TFF, TPLB wamulike marefa hawa kulinda ubora Ligi Kuu

29Nov 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TFF, TPLB wamulike marefa hawa kulinda ubora Ligi Kuu

HAKUNA ubishi Ligi Kuu Bara imekuwa kivutio kikubwa kwa watazamaji katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati na nidhahiri kushika nafasi ya nane kwa ubora barani Afrika imestahili.

Kwa kulitambua hilo, tuna kila sababu ya kutoa kongole kwanza kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bodi ya Ligi (TPLB), wadau wote wa soka hususan wadhamini kuanzia ngazi ya klabu hadi wa ligi hiyo pamoja na mashabiki wote kwa kuiunga mkono.

Wote tunatambua namna TFF na TPLB walivyotumia nguvu kubwa kuwashawishi wadhamini hadi kuandika historia kwa mara ya kwanza tangu ligi hiyo kuanzishwa nchini kuwapo kwa wadhamini wakubwa zaidi ya watatu walikubali kudhamini Ligi Kuu kwa mabilioni ya shilingi.

Lakini Watanzania kugeukia kuangalia mechi za Ligi Kuu Bara na kuacha ligi pendwa kama ya England, Hispania, Italia, Ujerumani na Ufaransa au wakati mwingine inapolazimu kuangalia zote kwa pamoja, hakika si kazi ya mchezo iliyofanywa katika kuiboresha na kuwa na mvuto.

Ubora huo pia umechangia kuzidi kuongezeka wachezaji wengi wa kigeni wanaovutiwa kuja kucheza soka nchini na si Ligi Kuu tu bali hata Ligi Daraja la Kwanza (Championship) kwa sasa wapo wageni wengi na wameongeza ushindani huko na viwango vya wachezaji wazawa.

Haya yote ni kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa katika klabu zetu hususan za Ligi Kuu, hivyo wachezaji na klabu za Championship kwa pamoja wanatamani kupanda kucheza Ligi Kuu ili kufaidi matunda hayo ya uwekezaji.

Tunaamini 'keki' iliyopo Ligi Kuu Bara ni tamu na ndiyo maana wachezaji mbalimbali wanavutiwa kuja kucheza hapa nchini, tena kutoka mataifa ambayo hapo mwanzo wakitoka kwao ni walikuwa wanakwenda moja kwa moja Ulaya ama nchi za Kiarubu kuliko na malipo mazuri.

Lakini kwa sasa Ligi Kuu kuna wachezaji kutoka Senegal, Mali na Ghana mataifa ni mara chache wachezaji wake kutoka kwao kucheza Afrika hususan ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Pia katika Klabu ya Simba kwa sasa tunashuhudia mchezaji ambaye ametoka kucheza michuano ya kuwania kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, Peter Banda, akiwa na FC Sheriff Tiraspol ya Moldova, ingawa tangu ajiunge na 'Wekundu wa Msimbazi' hao, bado hajapata nafasi ya kutosha kuonyesha uwezo wake, hayo yote ni matunda ya kuongezeka ubora wa Ligi Kuu.

Kutokana na ongezeko la nyota hao nchini, ni wazi ligi yetu itaendelea kutupiwa jicho kila kona barani Afrika na hata Ulaya kwa mawakala kuja kufuatilia vipaji ili kuvitafutia soko. Hivyo, huu ni wakati kwa TFF, TPLB kuongeza umakini na kuchukua hatua kali kwa wote ambao wanataka kuitia doa hususan waamuzi, ambao wakati huu ikiwa ndiyo ipo raundi ya saba msimu huu, malalamiko ya kutotenda haki yamekuwa mengi kwao.

Tunatambua yapo makosa ya kibinadamu na ndiyo maana hata wenzetu barani Ulaya, Asia na kwingineko, wamekuwa wakitumia teknolojia ya video ya kumsaidia refa (VAR) ili kuondoa utata ama lawama.

Lakini pamoja na kutotumia VAR katika ligi yetu, yapo makosa mengi ya wazi ambayo yamekuwa yakifanywa na baadhi ya waamuzi kwa makusudi ama mapenzi yao kwa baadhi ya klabu au pengine huenda ni kwa maslahi yao binafsi, hivyo kwa marefa hawa, hawana budi kuchukuliwa hatua kali.

Lengo letu ni kutaka kuona ligi yetu ikipanda viwango vya ubora na wachezaji wakipata soko nje ya nchi ili kuvutia wawekezaji zaidi, na hilo haliwezi kutokea kama waamuzi wanaovurunda wataendelea kufumbiwa macho. Katika hilo, ni vema pia TFF na TPLB ikamulika maslahi yao kwa mapana zaidi ili kuwapunguzia kuingia vishawishini.

Habari Kubwa