Tufanye utafiti zaidi kukielewa kiharusi

31Oct 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tufanye utafiti zaidi kukielewa kiharusi

TAARIFA kuwa idadi ya watu wanaofariki dunia kutokana na kiharusi nchini ni kubwa ni habari ambazo licha ya kusikitisha zinaogopesha pia.

Zinaogopesha kwa kuwa zinawagusa Watanzania wote baada ya wataalamu kueleza kuwa matatizo ya kiharusi yanawaathiri watu wa rika zote na si wazee kama ilivyokuwa imezoeleka hapo awali.

Licha ya kuhofisha na kusikitika ni vyema pia kuanza uwajibikaji zaidi katika kuwahamasisha wananchi kuanzia watoto shuleni, vyuoni na umma kwenye jamii zetu ili waamke na kuchukua hatia dhidi ya maradhi haya.

Tatizo tulilonalo Watanzania ni kuamini kuwa kiharusi ni tatizo la kurogwa , licha ya kwamba wasomi wanatueleza kuwa ni ukosefu wa hewa safi na chakula ubongoni kwa sekunde chache.

Chakula na hewa hiyo hufikishwa na damu licha ya kwamba kitaalamu damu haiugusi ubongo, moja kwa moja, lakini kuna utaratibu wa kufikisha virutubisho hivyo.

Kwa maana nyingine ni kwamba mfumo unaopeleka chakula na hewa na virutubisho unapochelewa kuhudumia ubongo tatizo hutokea.

Wataalamu wa masuala ya mishipa ya fahamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, wanaeleza wakati wa Siku ya Kiharusi Duniani (Oktoba 29), kuwa ni ugonjwa wa pili kwa kuua watu duniani.

Aidha, wanautaja kuwa ni chanzo cha ulemavu kwa Watanzania wengi ambao mara nyingi wanafika Muhimbili wakiwa wamechelewa.

Inawezekana wanachelewa kwa vile wengi hukimbilia kwa waganga wakiamini kuwa wamerogwa.

Taarifa hizi za madaktari bingwa zinaturudisha kule kule kwenye utamaduni wa Watanzania wa kuchelewa kuripoti hospitalini tatizo lolote kuanzia degedege na hata kina mama kujifungua.

Ni kawaida kwa watu wengi kupuuza kwenda hospitalini kutokana na kuamini zaidi ushirikina na kukimbilia kwenye tunguri na kupigwa chale.

Wapo watu wanaoamini kuwa ugonjwa wa kiharusi ni wa kulogwa na huitwa ‘kipapai’ na kwa msingi huo hukimbilia kwa waganga ambako nako hawaponi, wakizidiwa ndipo hukimbilia hospitalini.

Hali inatisha kwa vile wataalamu wanaeleza kuwa wastani wa wagonjwa watatu hadi watano hupokelewa kila siku hospitalini hapo ambao licha ya kufika wengi wanachelewa na kama wangewahi wangepona kwani ukifika hospitalini saa sita baada ya kuugua ugonjwa unatibika.

Taarifa za kitisho cha ugonjwa huo ni vyema zianze kufanyiwa kazi kwa kutumia utafiti na uchunguzi zaidi ili watu wafahamu chanzo cha maradhi hayo kwa ufasaha.

Tungependa kupata maelezo na taarifa zaidi kwanini ugonjwa huo umezidi zama hizi na ni vipi vichocheo vyake? Je kuna uhusiano na matatizo mengine kama ya moyo, shinikizo la damu, uvimbe kwenye ubongo na magonjwa yakiwamo kisukari. Na zipi ni njia za kujikinga?

Watu wanaweza kujichunguza kwa namna gani kufahamu kuwa wana tatizo hilo? Kwa watu wa kawaida wanaoishi vijijini wanaweza kuchukua tahadhari zipi kujiepusha na tatizo hilo?

Tunapenda kupata taarifa zaidi kwa vile kuna maelezo ya jumla yanayotolewa na wataalamu kuwa matatizo ya moyo na kiharusi ni matokeo ya mitindo ya maisha watu wanayoishi.

Maelezo yao ni kwamba watu wengi hawafanyi mazoezi, hutumia kwa wingi vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi mno, ni wanene kupindukia na pia hawachunguzi afya zao.

Wakati mwingine tunaona kuwa maelezo hayo si ya kuridhisha kwa vile kuna watu wembamba, wanaofanyakazi sana wanaoishi vijijini ambao hawana miili mikubwa waliopoteza maisha kutona na kiharusi.

Ndiyo maana tunasisitiza kuwa ukifanyika utafiti zaidi na kuzifahamu njia za kukabiliana na tatizo hilo utakuwa mwanzo wa kupata ufumbuzi na kuepusha madhara ya kiharusi.

Habari Kubwa