Tuendelee kuchukua hatua dhidi ya mvua

16Jan 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tuendelee kuchukua hatua dhidi ya mvua

MVUA zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini, zimeendelea kusababisha athari kwa wakazi wa maeneo husika.

Mvua hizo zilizoanza Septemba mwaka jana, zimekuwa zikiharibu miundombinu ya barabara na madaraja pamoja na majengo, vifo na kuwakosesha watu makazi kutokana na maji kuzingira nyumba na kuzibomoa.

Mvua ni neema na zinahitajika, lakini pale zinaponyesha na kusababisha madhara kwa binadamu inakuwa kinyume cha matarajio yake, kwa sababu matarajio ni kusaidia shughuli za uzalishaji wa chakula na mahitaji mengine ya maji yakiwamo matumizi ya nyumbani na katika taasisi.

Hatutataja matukio yote yaliyosababishwa na athari za mvua hizo, lakini matukio ya karibuni ni mvua kubwa ya mafuriko wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro, ambayo ilisababisha maelfu ya watu kupoteza makazi, hivyo kwenda kuishi kwa ndugu, jamaa, majirani na marafiki. Mvua hiyo pia ilisomba makaburi takribani 14.

Wakazi kadhaa wa Wilaya ya Mvomero waliopoteza makazi wanaendelea kujihifadhi kwa ndugu, jamaa, marafiki na majirani, huku wakiomba kupatiwa makazi ya muda pamoja na misaada ya kibinadamu kutoka serikalini, wadau na wasamaria wema.

Katika tukio lingine, zaidi ya watu 1,000 wameripotiwa kukosa makazi, baada ya nyumba 237 kubomolewa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Dodoma.

Wakazi walioathirika kutokana na mvua hizo usiku za kuamkia juzi ni wa Wilaya ya Bahi, huku miundombinu ya barabara ikiharibiwa.

Hayo yalibainishwa juzi na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mwanahamisi Munkunda, alipokuwa akizungumza, baada ya ziara ya kukagua maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, huku akiwataka wazazi kuhakikisha watoto wanacheza kwenye maeneo salama badala ya kuogelea kwenye mito na madimbwi yaliyojaa maji.

Alisema kuna mito mingi ya maji kutoka mikoa jirani na wilaya inayoishia katika Wilaya ya Bahi, hivyo wananchi wachukue tahadhari kutokana na maji kuingia kwenye makazi ya watu.

Kimsingi, athari za mvua zinazoendelea kunyesha zinaweza kuwa kubwa kama wananchi hawatachukua hatua kama mamlaka hususan Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) zinavyosisitiza wananchi kuchukua hatua.

Mamlaka hiyo imeshatabiri kuwa mvua zitaendelea kunyesha hadi Aprili, hivyo kutoa angalizo kwa wananchi kuchukua tahadhari, hivyo kwa upande watu tunapenda kusisitiza wananchi wasipuuze kuchukua tahadhari.

Tahadhari kubwa ni kuwa wanaoishi maeneo hatarishi kama ya mabondeni na mapitio yote ya maji waondoke kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kupata madhara yatokanayo na mafuriko.

Ikumbukwe kuwa moja ya athari za mabadiliko ya tabianchi ni mvua ambazo hazifuati msimu, na zinaponyesha zinakuwa na athari nyingi ikiwamo mafuriko na upepo.

Athari hizi za mabadiliko ya tabianchi zinayakumba na kuyaathiri maeneo mengi duniani, hivyo Tanzania hatuwezi kuwa kisiwa badala yake tuchukue tahadhari.

Tukumbuke kuwa serikali haina uwezo wa kuwasaidia watu wote wanaopata athari ya mvua hususan wale ambao wamekuwa wakikaidi maelekezo ya kuyahama maeneo hatarishi kwa muda mrefu.

Ni matumaini yetu kuwa wananchi watachukua hatua kutokana na taarifa pamoja na ushauri unaotolewa mara kwa mara na mamlaka husika.

Habari Kubwa