TPLB imulike upya adhabu kwa waamuzi

15Feb 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TPLB imulike upya adhabu kwa waamuzi

KWA mara nyingine tena Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Februari 10, mwaka huo ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi na kisha juzi kufanya uamuzi wa kuwafungia baadhi ya waamuzi.

Kamati hiyo, ilibaini katika mechi namba 190 wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Lipuli FC mwamuzi wa kati, Abubakar Mturo na mwamuzi msaidizi namba mbili, Joseph Pombe walishindwa kumudu pambano hilo.

Kubwa katika mchezo huo, waamuzi hao walishindwa kutafsiri vyema mpira uliokuwa umeibua mvutano mkubwa kuwa ni goli au si goli baada ya kipa wa Yanga, Metacha Mnata kuukandalimiza mpira upande wa ndani wa mlingoti.

Mturo na Pombe kwa pamoja walishauriana na kuamuru ipigwe kona, uamuzi ambao ulishangaza wadau na mashabiki wengi wa soka ndani na hata nje ya nchi waliokuwa wakifuatilia kupitia luninga.

Hata hivyo, kwa kuzingatia Kanuni namba 39(1) ya Ligi Kuu Kuhusu Udhibiti wa Waamuzi, Kamati hiyo ya TPLB ikawafungia Mturo na Pombe kwa kipindi cha miezi mitatu kila mmoja.

Kifungo kwa waamuzi hao wawili kimekuja ikiwa ni siku chache tangu kamati hiyo ilipomfungia kwa kipindi cha miaka mitatu mwamuzi namba mbili, Kassim Shafisha wa mechi kati ya Simba na Namungo FC.

Safisha alikumbwa na adhabu hiyo kwa kushindwa kutafsiri vema sheria 17 za soka kwa upande wa kuotea (offside) baada ya kulikubali bao la kuotea la Meddie Kagere wa Simba.

Kwa ujumla, Nipashe tunaipongeza TPLB kwa hatua ambazo imeanza kuzichukua kwa waamuzi kwani walikuwa wanalipeleka soka letu sehemu isiyoyojulikana.

Tunaamini adhabu hizo zitawaamsha waamuzi na kurudi katika mstari na hatimaye timu kushinda kwa uwezo wake uwanjani na si kwa kutegemea mbeleko ama makosa ya waamuzi.

Lakini pia tunaiomba TPLB inapotoa adhabu hizi kuzingatia kanuni zaidi na kutoangalia sura, undugu ama urafiki, kwani namna inavyotoa adhabu hizo kunazua maswali mengi.

Hii ni kutokana na waamuzi wa mechi dhidi ya Yanga na Lipuli FC, Mturo na Pombe na yule wa mchezo kati ya Simba na Namungo FC, Shafisha, makosa yao yote ni kushindwa kutafsiri sheria, lakini adhabu zikionekana kutofautiana sana.

Kitendo cha TPLB kumfungia Shafisha kwa kipindi cha miaka mitatu huku Mturo na Pombe wakifungiwa kwa miezi mitatu kila mmoja kwetu sisi Nipashe tunaona adhabu hiyo ilitolewa kimhemko zaidi.

Tunatambua suala la kubaini mchezaji kaotea ama la ni kitendo ambacho kinatokea kwa haraka zaidi na ndiyo maana wenzetu nchi zilizoendelea kisoka wameamua kuweka teknolojia ya video kumsaidia mwamuzi, VAR.

Ikumbukwe pia kuna makosa ya kiubinadamu, hivyo Nipashe tulitarajia kuona adhabu ya Shafisha ikiwa ndogo zaidi kuliko hii ya Mturo na Pombe, ambao walichukua dakika kadhaa kujadiliana uwanjani kabla ya kufikia uamuzi wa kuamuru ipigwe kona, lakini mambo yamekuwa tofauti.

Tunasema hivyo kwa sababu hata watoto wanaocheza soka mchangani hadi leo wakiitazama video ya tukio hilo la mechi ya Yanga na Lipuli wanahoji ilikuaje waamuzi hao kuamuru itengwe kona, lakini kwa bao la Kagere linahitaji umakini kubaini aliotea na kama mshika kibendera alipepesa macho ama alizembea kwenda na kasi ya mpira, ni wazi asingeweza kubaini kama aliotea.

Habari Kubwa