Tozo hizi mzigo kwa wananchi

16Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tozo hizi mzigo kwa wananchi

JANA kampuni za simu zilianza kutekeleza tozo mpya iliyopitishwa kwenye Bajeti ya mwaka 2021/22 ambayo ni kukata kati ya Sh. 10 hadi 200 kwa siku kwenye kila vocha ambayo mtumiaji ataweka, na kutoza kati ya Sh. 10 hadi 10,000 kwa kila muamala wa fedha, ambao mhusika atafanya.

Kodi hii ilipewa jina la kodi ya uzalendo na ilipitishwa na Bunge ikielezwa inakwenda kusaidia nchi kupata fedha zitakazoelekezwa kwenye miradi ya barabara vijijini, elimu, afya na maji lengo ni kuboresha huduma kwa wananchi hasa waishio vijijini.

Katika siku za mwanzo za utekelezaji imekuwa ni maumivu kwa wananchi hasa kodi ya miamala kwa kuwa sasa mwananchi anakatwa tozo ya mtoa huduma, kodi ya serikali na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika kila muamala atakaoufanya.

Tozo ya kampuni inatofautiana kutoka kampuni moja hadi nyingine. Lakini kodi ya serikali nayo inatofautiana kulingana na viwango vya watumaji au wapokeaji, vivyo hivyo kwa kodi ya VAT.

Jana wananchi wengi walipata mshtuko pale walipofanya miamala kutokana na makato kuwa makubwa, lakini hofu inayoibuliwa kuwa kuna uwezakano mkubwa kutokea athari ukiwamo mfumuko wa bei hasa ikizingatiwa kwa sasa mafuta yamepanda bei lita moja ya petroli kufikia Sh. 2,405.

Mathalani, mtandao wa Tigo kwa sasa makato yanaanzia Sh. 310 kwa anayetoa kwa wakala/ATM  kati ya Sh. 1,000 hadi 1,999 na kwa anayetoa kati ya Sh. milioni 3 hadi milioni 10 anakatwa Sh. 20,000, huku anayetuma kwenda mitandao mingine anakatwa Sh.15 kwa anayetuma Sh. 100 hadi 999 wakati anayetuma kati ya Sh. milioni 3 hadi milioni 10 anakatwa Sh. 15,000.

Aidha, kutuma fedha Tigo kwenda Tigo ni Sh. 15 kwa kiwango cha Sh. 100 hadi 1,999, huku anayetuma Sh. milioni 3 hadi milioni 10 atakatwa Sh. 15,000.

Mtandao mwingine gharama zake ni ukitoa Sh. 100,000 kwa wakala unakatwa Sh. 6,100 ikiwa imepanda kutoka Sh. 3,600 wakati kwa kiwango cha juu cha milioni 3 ilikuwa Sh. 10,000 na sasa ni 20,000.

Katika moja ya mtandao mtu alitoa Sh. 60,000 kwa wakala akakatwa Sh.4,750 ikiwa ni ada ya kampuni ya simu Sh. 2,700, kodi ya serikali Sh. 2,050.

Mjadala uliopo kwenye mitandao ya kijamii kuwa gharama ya kutuma na kutoa fedha husika ni kubwa kuliko nauli ya muhusika kuja kuchukua, na wengi wanasema ni bora kupanda basi kwenda kuchukua.

Kodi hii ina lengo jema la kuboresha huduma za kijamii, lakini kuna hofu huenda ikasababisha athari nyingine ya kupungua kwa ajira kwa maana sasa wengi hawatatumia huduma za simu kutuma au kupokea fedha, bali wataanza kutumia huduma za benki.

Kwa sasa anayenunua umeme kwa simu au kulipia huduma nyingine kama za maji basi anakatwa fedha mara mbili; kwa maana nyingine utalipia Luku na wakati huo huo utalipia kodi ya majengo, jambo ambalo ni mzigo mkubwa kwa mwananchi wa kawaida.

Pia kutokana na ongezeko hilo, kuna uwezekano mkubwa wa wananchi kuanza kuficha fedha ndani au kutembea nazo nyingi, huku wengi wataanza kutumia mawakala na benki zaidi kuliko mitandao ya simu, hivyo kudumaza biashara nyingine.

Kama suala hili halitachukuliwa kwa umakini, kuna uwezekano wa kutokea athari zaidi kwa wananchi na uchumi wa kwa ujumla. Ipo haja ya kuliangalia suala hili kwa jicho la pili kwa kuzingatia kuwa miamala ya simu inatumiwa na wengi wakiwamo wa vijijini wenye kipato kidogo.

Kadhalika, itaongeza foleni barabarani, kwa kuwa wengi wataamua kupeleka fedha wenyewe na wakati huo huo watu watapoteza muda mwingi barabarani badala ya kutumia kuzalisha. Athari nyingine inayoweza kutokea ni kupungua mzunguko wa fedha.

Habari Kubwa