Tuichangamkie fursa ya gesi iliyogundulika

30Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tuichangamkie fursa ya gesi iliyogundulika

KUNA taarifa njema na za kutia matumaini kwa Watanzania, kwamba kiasi kikubwa cha gesi aina ya Helium imegundulika nchini.

Taarifa hiyo imetolewa na watafiti kutoka Uingereza na Norway kwamba gesi hiyo inatumika kwenye mashine za uchunguzi wa binadamu za MRI, nyukilia na sekta nyingine ya teknolojia, nishati ambayo ilikuwa hatarini kutoweka duniani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Japan juzi kwa vyombo vya habari na wataalamu hao na kuandikwa kwenye magazeti mbalimbali ya kimataifa, kiasi hicho cha gesi iliyopatikana kwenye bonde la ufa, ni kikubwa zaidi kuliko kiasi kingine kilichopo maeneo tofauti duniani.

Watafiti waliogundua gesi hiyo ni kutoka vyuo vikuu vya Oxford na Durham vya Uingereza kwa kushirikiana na Kampuni ya Helium One ya Norway, ambayo ina kibali cha kufanya utafiti wa uwapo wa nishati hiyo nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wataalamu hao wamefanya hesabu na kuthibitisha kwamba katika eneo moja la bonde la ufa kuna gesi kiasi cha futi za ujazo bilioni 54 (Billion Cubic Feet - BCF) ambazo ni sawasawa na mita za ujazo bilioni 1.5, kiasi hiki pekee kinatosha kuzijaza mashine za matibabu za MRI milioni 1.2.

Mmoja wa watafiti hao alisema kwa mwaka, duniani kuna uhitaji wa gesi ya helium kiasi cha futi za ujazo bilioni nane, (mita za ujazo milioni 226) na kwamba Marekani ambayo ndiyo yenye hifadhi kubwa ya gesi hiyo duniani, kwa sasa ina kiasi cha futi za ujazo bilioni 24.2 sawa na mita za ujazo milioni 685.

Ingawa Serikali haikuwa tayari kutoa ufafanuzi kuhusiana na suala hilo zaidi ya kuthibitisha kuwa kampuni hiyo inafanya utafiti nchini, lakini hatua hiyo inaleta matumaini kwamba nchi yetu imepata rasilimali muhimu ambayo inaweza kuisaidia kupaa kiuchumi.

Kinachofurahisha ni kuwa taarifa hizo zimetolewa wakati Serikali ikijipanga kuipelaka Tanzania katika uchumi wa kati kupitia kwenye viwanda, hivyo tunaamini kuwa mamlaka husika zitafuatilia haraka taarifa hizo na kuzifanyia kazi.

Kama Serikali imepania Tanzania iwe ni nchi ya viwanda, zinahitajika jitihada za kuhakikisha kwamba rasilimali zilizopo na zinazogungulika kama gesi hiyo zinatumika ipasavyo kubadilisha maisha ya wananchi na na kupaisha uchumi wa nchi.

Tunasema hivyo kwa kuwa licha ya Tanzania kuwa na rasilimali nyingi na za pekee kama madini ya Tanzanite, mbuga za wanyama, misitu na nyingine, lakini hazijasaidia kubadili maisha ya wananchi.

Kuna nchi ambazo zina rasilimali kidogo, lakini kutokana na umakini wao zimezitumia vizuri na kusaidia kuboresha maisha ya wananchi wake na kuzipaisha kiuchumi.

Ni matarajio yetu kwamba Serikali itapeleka wataalamu wake kujiridhisha na kiasi cha gesi iliyogundulika kama alivyosema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk. James Mataragio sambamba na kauli ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhomgo kuitaka kampuni hiyo kuchimba na kueleza ni kiasi cha gesi iliyoko.

Kama tulifanya makosa huko nyuma kwa kutokutumia vizuri rasilimali ambazo nchi yetu imejariwa kuwa nazo, sasa na ni wakati wa kujisahihisha na kuichangamkia fursa ya fursa ya gesi iliyogundulika ili isaidie kuboresha maisha ya wananchi na na uchumi wa nchi yetu.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa