TRA ijisahihishe malalamiko haya

13Apr 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
TRA ijisahihishe malalamiko haya

JUZI Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), aliibua madai mazito dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kumfilisi fedha zote kwenye akaunti ya biashara, binafsi na aliyokuwa akipokelea mshahara wa bunge.

Alieleza namna alivyoandikiwa barua kwenye barua pepe binafsi na siyo ya kampuni, huku wakijua yuko gerezani na kila akipandishwa mahakamani alikosa dhamana.

Alibainisha kuwa barua ya awali ilionyesha anadaiwa kodi ya Sh. bilioni 2 na kutokana na kutojitetea kwa wakati alitozwa riba na deni kufikia Sh. bilioni 2.6.

Aidha, alieleza namna ambavyo kila aina ya biashara aliyokuwa akifungua ilikamatwa, iliharibiwa na kutozwa kodi kubwa kiasi cha kuamua kuacha kila kitu na kuhamishia uwekezaji wake katika nchi za Dubai na Afrika Kusini kama watu wengine duniani.

Madai ya Mbowe yamekuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuitaka TRA kukusanya kodi kwa kufuata taratibu badala ya kutumia ubabe na kufikilisi watu kiasi cha kesho na keshokutwa kukosa pa kwenda kukusanya.

Mbowe ni mmoja kati ya wafanyabiashara wengi waliojikuta kwenye mikono ya kikosi kazi maalum cha kukusanya kodi, ambacho kilidaiwa kutoaangalia uendelevu wa biashara husika bali kukusanya kilichopo kwa wakati huo.

Mbowe ni mmoja kati ya wengi wenye maumivu hayo na huenda kuna ambao wako gerezani, au wamekimbia nchi kama Rais Samia alivyoeleza, na sasa kwa mabadiliko na mwelekeo mpya ni muhimu sana ukafanyika utaratibu wa kujenga imani na ujasiri kwa wafanyabiashara.

Ni muhimu sana TRA ikakutana na jumuiya ya wafanyabiashara kuweka mambo sawa, kwanza kuwaaminisha na kuwapa ujasiri kuwa wanaweza kuendelea na biashara zao bila kubugudhiwa.

Kilio cha wafanyabiashana na wawekezaji kama Mbowe maumivu yake siyo kwao tu bali kwa watu wa kawaida kabisa, waliokuwa wameajiriwa ambao walilazimika kwenda nyumbani na kukaa mtaani bila kazi, na yanakwenda moja kwa moja kwa watoto na wategemezi wengine.

Mtu huyu hataweza kupata matibabu kwa sababu hana fedha na hana bima ya afya, mwanaye hatasoma shule nzuri aliyokuwa anasoma awali, na kama alikuwa amepanga hatalipa kodi ya nyumba na bili mbalimbali za maji, umeme na nyinginezo.

Hali hiyo itaondoa mzunguko wa fedha kwa watu na hali ya maisha itakuwa ngumu sana, hii yote ikiwa ni madhara ya kumkabili mfanyabiashara mkubwa na kukamua fedha zake.

Sasa wanawenda kuwekeza nje ya nchi, maana yake wanakwenda kuimarisha uchumi wa nchi husika, wanachangia pato la nchi husika na anaajiri watu wa nchi hiyo ambako watalipa kodi kupitia manunuzi na kodi ya mishahara.

Ajira hizi zingeenda kwa Watanzania, kipato hicho kingebaki nchini, na maendeleo hayo yangebaki nchini, ndiyo maana tunasema TRA ina nafasi kubwa sana ya kuwarudisha kupitia imani na kuwatengenezea mazingira rafiki.

Ni muhimu wafanyabishara hao wakaelezwa fedha zilizochukuliwa kwenye akaunti zao zimekwenda wapi, kama zililipia kodi za nyuma je, walipewa nafasi ya kupitia hayo madai kama ni kweli? Kama haikufanyika hivyo ni muhimu utaratibu ukafanyika kuhakikisha haki inapatikana.

Rais Samia kaweka bayana kuwa anataka kodi ikusanywe ila isiwe ni ya dhuluma, bali ile ya Kaisari iliyoamuriwa kwenye vitabu vitakatifu.

Tunatarajia kuona mazingira mazuri yanarejea na elimu kwa mlipamkodi inaongezeka ili kila mmoja afurahie kulipa kodi kwa kuwa ana uhakika inakwenda kutekeleza shughuli za maendeleo.

Ni muhimu yaliyoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), yanafanyiwa kazi ili kuongeza morali wa kazi na kulipa kodi, kwa kuwa wananchi wanaposikia mtu amechota mabilioni na bado ameachwa akitamba mtaani, basi kila mtu ataona ni sawa kufanya hivyo, na matokeo yake ujanja ujanja utaongezeka na kuua motisha ya watu kulipa kodi kwa hiyari na kwa wakati mwafaka.

Habari Kubwa