Tunahitaji kuvumiliana kwenye suala la mipaka

21May 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tunahitaji kuvumiliana kwenye suala la mipaka

KUFUNGA mipaka baina ya nchi jirani kulikofanywa wiki iliyopita kunatajwa kuwa ni jitihada za nchi kudhibiti maambukizo ya corona.

Ilianza kwa Kenya kufunga mpaka wake na Tanzania na kukataza raia na wasafiri kutoka Tanzania kuingia ndani ya taifa hilo.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, alitangaza wiki iliyopita kuwa mipaka ya Tanzania na Somalia itafungwa, isipokuwa tu yataruhusiwa magari ya shehena. Ni kutokana na ongezeko la maambukizo ya corona yanayochangiwa na safari za kuvuka mipaka.

Aidha, tuliyasikia maagizo yake yaliyotolewa wiki iliyopita Mei 16 na haikuishia hapo nchini Zambia Rais Edgar Lungu, alitangaza kufunga mipaka kati ya Tanzania na Zambia kwa maelezo kuwa ni kudhibiti kuenea kwa corona kunakosababishwa na mwingiliano wa raia wa nchi jirani kuvuka mipaka.

Ni jambo lililofanyika na viongozi na kwa Kenya ilikuwa ni lazima kwa madereva kupimwa corona na baadhi waliviambia vyombo vya habari vya kimataifa kuwa walilazimishwa kupimwa kwa kutumia kipimo kimoja na kwamba iwapo wana maradhi watarudishwa nyumbani mara moja.

Madereva wa Tanzania waliokwenda Rwanda walifanyiwa pia mambo ambayo hayakupendeza masikioni kwani walivieleza vyombo hivyo kuwa wanapoonekana mitaani, raia waliziba nyuso zao na kuwatuhumu kuwa wanawasambazia corona.

Kwa ujumla hadithi za kufunga mipaka hazikuwapendeza wengi na serikali ililipokea na kulifanyia kazi ndipo Mkuu wa Mkoa wa Tanga akatangaza kufunga mpaka wa Horohoro na kuwa mwanzo wa malalamiko.

Aidha, mkoani Mara na Arusha ilifungwa pia, serikali mikoani humo ikieleza kuwa itahusika na kuzuia malori na wasafiri kutoka Kenya ili kudhibiti usambaaji wa ugonjwa unaoanzia mpakani.

Tumekisikia kilio cha Kenya na kutafakari kile madereva wa Tanzania walichosema na kufuatilia taarifa za usafirishaji katika mataifa mengine nje ya Afrika na kuona kuwa suala la biashara na usafirishaji wa shehena na abiria linahitaji kuridhiana na si kukurupuka ambako mara nyingi huishia kuumizana.

Kwa mataifa ya Afrika Mashariki, Nchi za Jukuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na hata masuala ya kiukanda na mtangamano kwa ujumla tunakumbushana kuwa kila mmoja anamtegemea mwenzake bila kujali kuwa tupo ndani ya mipaka yetu.

Ni vyema kutendeana kwa upole, haki na ikibidi kuwasiliana na kuweka taratibu zisizoumiza kwani kukomoana hakusaidia mtu au taifa lolote.

Ikumbukwe kuwa kuwakwamisha madereva wa Tanzania na shehena zao ndani ya Kenya au Rwanda na hata kuwarudisha nyumbani wenye corona au kuwapima na kipimo kimoja cha kutumbukiza pamba puani au kooni ili kupata ute wenye virusi ni jambo linalostahili kuomba radhi.

Tukizungumzia kutumia kipimo kimoja ni kinyume cha haki za binadamu na kama ni kweli ni kuwaambukiza watu magonjwa kwa makusudi. Ndiyo maana tunasema usimtendee mwenzako usilotaka kutendewa naye.

Kutaarifiwa kuwa unaumwa corona rudi kwenu ukatibiwe ni kwenda kinyume na ubinadamu. Suala la shehena kuzuiliwa mpakani haijalishi ni ya kutoka taifa gani. Ni biashara. Kuna muda unaopotea, gharama inayopatikana na mwisho kinachojiri ni hasara.

Kinachotokea mpakani sasa baada ya Tanzania kufunga mpaka ni udhihirisho kuwa mkuki kwa mnyama ni mtamu lakini kwa binadamu ni mchungu.

Tukumbuke mataifa yetu yanategemeana kiuchumi, kibiashara na hata kujikimu. Ni wazi bidhaa za vyakula na mahitaji muhimu ya binadamu yanaweza kutoka upande mmoja wakati vitu vya viwandani vinazalishwa kutoka nyingine. Hivyo viongozi tuheshimiane na kuacha ubabe.

Habari Kubwa