Tunahitaji teknolojia mbadala barabarani

15Mar 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tunahitaji teknolojia mbadala barabarani

KILA anayeingia Dar es Salaam anafahamu jinsi wakati mwingi kunavyokuwa na ugumu wa kuendesha chombo cha usafiri kwenye barabara za jiji hili

Hata hivyo, ni jukumu la kila dereva na abiria kulinda maisha kwa kuzuia ajali za barabarani, ziwe zinazotokana na kutembea au kuwa kwenye vyombo vya moto.

Licha ya ugumu huo, serikali na wadau wanajitahidi kuhakikisha kila wakati wasafiri na watumia barabara wanalindwa na kuwa salama.
Kila mara unapofanyika ukaguzi na ukamilishaji wa jukumu la wiki ya nenda kwa usalama barabarani, ulinzi na usalama zaidi ni mambo yanayozingatiwa kulinda maisha ya polisi, abiria, vyombo na watumia barabara kwa ujumla.

Hata hivyo, tunaona kuwa tunahitaji kuwalinda zaidi na kutoa kipaumbele cha usalama kwa maofisa usalama wa barabarani, wanaoongoza magari kwa kuwa kama ilivyo vigumu kuendesha, ndivyo inavyokuwa taabu pia kwa wasimamizi hawa wa barabarani kufanyakazi zao kwa usalama hasa wanapoongoza magari asubuhi, jioni na usiku.

Tunashauri kuwa wakati huu zinapojengwa barabara mpya jijini Dar es Salaam na miji mingine zibuniwe mbinu za kisasa za kuwawezesha trafiki kufanyakazi zao kwa usalama na weledi zaidi kwani kinachojiri leo kinawaweka kwenye hatari kubwa zaidi.

Umma utakubaliana nasi kuwa, wanaoendesha magari wana ufahamu tofauti, wapo wanaojua wanachokifanya, wengine hawaelewi wala hawazingatii sheria za barabarani, wapo wagonjwa wa akili, wengine inawezekana wana msongo wa mawazo na wamechanganyikiwa au inawezekana baadhi wana taharuki kutokana na maisha au mazingira na mikasa inayowapata wakati huo.

Wapo wanaendesha kasi kupindukia, kuna wengine wenye magari mabovu, wapo baadhi wasiojua kuendesha na kwa ujumla barabarani panakuwa si mahali salama kwa yeyote.

Kwa hiyo wote hawa wanapokuwa barabarani kuanzia wenye magari makubwa kwa madogo, pikipiki, baiskeli, mikokoteni na bajaj, wanayaweka mazingira ya trafiki hatarini zaidi na maisha kuwa rehani kila wakati.

Ndiyo maana tunazishauri mamlaka za kitafiti na kitaalamu kutafuta mbinu za kisasa zaidi za kuwasaidia trafiki kufanyakazi zao kwa usalama na weledi kuliko kuacha mambo kubaki kama yalivyo leo.

Tunafikiria zaidi kutokana na polisi hao kufanyakazi katika mazingira magumu na wakati mwingine kulazimika kusimama katikati ya barabara na kuhatarisha maisha yao.

Jana gazeti hili liliandika taarifa za kusakwa kwa dereva wa bajaj aliyemgonga na kumjeruhi polisi wa barabarani mkoani Shinyanga.
Hili lituguse sote kuwa polisi hawa wanaumia, maisha yao yako hatarini. Ni wakati wa kutumia mbinu mpya na mikakati ya kisasa ya kuokoa maisha ya trafiki badala ya kuwaacha kufanyakazi katika mazingira magumu kwenye barabara zetu.

Iwapo tunajiridhisha kuwa wingi wa magari barabarani haudhibiti kwa kutumia taa ni vyema sasa kujiongeza zaidi na kujipanga kwa kuangalia mifano kwenye nchi nyingine ambazo nazo zilikuwa na tatizo la kuongoza magari kwa kutumia taa za usalama.

Tunatoa ushauri huu kwa sababu dunia imebadilika kitekinolojia na vyombo vya usafiri navyo vimebadilika vingi vinatumia utaratibu wa kujiendesha vyenyewe au teknolojia ya ‘automatic’ ambayo ndiyo iliyoko kwenye uendeshaji wa mitambo viwandani na magari.

Tunashauri wataalamu wa vyuo vikuu UDSM, Chuo cha Usafirishaji, Taasisi za Ufundi na Teknolojia za Dar es Salaam na Arusha pia zihusishwe kumaliza tatizo hili.

Tunashauri wadau wengine wenye utaalamu wa kiuhandisi wajitokeze na kushauriana na mamlaka za kitafiti na Jeshi la Polisi ili kupata teknolojia mbadala inayolinda maisha ya trafiki wanaoongoza magari barabarani.

Habari Kubwa