Tujipange kutekeleza bajeti ya mwaka huu

01Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tujipange kutekeleza bajeti ya mwaka huu

UTEKELEZAJI wa bajeti ya Serikali kwa mwaka huu wa fedha 2016/17 unaanza leo. Utekelezaji huo utasababisha bei na gharama za baadhi ya bidhaa na huduma kupanda.

Katika bajeti hiyo iliyowasilishwa katika Bunge na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Juni 8 mwaka huu, Serikali ilipendekeza mambo kadhaa ambayo yatasababisha gharama na bei hizo kupanda. Kikubwa zaidi ni kwamba bajeti hiyo imeweka kodi zaidi katika bidhaa na huduma.

Kutokana na wingi wa kodi ambazo Serikali ilipendekeza na baadaye Bunge kuridhia, wananchi watalazika kuingia zaidi mfukoni kulipa kodi mpya zilizoanzishwa na kugharamia huduma ama kununua bidhaa ambazo bei zake zitaenda juu kutokana na ongezeko la kodi.

Serikali itatoza tozo ya asilimia 10 ya gharama za miamala ya simu. Ingawa kampuni za simu hazikutoa tamko lolote la kukusudia kuongeza gharama, lakini kama zitafanywa hivyo, ni dhahiri watumiaji wa kodi wataumia. Kuna ongezeko la kodi pia katika vinywaji vyote, hivyo Watanzania wengi watalazimika kutumia fedha zaidi.

Benki nyingi za biashara jana zilitoa matangazo zikionyesha kuwa kuanzia leo zitapandisha gharama za kuhifadhi fedha na miamala kwa asilimia 18, hivyo kuanzia leo watumiaji wa benki wataanza kutozwa gharama hizo.

Serikali pia leo itaanza kutoza kodi zaidi za kusajili pikipiki na magari pamoja na uingizaji wa mitumba kutoka nje. Nyingine ni mafuta ya kula kutoka nje pamoja na kuanza kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) katika huduma za utalii.

Serikali ina haki ya kutoza kodi hizo kwa ajili ya kupata fedha za kujiendesha pamoja na za kutoa huduma muhimu kwa jamii kama afya, elimu, maji, barabara na nyingine zinazowagusa wananchi moja kwa moja. Hata hivyo, matarajia ya wananchi ni Serikali inapaswa kuboresha huduma kwa wananchi kwa kuwa kwa kulipa kodi watakuwa wametimiza wajibu wao na Serikali itakuwa imetekeleza wajibu wake kwa kutoa huduma bora kwa walipakodi wake.

Miaka michache iliyopita Bunge lilikuwa likiidhinisha fedha kwa wizara zote kwa ajili ya matumizi na maendeleo, lakini jambo la kushangaza na kusikitisha ni kwamba ni asilimia ndogo ilipelekwa kutekeleza miradi ya maendeleo na Serikali haikutoa sababu za kuridhisha zilizosababisha hali hiyo zaidi ya kisingizio cha uhaba wa fedha.

Kinachoonekana ni kwamba fedha hizo hazikupelekwa kwenye maendeleo kutokana Serikali wakati ule kutokuwa makini katika ukusanyaji wa mapato pamoja na nidhamu katika matumizi.

Hata hivyo, mipango Serikali ya Awamu ya Tano katika bajeti ya mwaka huu pamoja na ahadi za Rais John Magufuli inatoa matumaini kuwa pamoja na ongezeko la kodi sambamba na kodi mpya, Serikali itapeleka fedha za kutosha katika shughuli za maendeleo.

Matumaini hayo pia yanatokana na bajeti hiyo kuonyesha kwamba asilimia 40 ya fedha za bajeti za mwaka huu itapelekwa kwenye miradi ya maendeleo ikiwamo kununulia ndege mpya za serikali, meli mpya Ziwa Victoria, ujenzi wa reli ya kisasa na mambo mengine.

Gharama za maisha zitapanda, lakini jambo la msingi ni kila mmoja kujipanga kwa nafasi yake na la msingi ni kujituma na kufanya kazi kwa bidii.

Tunaishauri Serikali kwa upande wake ihakikishe inakusanya mapato na kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi, kubana matumizi na kuelekeza fedha zaidi katika miradi ya maendeleo. Ni matumaini yetu kuwa hakuna watoa huduma watakaopandisha bei za bidhaa na huduma kiholela kwa kisingizio cha kupanda kwa gharama za maisha.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa