TFF, TPLB umakini uongezwe mechi hizi za mwisho Ligi Kuu

05Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TFF, TPLB umakini uongezwe mechi hizi za mwisho Ligi Kuu

ZIMEBAKI takribani raundi mbili kwa timu 15 kati ya 18 zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kuhitimisha msimu huu wa 2020/21, ambao utashuhudiwa zikishuka timu nne moja kwa moja Ligi Daraja la Kwanza.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Simba ipo kileleni ikiwa na pointi 73 zilizotokana na mechi 30, huku Yanga ikiwa nafasi ya pili na alama zake 70 baada ya kushuka dimbani mara 32 sawa na Azam FC yenye pointi 64 katika nafasi ya tatu.

Hata hivyo, mbio za kuwania ubingwa zinaonekana kubaki kwa farasi mmoja, Simba kutokana na kuhitaji pointi nne tu katika michezo yake minne iliyobaki ili kutwaa taji hilo kwa mara ya nne mfululizo.

Yanga hata ikishinda michezo zake zote mbili zilizosalia, itafikisha pointi 76 huku Azam FC, yenyewe kama ikishinda itamaliza na alama 70, hivyo ni vigumu kwa timu hizo kuwa na matumaini ya kutwaa ubingwa huo kwa msimu huu.

Kwa upande wa zinazoshuka daraja, tayari Mwadui FC imeaga mapema Ligi Kuu kutokana na kuvuna pointi 19 tu katika mechi 32, hivyo hata kama ikishinda michezo yake miwili iliyobaki itaishia kufikisha alama 25 ambazo ni chini ya Coastal Union (34), Gwambina FC (34) na Ihefu FC yenye alama 35, zote zikipigana vikumbo kukwepa kushuka daraja.

Lakini Ruvu Shooting yenye pointi 38, Mtibwa Sugar (38), Kagera Sugar (37), Mbeya City (36) na JKT Tanzania pointi 36, nazo hazipo sehemu salama kwani endapo zikipoteza michezo yao miwili iliyobaki huku Coastal Union, Gwambina, na Ihefu FC zikishinda, nazo zinaweza kujikuta zikiwa timu tatu kati ya zitakazoungana na Mwadui kushuka daraja.

Ikumbukwe pia timu mbili zilizoongoza Kundi A na B, kwenye Ligi Daraja la Kwanza zimepanda moja kwa moja Ligi Kuu, huku zilizomaliza nafasi ya ya pili katika makundi hayo mawili zikisubiri kucheza mechi za mtoano dhidi ya zitakazoshika nafasi ya 13 na 14 kwenye Ligi Kuu ili kuwania nafasi mbili za kucheza ligi hiyo ambayo msimu ujao itajumuisha timu 16 tu kutoka 18 za sasa.

Hivyo, ni wazi kwa namna msimamo wa Ligi Kuu ulivyo kwa sasa, huku timu zinazowania kubaki Ligi Kuu msimu ujao zikipishana kwa pointi chache, ushindani utakuwa mkubwa sana katika michezo hii miwili iliyobaki kwa kila timu.

Kwa mantiki hiyo, Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB), wanapaswa kuongeza umakini kwenye michezo iliyobaki ili kuepuka upangaji wa matokeo hususan kwa timu zinazowania kubaki Ligi Kuu pindi zitakapokutana na zile ambazo tayari zipo salama na hazina cha kupoteza.

Tunatambua pia hujuma na upangaji matokeo, mkono wa rushwa unaweza kupitia kwa waamuzi ambao kwa misimu kadhaa sasa wamekuwa wakilalamikiwa kwa kuzifinyanga sheria 17 za soka, hususan wakati kama huu wa kuelekea mwishoni mwa msimu.

Kwa kuzingatia hilo, tunaitaka TFF na TPLB kuongeza umakini ili kahakikisha timu zitakazoshuka daraja ama kubaki Ligi Kuu, ziwe zile zilizostahili kutokana na uwezo wao na si kwa kubebwa kwa njia yoyote ile.

Hilo halipaswi kuachwa kwa TFF na TPLB pekee, bali pia hawana budi kushirikisha TAKUKURU, lakini pia viongozi wa klabu, makocha pamoja na wachezaji wakiwa mstari wa mbele kukataa kuhusishwa kwa namna yoyote ile katika upangaji huo wa matokeo.

Nipashe tunataka kuona Ligi Kuu msimu ujao ushindani ukiongezeka na ligi yetu kuzidi kuwa bora zaidi barani Afrika, hilo linawezekana tu kama timu zote 16 shiriki zitatokana na uwezo wao binafsi kisoka na si kubebwa kwa namna yoyote ile.

Habari Kubwa