Tumsikie Rais kwa kuwatunza wasichana

09Oct 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tumsikie Rais kwa kuwatunza wasichana

ASANTE Rais John Magufuli, kwa kumtetea binti wa Tanzania ambaye amesikia ukiwakanya wanaowapa mimba wanafunzi na wazazi na walezi wanaowaoza watoto kuacha uovu huo.

Angalizo la Rais alilolitoa juzi mkoani Rukwa na Katavi linaungwa mkono na kila mmoja na hasa watetezi wa haki za wanawake na watoto.

Wakati Rais anawaonya wanaochezea hatima ya watoto, anazungumzia zaidi suala la elimu.

Anakumbusha kuwa serikali inagharamia elimu kila mwezi kwa kutoa mabilioni ya ruzuku na haitakubali fedha zinazokwenda shuleni zisiwanufaisha wasichana.

Anasisitiza elimu kwanza, kwa vile anafahamu kuwa elimu ni moja ya eneo nyeti na muhimu katika kuwawezesha wanawake kumudu maisha yao na za familia zao.

Ndiyo maana anawaonya wanaowadhulumu wasichana na mabinti kuwa taifa haliwezi kuvumilia.

Rais anasema kila mwezi yanatolewa mabilioni kusomesha watoto wake wa kike na wa kiume na kuachana na mienendo inayodunisha jamii.

Anawakumbusha kuwa watoto wadogo 229 wamepata mimba katika mkoa huo, lakini hajasikia wanaume 229 wakiwa wamefungwa jela.

Anaonya kuwa haya si mambo ya kuvumiliwa tena kwa sababu sheria zipo, vyombo vya dola na viongozi wapo na wanatakiwa kuchukua hatua.

Tunaungana na Rais kwa kueleza kuwa si wakati wa kuvumilia anguko hilo la mabinti wawe shuleni au mitaani.

Kama taifa hatuwezi kuisahau mikutano mikubwa ya dunia iliyozungumzia masuala ya ustawi wa wanawake ya Cairo -Misri na Beijing nchini China.

Mkutano wa Beijing ni muhimu kwa taifa hili kwa vile ulisimamiwa na Balozi Getrude Mongela na ajenda zilizozungumzwa humo nyingi ni mchango wake ambao kama taifa tunatakiwa kuuenzi kwa kuwasomesha na kuwaendeleza wanawake.

Kama Rais alivyosema hiyo ni aibu na kuwataka, wabunge, madiwani, viongozi wa dini, mashehe na machifu walisimamie linaleta doa kwenye mikoa yao.

Angalizo hili la Rais ni muhimu kwani elimu pekee ndiyo itakayowahakikishia wanawake maisha bora kwani bila, elimu hakuna maendeleo na ukandamizaji wa watoto na jamii hautakoma.

Kwa Tanzania suala la wanawake na mabinti kuwa nyuma kimaendeleo halina ubishi. Ndiyo maana Rais anasema wasichana wawe kama nyara za serikali kila mmoja awalinda.

Ikumbukwe kuwa kwenye elimu ndiko ambako wanawake na mabinti wako nyuma zaidi. Mathalani, tunapozungumzia idadi ya watoto ambao walitakiwa kuwa shuleni lakini hawapo, wengi watakuwa wasichana.

Tukitaja takwimu za watoto walionyanyaswa, wengi ni wa kike, kadhalika kila jambo litawataja wanawake kuwa ndiyo wanaoumia zaidi.

Kwa hiyo tuungane na Rais kuwalinda na kuwapa wasichana elimu kwani ndiyo dawa pekee ya kuondoa umaskini wa taifa letu.

Kuwasomesha ni kuwahakikishia uwezo mkubwa na nguvu za kutosha zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya maisha yao na ya nchi yao.

Ikumbukwe kuwa ni lazima wanawake kama raia wa taifa hili wawe na afya bora na hiyo iwe sababu nyingine ya kuwawezesha kusoma na kupata elimu bora.

Faida nyingine muhimu kwa taifa inayotokana na elimu ya wanawake ni kuwa na ujuzi, kupata taarifa mbalimbali (information) na kujiamini kwa kila wanalofanya.

Iwe afya ya uzazi, malezi bora na uwekezaji huko ndiko utakakowezesha kuwa na familia na wazazi bora, wafanyakazi mahiri na makini na raia wema.

Tukumbuke kuwa mwanamke aliyeelimika si rahisi kujiingiza katika mambo yasiyo na maadili yanayoangamiza maisha.
Mathalani, kuuza mihadarati na kufanikisha matumizi ya dawa hizo miongoni mwa vijana.

Tunaamini kuwa wanawake wasomi na walioelimika ni watendaji na wachapakazi mahiri ofisini na nyumbani.

Hivyo tuungane na Rais kuwalinda na kuwatetea wasichana mitaani na shuleni.

Habari Kubwa