Tuepuke ubabaishaji huu kwenye michezo

13Aug 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tuepuke ubabaishaji huu kwenye michezo

WIKI hii kulikuwa na taarifa kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuhusiana na tishio la Klabu ya Yanga kushushwa daraja kutokana na kushindwa kuwasilisha Shirikisho la Soka Ulimwenguni - Fifa majina ya wachezaji watakaowatumia kwa ajili ya michuano ya Ligi Kuu.

Tishio hilo halikuwa kwa klabu hiyo ya Jangwani peke yake, bali pia klabu ya Coastal Union ya Tanga, ambayo nayo ilishindwa kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa Fifa, klabu za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza (DFL) na Daraja la Pili (SDL), zilipaswa hadi kufikia Agosti 6 mwaka huu ziwe zimekamilisha kuwasilisha majina ya wachezaji wao.

Majina hayo yalipaswa kuwasilishwa kupitia mfumo wa kisasa wa kielektroniki wa uhamisho wa wachezaji wa ndani (DTMS).

Kushindwa kwa klabu hizo kuwasilisha Fifa majina ya wachezaji kwa muda uliopaswa ni kielelezo cha kushindwa kuwajibika kulingana na mahitaji ya muda.

Klabu hizi zilikuwa na muda mwingi wa kufanya hivyo, lakini kutokana na utumwa wa kufanya kazi kibabaishaji, ndiyo kiini cha klabu hizo kukabiliwa na adhabu ya kushushwa daraja au kutozwa faini.

Tunashindwa kuelewa klabu kubwa kama Yanga, yenye mfumo wa uongozi makini wanaweza kusubiri hadi siku ya mwisho kufanya hivyo tena kwa kukumbushwa?

Klabu kubwa kama Yanga, ilipaswa mapema kuwasilisha majina yake sehemu husika ili kuepuka uwezekano wa adhabu au kushushwa daraja.

Kwa kushindwa kwenda na muda, sasa klabu hiyo ya Jangwani na Coastal Union zinasubiri majaliwa ya Fifa ili kunusuriki na adhabu wanayoweza kupewa.

Kama wadau wa michezo, tungependa kuchukua nafasi hii kuwakumbusha viongozi wetu wa klabu za soka kujiondoa kwenye utumwa wa kufanya kazi kwa mazoea.

Dunia ya sasa iliyojaa kila aina ya changamoto, inahitaji viongozi wenye dhamira ya kweli ya uwajibikaji na siyo kinyume chake.

Utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea kama ilivyoonekana kwa viongozi wa Yanga, ambao utetezi wao hakuwa na mashiko haupaswi kuwa sehemu ya familia ya wapenda soka nchini.

Nipashe tunaamini kuwa, soka letu linaweza kusonga mbele pale tu tutakapoamua kwenda sambamba na kasi ya wenzetu, ambao wanaendelea kuwa mifano ya mafanikio kila kukicha.

Haipo sababu ya kuendelea na viongozi wenye taswira dhaifu na waliokosa ubunifu katika ustawi wa michezo nchini.
Mwisho, tungependa kuzipongeza klabu zote zilizokamilisha kuwasilisha majina ya wachezaji wao kwa wakati.

Tunaamini zile zilizoshindwa kufanya hivyo msimu huu, zitajifunza kutoka kwa wenzao waliokwenda na muda na kukamilisha kazi ya kuwasilisha majina.

Habari Kubwa