanuni hizo.

Tunaamini waamuzi pekee kupewa darasa hilo haitasaidia kuondoa malalamiko kwa kuwa bado wachezaji watakuwa wakiamini wameonewa pindi wanapoadhibiwa kulingana na mabadiliko hayo ya kanuni kutokana na kutozifahamu.

Tayari TFF kupitia Chama cha Waamuzi nchini imeshakamilisha wajibu wake kwa waamuzi watakaochezesha Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza, hivyo ni wakati wa klabu sasa kutoa darasa kwa wachezaji wao na mabenchi yao ya ufundi kabla ya ligi kuanza.

Nipashe kama wadau wa soka hatutaki kabisa kuona malalamiko ya msimu uliopita kwa waamuzi yakijirudia tena msimu huu mpya.

Lakini wasiwasi wetu ni kwamba msimu huu kuna uwezekano mkubwa waamuzi wakabebeshwa lawama zisizowahusu kutokana na wachezaji, makocha, viongozi wa klabu na hata mashabiki kutofahamu mabadiliko hayo.

Hivyo kuna haja kubwa kwa TFF kuzisisitiza klabu kuona haja ya kutoa darasa kwa wachezaji wao ili kuepuka lawama zinazoweza kuelekezwa kwa waamuzi kutokana na uelewa mdogo wa mabadiliko ya kanuni zilizofanyiwa marekebisho.

Lakini pia sote tunafahamu kama si kushuhudia baadhi ya wachambuzi wa soka na wanahabari kupitia vyombo vyao vya habari (si Nipashe) kutokana na uelewa wao mdogo wa kanuni, wakiongeza mihemko kwa mashabiki wa soka, hivyo waamuzi kuonekana wamevurunda na kuadhibiwa.

Kwa mantiki hiyo, TFF haina budi kutazama upande huu wa pili kwa kuwaandalia semina wanahabari kabla ya ligi kuanza na kuweza kukumbushana baadhi ya kanuni zilizofanyiwa marekebisho jambo litakalosaidia kufikisha ujumbe/habari sahihi kwa mashabiki.

Lengo letu ni kuona malalamiko yakipungua kama si kuisha kabisa na hatimaye kupatikana bingwa halali ambaye ataiwakilisha vema nchi kwenye michuano ya kimataifa na hilo litawezekana tu kwa TFF kulimulika hili pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza msimu uliopita.

Habari Kubwa