Tujifunze kuhifadhi chakula wakati wa shida

11Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tujifunze kuhifadhi chakula wakati wa shida

BEI ya mahindi katika masoko mbalimbali mikoa ya Kanda ya Kaskazini (Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara) imepanda kutoka Sh. 55,000 hadi 127,000 gunia la kilo 100.

Pia zao hilo linadaiwa kuadimika katika baadhi ya maeneo na kuomba chakula cha msaada hasa kwa wananchi wa maeneo ya Longido.

Bei zilianza kupanda tangu mwezi Desemba mwaka jana, na sababu kubwa ikielezwa kutokana na kupungua kwa mvua, jambo lililosababisha mavuno kuwa hafifu tofauti na matarajio.

Kupanda kwa nafaka hiyo kumesababisha unga kupanda kutoka Sh. 1,000 kwa kilo moja hadi 1,200 hali inayopandisha hali ya maisha kwa wengi ambao hutegemea kama chakula kikuu.

Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa mvua ilikuwa chache na kuchelewa kiasi cha mahindi na mazao mengine kukauka kabla ya wakati, au kushindwa kustawi kiasi cha kutotoa mazao.

Hali hiyo imeathiri nchi nyingi duniani kiasi cha Kenya kutangaza ukame kama janga la kitaifa kwa kuwa binadamu, wanyama na viumbe wengine wamekufa kutokana na kukosa maji na chakula.

Chakula husafirishwa kwenda Kenya, lakini hupelekwa pia Somalia na Ethiopia ambazo sehemu kubwa ya nchi inakabiliwa na ukame na kutegemea chakula kutoka nchini.

Hakuna ubishi kuwa maeneo mengi ya Tanzania yana ardhi yenye rutuba ifaayo kwa kilimo na hulisha nchi nyingi ikiwamo Kenya na ndiyo maana vyakula vingi husafirishwa kwenda huko.

Hali ya ukame imekuwa tishio maeneo mengi kwa sasa, pia mvua hazitabiriki kiasi cha wakulima kushindwa kujua ni wakati gani walime na aina ya mazao, hapa ndipo unakuja umuhimu wa kusisitiza kilimo cha mazao yanayostahimili ukame ambayo yatafaa kwa chakula.

Wafanyabiashara hunusa harufu ya faida kwa haraka na kwa kuwa tupo kwenye soko huria basi wanaruhusiwa kuuza na kununua wanapotaka ikiwamo nje ya nchi na ndicho kilichofanyika.

Wapo wanaouza mahindi mabichi ambayo huchemshwa au kuchomwa, na wengine husubiri na kuuza mahindi makavu ambayo hutumiwa kwenye ugali, uji na vyakula vingine muhimu kwa binadamu na wanyama.

Kwa sasa mahindi kuadimika maana yake yamefichwa kusubiri bei kupanda au yamesafirishwa kwa wingi kwenda nje ya nchi, na sasa inatakiwa kuchukua hatua madhubuti.

Tunaamini akiba ya chakula iliyopo Ghala la Taifa la Chakula (NRFA), itatumika kusaidia wananchi wenye uhitaji kwa sasa kununua kwa bei nafuu, ikiwa ni pamoja na Waziri wa Kilimo kufuatilia kwa karibu ikiwa ni pamoja na kitengo cha maafa kuanza kutambua wenye uhitaji na kupeleka msaada.

Ni muhimu kuelimisha wakulima kuwa wasiuze mazao mabichi bali waone umuhimu wa kuuza baada ya kukomaa, lakini kuhimiza kilimo cha umwagiliaji kwa kuhifadhi maji ya mvua ili kukabili hali ngumu wakati wa ukame.

Pia ni muhimu kuangalia uwezekano wa kutosheleza soko la ndani kabla ya kuruhusu mazao hayo kusafirishwa nje, kwa kuwa tangu mipaka ifunguliwe watu wameendelea kusafirisha nje na kusahau kuacha akiba ndani.

Aidha, tunajua ni wakati wa soko huria lakini bado tuna wajibu wa kuhakikisha hatuuzi chakula chote na kukosa akiba.

Habari Kubwa