Tuchangamkie fursa Kiswahili nje ya nchi

07Jun 2019
Mhariri
Nipashe
Tuchangamkie fursa Kiswahili nje ya nchi

LUGHA ya Kiswahili ni fursa, ambayo Watanzania hawajaichangamkia ipasavyo kama inavyostahili.

Tunasema hivyo kwa kuwa mahitaji yake yanazidi kuongezeka kila uchao katika nchi za bara la Afrika hususan Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.

Kukua na kupanuka kwa lugha ya Kiswahili na kusababisha mahitaji ya wataalamu wa kuifundisha, kumezifanya nchi kadhaa kuchangamkia fursa hiyo kwa kuandaa kuzalisha wataalamu wake kwenda kufundisha nje ya nchi zao.

Kuna mifano kadhaa inayoonyesha hivyo. Kwa mfano, baadhi ya nchi za Afrika Mashariki licha ya kutotumia lugha hiyo kama lugha rasmi, lakini raia wake wengi wanajipenyeza katika nchi nyingine zinazowahitaji wataalamu wa kuifundisha.

Kimsingi, Tanzania ambako Kiswahili kinazungumzwa na wananchi wote na ni lugha rasmi, raia wake hawajaichangamkia fursa ya kwenda kufundisha lugha hiyo ng’ambo ambako mahitaji ni makubwa.

Kuna vyuo vikuu na taasisi nyingi za elimu katika nchi kadhaa kama Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na nchi za kusini mwa Afrika kama Afrika Kusini, Zimbabwe, Namibia, Zambia, Malawi, Botswana na nyingine, ambazo wataalamu wetu wangechangamkia kwenda kufundisha Kiswahili.

Licha ya kuchelewa kuchangamkia fursa hiyo, lakini muda bado upo na ni sasa kutokana na mahitaji makubwa, hivyo tunashauri zichukuliwe hatua mbalimbali za kuwezesha watu wetu kuziomba nafasi hizo kwa kuwa zina manufaa mengi kwao binafsi na taifa, yakiwamo ajira na pato lao kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu.

Limekuwa jambo zuri kutokana na Rais John Magufuli kufungua njia hiyo kwa kuonyesha mfano alipofanya ziara rasmi ya kikazi katika nchi za Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe hivi karibuni.

Rais Magufuli aliwakabidhi viongozi wakuu wa mataifa hayo vitabu kadhaa vya lugha ya Kiswahili pamoja na kamusi. Hatua hiyo ya Rais ni kuitangaza lugha ya Kiswahili nje ili iwe sehemu ya fursa za kulinufaisha taifa letu.

Tunampongeza sana na tunawashauri viongozi wengine, wawakilishi wetu nje na Watanzania kwa ujumla kukitangaza Kiswahili wanapokuwa ughaibuni kwa lengo la kuwafanya watu wa nje kuelewa kuwa wanaweza kuwapata wataalamu wa lugha hiyo kutoka Tanzania.

Jitihada nyingine za kutia moyo katika kuchangamkia fursa za nje,  Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limetaja mikakati yake ya kuandaa wasomi wa kufundisha lugha hiyo nje, ikiwamo kuandaa kanzidata ya wanataaluma wote wa Kiswahili nchini na kuwapa mafunzo maalum.

Akizungumza na gazeti hili juzi msemaji wa Baraza hilo, Consolata Mushi alisema kanzidata hiyo itasaidia kuwatambua wanataaluma wote wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo nje ya nchi ili kuwaweka tayari kwa fursa hizo.

Kwa mujibu wa Bakita, awali zilikuwa zikija fursa moja moja, hivyo sasa wanaandaa kanzidata ya kuwatambua wanataaluma wote wa Kiswahili, ili iwe rahisi zinapokuja fursa pawapo na utaratibu mzuri.

Mkakati wa Bakita kuandaa wataalamu ni mzuri, isipokuwa uende sambamba na jitihada nyingine za ziada, ikiwamo kushirikiana na kufanyakazi pamoja na vyuo vikuu nchini ambavyo vinafundisha lugha ya Kiswahili na vina taasisi za kuendelea lugha hiyo kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Pia njia nyingine ni Bakita na vyuo vyetu vikuu kwenda katika vyuo vya nje kufanya ushawishi ili viwape fursa za ajira wataalamu kutoka nchini.

Habari Kubwa