Tujihadhari corona, lakini tuchape kazi

24Mar 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tujihadhari corona, lakini tuchape kazi

UGONJWA wa corona, umesambaa kwenye zaidi ya maeneo ya utawala au nchi 187 kati yake 34 ni za Afrika, ikiwa ni watu 294,110 wameambukizwa na kati yake 12,944 wamefariki.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), nchi inayoongoza kwa maambukizi na vifo ni China ikiwa na watu 81,499 huku nje ya China inayoongoza ikiwa ni Italia yenye maambukizi 53,578.

Kila nchi imetangaza hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na ugonjwa huo, huku baadhi zikifunga kila kitu na raia wake hawaruhusiwi kutoka nje na iwapo watakamatwa wanachukuliwa hatua kali. Baadhi zimefungulia wafungwa wote magerezani.

Juzi Rais John Magufuli, alihutubia taifa na kueleza kuwa kuna watu 12 wamegundulika, na hatua zilizochukuliwa ni kwa wote wanaoingia nchini kutoka nchi zenye maambukizi ya corona watawekwa kwenye uangalizi wa siku 14 kwa gharama zao.

Aidha, aliwasihi Watanzania kuendelea na shughuli za uzalishaji, huku wakichukua tahadhari zote muhimu, ikiwa ni siku chache baada ya kutangaza kufunga shule, vyuo na michezo mbalimbali.

Alisema waendelee kuchapa kazi kwa bidii ili kuijenga nchi, na kwamba ugonjwa huo usiwe kigezo au sababu ya kuacha kufanya kazi kwa bidii badala yake iwe hamasa zaidi ya kuchapa kazi.

Tunakubaliana na alichokielekeza Rais kwa kuwa lazima maisha yaendelee, kwa kuwa hata nchi zenye maambukizi ambazo zina uchumi mkubwa kama Italia na Ufaransa shughuli za viwanda zinaendelea kwa tahadhari kubwa, kwa kuwa wanajua wakifunga kila kitu ni sawa na kusimamisha nchi.

Kama nchi kubwa duniani kama hizo zimechukua tahadhari za kuzuia watu kutotoka nje, lakini kazi zinaendelea kwa njia ya mtandao na uzalishaji unafanyika, maana yake ni kuwa licha ya janga lililopo ni lazima uzalishaji uendelee kwa ustawi wa watu wake.

Hivyo, kuendelea na kazi kwa tahadhari kubwa ni suala la kutiliwa maanani, ingawa kwa hali ya umaskini wa nchi zetu, ukosefu wa huduma za mtandaoni ni vigumu sana kwa kazi zote kufanyika kutoka nyumbani.

Wenzetu wameweza kutangaza hivyo kwa kuwa wana uhakika wa miundombinu, watu wake wana utayari wa kufanyakazi na watafanya kwa uaminifu tofauti na nchini ambako mtu anategemea vifaa vya kazi vya ofisi na huduma ya intaneti.

Kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania ni wachache wana akiba ya kutosha ya chakula na fedha, wengi ni wale wanaotoka kutafuta mkate wa siku kwamba wakishindwa kutoka basi watashinda njaa. Kwa kuzingatia mazingira hayo, ndiyo maana lazima shughuli za uzalishaji ziendelee, lakini kwa tahadhari kubwa ili maambukizi yasiendelee kusambaa.

Hakuna ubishi kuwa iwapo serikali itatangaza kufunga maeneo yote na watu kuzuiwa kutoka, nchi itasimama. Siyo kila maamuzi yanayofanywa na mataifa mengine kuigwa na nchi yetu, lazima kila uamuzi uzingatie mazingira ya nchi husika.

Sisi tunasema ni vyema kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa fya na kuchukua tahadhari bila kupaniki, huku tukiendelea kutafuta mkate wa siku kama kawaida, na si kukimbilia kufunga biashara au kusimamisha uzalishaji.

Sisi kama taifa, hatuna baba wala mjomba wa kutusaidia bure, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuendelea kufanya kazi za kujenga taifa, huku tukichukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya corona.

Mathalani, zipo nchi zimetangaza kusimamisha riba za mikopo, kodi za nyumba na watu wanalipwa mishahara wakiwa nyumbani, kwa serikali yao kutenga fungu la fedha kwa ajili hiyo. Hata hivyo, kwa nchi yetu na nyingine zinazoendelea hali ya uchumi haituruhusu kufanya hivyo.