Tuepuke simu barabarani kupunguza ajali sikukuu

18Dec 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tuepuke simu barabarani kupunguza ajali sikukuu

HUU ni msimu wa sikukuu ambao kama taifa tunalazimika kuchukua tahadhari zote kuwaepusha wananchi na ajali zinazosababisha vifo, uharibifu wa mali na njia za usafiri.

Katika moja ya taarifa kubwa zilizochapishwa na gazeti hili Jumatatu wiki hii ni tahadhari kwa serikali na wadau wa usalama barabarani kuendelea kuchelewesha sheria ya matumizi ya simu barabarani.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA) idadi ya wanaotumia simu nchini ni takribani milioni 40 na pengine kati ya wote hao madereva huenda wanatumia simu. Idadi hiyo ni kubwa mno na bila udhibiti wa kisheria kuna uwezekano wa idadi kubwa ya watu kuangamizwa kutokana na matumizi ya simu barabarani.

TCRA inaeleza kuwa matumizi ya simu yanateka akili za watumiaji kiasi cha kuvuka barabara, huku wakiendelea kusikiliza au kusoma ujumbe na wengine wameweka visikilizio masikioni.

Matokeo yake ni kupata ajali zinazosababishwa na gari au pikipiki na wengine kupoteza maisha. Ndiyo maana sheria ya kudhibiti matumizi ya simu barabarani inahitajika haraka kwa lengo la kudhibiti, madereva, abiria na wanaotembea.

Kutokana na kutojali usalama na maisha imekuwa kawaida dereva wa basi anaendesha watu zaidi ya 50 kuongea na simu akiwa barabarani, kadhalika wa bodaboda na magari madogo naye hufanya hivyo.

Matokeo yake ni kusababisha ajali, ndiyo maana sheria ya udhibiti matumizi ya simu barabarani sasa ni lazima. Kwa mataifa mengine kuna sheria za kutumia simu aidha kwa kuweka gari pembeni au kutoka nje ya gari na wakati mwingine kutumia kifaa kingine badala ya kuweka simu masikioni ambacho kwa kuendesha kwenye kiwango kidogo cha mwendo dereva anaweza kuzungumza.

Licha ya kwamba polisi wanasisitiza kuwa sheria iko mbioni na wamependekeza adhabu iwe Sh. 500,000 ikiwa dereva atakutwa anaendesha huku anatumia simu, ukweli ni kwamba Tanzania imechelewa kuandaa sheria hiyo.

Ni muhimu kuwa na sheria kali kwa kuwa matumizi ya simu hizo yamekuwa ni changamoto kubwa kwa kila mmoja hata wakati mwingine mlezi au mzazi anavuka barabara pamoja na watoto au mtoto lakini ameshikilia simu sikioni.

Si hivyo tu, wakati mwingine imetokea kuwa na misururu mirefu barabarani kutokana na watu kuchati na simu lakini wameweka visikilizio masikioni kiasi cha kuzuia kusikia hata honi au kelele nyingine zinazoendelea barabarani.

Tunapenda kuwakumbusha wadau kuwa msimu huu wa sikukuu ni hatari zaidi wakiwa barabarani na simu masikioni.

Ni kwa sababu wapo wanaoendesha huku wanasikiliza muziki au kutizama picha, wapo wengine wanaoandika ujumbe, kupiga simu au kusaka namba za mawasiliano ndani ya vifaa hivyo.

Yote hayo ni hatari tena si kwao tu bali kwa wengine wakiwamo watembeao, wanaotumia vyombo vya moto, wenye ulemavu na watoto ambao huwa sehemu ya ajali hizo.

Kwa hiyo msimu huu wa sikukuu za Noeli na Mwaka Mpya ni wakati wa kukumbushana kwa kuweka ujumbe wa mabango barabarani wa kuwahimiza madereva kupunguza mwendo na kuachana na simu.

Tunaona kuwa ni vyema kuanza kukumbusha sasa kwa kuweka ujumbe huo kwenye mabango kwenye njia zote na pia kuwahimiza wanaotumia pikipiki kutumia kofia ngumu ili kuokoa maisha pale ajali zinapotokea.

Wakati mwingine ni vyema kuweka namba za polisi na TCRA ili abiria waripoti taarifa za uendeshaji mbaya unaoambatana na matumizi ya simu wakati mtu yuko kwenye usukani.

Kinga ni bora kuliko tiba. Tuanze sasa kukumbushana ili kuokoa maisha na kuepusha ajali.

Habari Kubwa