Tumuunge mkono Samia kupata chanjo ya corona

29Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tumuunge mkono Samia kupata chanjo ya corona

Hatimaye Tanzania imeingia rasmi katika orodha ya mataifa duniani yaliyoanza kuchukua hatua ya kuwapa chanjo raia wake kuwakinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Jana, Samia Suluhu Hassan, aliwaongoza viongozi mbalimbali wa serikali, vyombo vya ulinzi na usalama na dini kupata chanjo hiyo, huku akitaja vigezo sita vilivyomfanya achanje.

Amesema hawezi kuhatarisha maisha yake, huku akijua anaongoza kundi kubwa la watu wanaomtegemea akiwa kama Rais, Amiri Jeshi Mkuu , mama, bibi, mke na mchungaji wa Watanzania.

Rais Samia alichoma chanjo aina ya Johnson & Johnson kwenye bega la kushoto saa 5:56 asubuhi Ikulu jijini Dar es Salaam, mbele ya viongozi mbalimbali wa serikali, huku tukio hilo likirushwa mubashara na vyombo mbalimbali vya habari.

Rais alisema Tanzania haiwezi kupuuza chanjo hiyo kwa kuwa hatuishi peke yetu, tunaishi na mataifa mengine hivyo hatuwezi kuishi kwa kujitenga na dunia inavyoenda, na kwamba haoni hatari ya kuchanja ilihali wanasayansi wa nje na ndani ya nchi wameshajiridhisha kuwa chanjo hiyo ni salama.

Tukio hilo sasa limefungua milango kwa Watanzania kuitumia fursa hiyo kuchanjwa, lengo likiwa ni kujilinda dhidi ya gonjwa hilo hatari, ambalo hadi sasa limeua mamilioni ya watu duniani na wengine wakiugua.

Aidha, gonjwa hilo limeathiri uchumi wa kila taifa, kutokana na shughuli za uzalishaji zikiwamo za viwandani kusimama au kupungua kwa kiwango kikubwa.

Sababu alizozieleza Rais Samia hapo juu kwamba ndizo zilizomsukuma achukue uamuzi wa kuchanja unamshawishi kila Mtanzania mwenye akili timamu na mzalendo kwa nchi yake kuuelewa na kumuunga mkono.

Kumuunga mkono maana yake ni kukubali kwenda kupata chanjo hiyo katika vituo vya huduma za afya ambavyo mamlaka husika zitavitolea maelekezo.

Tunawahimiza na kuwasisitiza wananchi wote wabadili mitazamo yao kwa kukubali kupewa chanjo hiyo kwa lengo la kujilinda na kuwalinda wengine, huku pia wakiendelea kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya maambukizi ya corona.

Tunasema hivyo kwa kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakitoa kauli za upotoshaji kuhusu chanzo za Covid-19 kwamba zina madhara kwa binadamu, hivyo kuwajaza hofu ya kuchanjwa.

Maelezo yanayoendelea kutolewa na wataalamu wa afya, yakiwamo yaliyotolewa naja wakati wa hafla ya uzinduzi wa chanjo hiyo yanadhihirisha bila kuacha shaka yoyote kuhusu usalama, ubora na umuhimu wa chanjo.

Ushauri wetu ni kwamba wananchi wawapuuze wale wote wanaotoa kauli za kuwapotosha kwa kuwa madhara ya corona yanaonekana katika maeneo kadhaa ya nchi.

Kadhalika, tunawahimiza kuzingatia wito wa Rais Samia wa kuwataka Watanzania watakaochanja wasijiachie kwa sababu wapo watu ambao hawajachanja.

Tunatarajia kuona shughuli za kutoa elimu ya corona na uhamasishaji wananchi kuchanja zikifanyika kwa kasi kubwa kupitia uratibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Itakuwa vyema kama viongozi wa dini nao wataelimisha waumini wao na kuwahimiza kupata chanjo.

Habari Kubwa