TFF, klabu zitupie jicho mikataba hii ya mkopo

21Dec 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TFF, klabu zitupie jicho mikataba hii ya mkopo

KWA sasa klabu za Tanzania zipo katika harakati za kuimarisha vikosi vyao, baada ya usajili wa dirisha dogo kufunguliwa rasmi kwa Tanzania Bara na hata ule wa visiwani Zanzibar.

Kwa Tanzania Bara, dirisha dogo lilifunguliwa tangu Desemba 16 na linatarajiwa kufungwa Januari 15, mwakani, wakati lile la Zanzibar likifunguliwa siku tano kabla na likitarajiwa kufungwa Januari 9, mwakani.

Kwanza ni uwanja mpana kwa klabu za Ligi Kuu Bara na Zanzibar pamoja na zile za Ligi Daraja la Kwanza na la Pili kuweza kutafuta wachezaji kuanzia Bara hadi visiwani kwa pande zote ili kuimarisha vikosi vyao kwa kuwa madirisha yote yapo wazi kwa sasa.

Tunatambua kufunguliwa kwa dirisha hilo ni nafasi pekee kwa klabu hususan kuweza kuboresha idara ambazo zilikuwa zimepwaya ama kuandamwa na majeruhi ili kuweza kujiimarisha kwa raundi ya pili ya ligi hiyo.

Aidha, Nipashe linafahamu katika dirisha hili wapo baadhi ya wachezaji watatemwa ili kutoa nafasi kwa nyota wapya ambao klabu husika zinaamini wanaweza kuzisaidia kutimiza malengo yao, lakini pia wapo walikuwa wanacheza kwa mkopo klabu zao zitahitaji kuwarejesha huku wengine wakitolewa kwa mkopo pia.

Hata hivyo, wakati huu harakati hizo za usajili zikiendelea kwa wachezaji kutoka klabu moja hadi nyingine, kumeanza kufurukuta mvutano kwa baadhi ya klabu kutokana na mikataba yao na wachezaji waliowatoa kwa mkopo kutokuwa na vipengele muhimu vinavyoweka mambo yote wazi.

Kwa siku takriban nne sasa, kumeibuka mvutano mkubwa kati ya Azam FC na Klabu ya Polisi Tanzania kuhusu mkataba wa mshambuliaji Ditram Nchimbi, anayedaiwa kupata baraka kutoka kwa klabu yake mama kusajiliwa na Yanga.

Kama ilivyo na inavyofahamika kwa klabu hizo mbili, ni kwamba Nchimbi alikuwa akiichezea Polisi Tanzania kwa mkataba wa mkopo akitokea Azam FC, ambao unaelezwa ulikuwa wa msimu mzima.

Kwa mujibu wa Polisi Tanzania walikubaliana na Azam kumtumia mchezaji huyo hadi mwishoni mwa msimu ndipo arejee klabuni kwake, na hapakuwa na kipengele chochote kinachoiruhusu Azam kumchukua katikati ya msimu, jambo ambalo linawafanya kupaza sauti za kumzuia kuuzwa Yanga.

Na kwa upande wa Azam FC inaeleza kwamba hapakuwa na kipengele chochote kinachoeleza kwamba hawataruhusiwa kumchukua mchezaji wao watakapomhitaji, huku wakiamini ni sawa na mtu kumpa mtoto wako akulelee, hivyo unapomhitaji unaweza kumchukua wakati wowote.

Azam pia, inaeleza baada ya Yanga kufika dau la kumnunua Nchimbi, ilitoa kipaumbele kwa Polisi Tanzania kama inamhitaji jumla imnunue, lakini ikawaeleza haina uwezo huo na kuwaruhusu kuendelea na taratibu zingine za kumuuza.

Kwa ujumla, Nipashe tumefuatilia kwa kina mvutano uliopo kwa klabu hizo mbili na kubaini kuna utata mkubwa na kutokuwapo kwa uwazi wa mikataba ya wachezaji wanaotolewa kwa mkopo kutoka klabu moja hadi nyingine.

Tunatambua mikataba ya mikopo kwa wachezaji huwa ina vipengele vingi muhimu na hawatolewi kiholela kama ambavyo klabu zetu nchini zinavyofanya, kwani; awali kabisani lazima mkopo huo uainishe wazi ni wa muda gani na nani hasa atamlipa mshahara mchezaji husika.

Pili mkataba wa mkopo unaweza kuwa na kipengele kwa klabu mama kumhitaji mchezaji wao muda wowote ama hataruhusiwa kucheza dhidi ya klabu yake hiyo pindi timu hizo zitakapokutana, lakini pia pindi itakapotaka kumuuza klabu anayoichezea kwa mkopo ipewe nafasi ya kwanza kumnunua na ikishindindwa ama kutohitaji tena huduma yake ndipo auzwe kwingineko.

Hayo ni machache tu katika mengi yanayopaswa kuwekwa wazi katika mikataba ya wachezaji wanaotolewa kwa mkopo, hivyo, Shirikisho la Soka nchini (TFF) na klabu kuna haja ya kukaa chini na kunyoosha mambo kwa kuhakikisha vipengele hivyo muhimu vinakuwapo ili kuepuka mivutano kama hii inayoendelea kwa Azam FC na Polisi Tanzania.

Habari Kubwa