Katika kutafakari kwanini wanafunzi wanashindwa mitihani na kuamua kutukana kuna majibu mengi lakini kuna mambo mengi yanayochangia wanafunzi kufeli mitihani hasa zama hizi ikiwa ni pamoja na maandalizi duni.
Huenda wanaofanya hayo ni wale waliokosa cha kuandika kutokana na kutokujiandaa kikamilifu badala yake wakaamua kutukana na kuchafua karatasi kwa kuandika matusi hivyo kuambulia sifuri pamoja na kufutiwa matokeo.
Ikumbukwe kuwa watoto wa zama hizi wanahitaji maandalizi na wazazi pamoja na walezi kuwafuatilia kwa sababu wanafanya mambo mengi lakini yanayoambatana na utandawazi. Tatizo la utandawazi lipo mijini na vijijini kwani kote kuna mitandao ya simu, kompyuta na picha za video zinaonekana bila mipaka.
Wazazi, walimu na walezi wanabaki na jukumu la kufuatilia iwapo watoto wanasoma, kulala, kula na kufanyakazi za nyumbani na michezo inayopasa badala ya kutizama televisheni , mitandao ya kijamii, kucheza ‘gemu’ au michezo ya kompyuta kwenye simu za wazazi, marafiki na walezi wao au kuangalia mambo mengine kwenye mitandao ya kijamii ambayo huenda yanawavuta zaidi kuliko kujifunza.
Japo wanaonekana wanasoma lakini huenda wanavutika zaidi na mambo ya ziada kuliko kuhangaika na mitihani ndiyo maana wanaamua kuandika matusi na kutukana badala ya kutoa majibu sahihi.
Pamoja na kwamba hatuwalaumu moja kwa moja kwa kutukana kwa sababu hatujui sababu ya kufanya hivyo tunaona kuwa walichofanya si busara kwa kuwa watoto wa leo wamebarikiwa na wamerahisishiwa kusoma. Wengi wanapata vitini kutoka kwenye mitandao ya kijamii na intanet.
Kuna baadhi wanasoma mafunzo ya ziada (tuition) bila kujali kuwa wapo mijini au vijijini hivyo walitakiwa kusaidiana na wazazi au walezi pamoja na walimu kujibu mitihani kikamilifu kwani lengo la kumtahini mwanafunzi ni kuona na kupima uelewa wake kwenye somo husika na darasa alipofikia.
Tuna wasiwasi kuwa huenda wanafunzi wasiosoma kikamilifu , wala wasiopitia mitihani ya miaka ya nyuma, au wasioandika nots au vitini vya mwalimu , wala kusoma vitabu, na kufanya mazoezi ndiyo wanaotukana badala ya kujibu maswali.
Ndiyo maana tunasema ni jukumu la wazazi na walezi kupitia na kuangalia kilichoko kwenye ripoti za mwalimu wa darasa zinazotolewa kila mwisho wa mwaka ili kujua namna ya kuwasaidia watoto wetu.
Mazingira ya sasa ni mabovu wanafunzi wanajiingiza kwenye makundi mabaya ya kihalifu ya kuvuta bangi, kujamiiana, kutumia mihadarati, ulevi na hata wizi. Yote haya wazazi wanayafahamu. Ndiyo maana ripoti za waalimu za mwisho wa mwaka ni muhimu kuzisoma na kufuatilia mwenendo wa mtoto wako badala ya kusubiri hadi kuibuliwa kuwa anatukana badala ya kutoa majibu sahihi ya mitihani.
Ni imani yetu kuwa wazazi na walezi, Necta, pamoja na walimu watachunguza sababu ya kujibu matusi kwenye mitihani na kuwafahamisha Watanzania sababu ili iwe fundisho na karipio kwa wahusika na pia wale wasiowajibika kusaidia watoto kujimudu na kujibu mitihani yao.
Wazazi na walezi pamoja na walimu wana jukumu la kufuatilia na kujua kwanini baadhi ya wanafunzi wanaamua kutukana badala ya kujibu mitihani kwani wakati mwingine kufaulu mitihani si kusoma pekee. Inawezekana lawama zikiwashukia waalimu kwa kuuliza hivi walimaliza silabasi? Waliwafundisha kikamilifu wanafunzi kwenye ‘ topiki’ muhimu ambazo ndizo maswali yanakotoka kila wakati?