TFF,ZFA soka letu haliendishwi kwa malumbano yasiyo na tija

08Feb 2016
Mhariri
Nipashe
TFF,ZFA soka letu haliendishwi kwa malumbano yasiyo na tija

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) ndizo taasisi zenye mamlaka ya kusimamia mchezo wa soka Tanzania.

Pamoja na ukaribu wa taasisi hizi katika kusimamia soka, lakini historia haijawahi kuziweka mbali na malumbano ya mara kwa mara.
Taasisi hizi zimekuwa kwenye mitafaruku kwa muda mrefu pamoja na kuwa na jukumu moja la kusimamia maendeleo ya michezo.
Malumbano yaliyotokea hivi karibuni kati ya TFF na ZFA ni mwendelezo wa muda mrefu wa mgogoro wa kimasilahi kati yao.
Ukubwa wa suala hilo la kimasilahi, lilipelekea kujadiliwa bungeni ambako nako kulitokea mvutano kuhusu fungu la Zanzibar katika ustawi wa soka lake.
Lakini pia kauli aliyotoa Rais wa TFF Jamal Malinzi dhidi ya viongozi wa muda wa ZFA, inaonyesha wazi kuwa mamlaka hizi hazijakaa vizuri.
Lakini pia tishio la ZFA kumtaka Malinzi kufuta kauli yake au akubali kupelekwa mahakamani, ni ishara nyingine kwamba mambo hajakaa sawa.
Katika ustawi wa soka la kisasa ambalo ndilo msingi muhimu wa ajira na pato kwa taifa, malumbano na migogoro haina nafasi.
Tunafahamu kuwa TFF na ZFA vimekuwa vikilumbana kwa muda mrefu na kiini ni masilahi, lakini hali hii haina tamati?
Duru zinazoshughulikia migogoro, migongano na mitafaruku, siku zote huamini majadiliano kama alama ya kwanza kumaliza tofauti.
Je, TFF na ZFA hawatambui haya? Wana sababu gani kuendelea kulumbana, wana sababu gani ya kuendelea kutumia muda mwingi kuzungumzia migogoro inayoweza kumalizwa kwa kukaa pamoja na kujadiliana?
Sisi Nipashe hatushawishiki kukubali kwamba, linalozungumzwa Visiwani kuhusiana na ustawi wa soka halina maana.
Lakini pia TFF, ambayo imeshika mpini kwa sababu ya kutambulika na mamlaka za juu za usimamizi wa soka Afrika (CAF) na Duniani (Fifa), iwe na majibu ya kuridhisha.
Dhamira yetu siyo kusimama kwenye mstari wa kuamua nani mshindi kati ya ZFA na TFF, lakini tunadhani pande hizi mbili zina nafasi kubwa ya kumaliza tofauti zao na kusimama pamoja kukuza soka la Tanzania.
Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano na kutokana na hilo kuna mambo tunapaswa kushirikiana hasa kwa ustawi wa michezo.
Ukaribu huu wa ZFA na TFF ndiyo ambao huunda timu moja ya taifa ya soka kwa ajili ya mashindano makubwa yanayotambuliwa na Fifa.
Kama tulivyoeleza awali, tunarudia tena. Nipashe siyo jaji wala hakimu katika mgogoro huu wa TFF na ZFA.
Kama wapenda michezo tunaona haipo sababu kwa mamlaka hizi kuendeleza malumbano yasiyo na tija kwa ustawi wa michezo.
Badala yake, tunadhani ni wakati muafaka kwa viongozi wa pande zote kukutaka na kuainisha maeneo yote yenye maswali mengi kuliko majibu na kuyatafutia ufumbuzi wa haraka.
Lazima tufanye hivyo haraka, siyo kwa faida ya viongozi wanaolumbana, bali kwa maendeleo ya soka la Tanzania.

Habari Kubwa