Timu Ligi Kuu ziache malalamiko, zijipange

23Jan 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Timu Ligi Kuu ziache malalamiko, zijipange

LIGI Kuu Tanzania Bara ambayo kwa sasa imesimama kwa ajili ya kutoa nafasi kwa Timu ya Taifa (Taifa Stars), inayoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), inatarajia kuendelea tena ifikapo Februari 19, mwaka huu.

Ligi hiyo inayoshirikisha timu 18 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, itaendelea katika mzunguko wa 19.

Hata hivyo, kabla ya kuanza kwa mzunguko huo, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imetangaza timu za Simba na Namungo FC zitacheza kwanza viporo vyake (mechi tatu kila timu), hii ni kutaka kuona klabu zote zitakuwa zimecheza mechi sawa kabla ya mzunguko wa 19 haujaanza rasmi.

Mabingwa watetezi, Simba ya jijini Dar es Salaam na Namungo ya mkoani Lindi zimekuwa na mechi za viporo kutokana na kubanwa na majukumu na mechi za kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Kuelekea mechi hizo za viporo na mzunguko wa pili ambao umeshaanza, Nipashe inazikumbusha timu zote kufanya maandalizi mazuri kwa ajili ya kufanya vyema katika mechi zake za hatua ya lala salama.

Timu zitakazojiandaa vizuri, zitajiweka katika nafasi ya kupata matokeo chanya na kujiimarisha kwenye mbio za kuwania ubingwa wa msimu huu, huku zilizokuwa katika hatari ya kushuka nazo zitajinasua na janga hilo.

Tunaamini kila timu kupitia makocha waliowaajiri zijiimarisha kwa kusajili wachezaji wapya kwa lengo la kuongeza nguvu baada ya kubaini upungufu uliyojitokeza wakati wa mzunguko wa kwanza na kuzifanya baadhi ya timu kupoteza idadi kubwa ya michezo.

Baada ya kukamilisha kwa zoezi la usajili wa dirisha dogo, muda ulipo ni timu kuendelea kujiimarisha kwa kufanya mazoezi yatakayowaweka imara kwa ajili ya kupambana kusaka pointi tatu katika kila mechi na hatimaye kutimiza malengo waliyojiwekea.

Tunawashauri timu zote kujipanga kuhakikisha kipenga cha lala salama kitakapoanza, kila upande unafanya majukumu yake na kuepuka kutumia muda mrefu kulalamika au kulaumu na badala yake kutumia nguvu zaidi katika kusaka pointi uwanjani.

Dunia ya sasa pointi hupatikana uwanjani, hakuna mteremko, hakuna miujiza, timu iliyosajili vizuri, iliyojiandaa vyema ndio yenye nafasi ya kutwaa ubingwa ambao bado uko wazi na hata walioko mkiani, pia wana nafasi ya kuondoka huko na kujihakikishia nafasi ya kubakia kwenye ligi hiyo ya juu upande wa Tanzania Bara.

Viongozi, makocha na wachezaji kila mmoja atakapotekeleza vyema majukumu yake, tuna hakika atakuwa ameisaidia klabu yake kwa asilimia kubwa kutimiza malengo yao na kuingilia majukumu ya mwingine, ni kutaka kujiondoa wenyewe kwenye ushindani.

Lakini tunawakumbusha viongozi wa klabu zote zinazoshiriki mashindano yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Nchini (TFF), kutumia njia sahihi za kuwasilisha malalamiko na kuacha tabia ya kuzungumza katika vyombo vya habari 'kiholela' na kujikuta wakijiweka matatani.

Kwa kutumia njia sahihi zilizowekwa, viongozi wa klabu hizo watakuwa wanajiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata haki wanayoililia na kukiuka sheria kwa kujiona wao wako juu ya TFF.

Pia waamuzi watakaopewa nafasi ya kuchezesha mechi zilizosalia ambazo zitatoa bingwa wa msimu 2020/21 au kwa maana nyingine mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa, tunawakumbusha kuchezesha kwa kufuata sheria 17 za mchezo huo.

Nipashe inawakumbusha waamuzi kwa kufanya hivyo au kutekeleza vizuri majukumu yenu, itasaidia kuondoa malalamiko kutoka kwa timu husika, mashabiki na wadau wa soka na vile vile itawapandisha kwenye madaraja ya juu katika taaluma hiyo.

Tunaikumbusha pia TFF kwa kuchukua hatua kwa wale wote watakaokwenda kinyume na taratibu na isisubiri kutoa adhabu baada ya wadau kulalamika kutokana na makosa mbalimbali yaliyofanywa.

Habari Kubwa